Uchaguzi wa bunge Iran | Matukio ya Kisiasa | DW | 13.03.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Uchaguzi wa bunge Iran

Huenda ukaimarisha nafasi ya Rais Mahmoud Ahmadinejad kuweza kuchaguliwa tena kwa kipindi cha pili mwaka ujao.

Rais wa Iran Mahmoud Ahmadinejad.

Rais wa Iran Mahmoud Ahmadinejad.

Wachambuzi wanasema hata kama wafuasi wake wa msimamo mkali watafanya vibaya katika uchaguzi huo Ijumaa (14.02.08), bado ni mapema kumkatia tamaa kiongozi huyo.

Baada ya juma moja la kampeni nzito, wairan milioni 44 wenye haki ya kupiga kura wataweza kuwachagua wabunge kutokana na makundi mawili ya wahafidhina na kundi moja la wapenda mageuzi, ili kuwaakilisha katika bunge la viti 290. Serikali inatarajia wapiga kura watajitokeza kwa wingi, ili kuwadhihirishia Wamarekani na "maadui "wengine kwamba mfumo wao ni mashuhuri.

Wairan wengi wameakasirishwa na kuongezeka kwa ughali wa maisha na ukosefu mkubwa wa ajira, lakini jibu halitotokana na kuwachagua wakosoaji wa Ahmadinejad wanaopendelea mageuzi, kwa sababu baraza kuu la uongozi ambalo huwa halichaguliwi, limewaengua wengi katika orodha ya wagombea.

Mchambuzi mmoja wa Kiiran wa masuala ya kisiasa, anasema" kuna hali ya kutoridhika juu ya sera ya kigeni na ughali wa maisha, lakini suala la nuklea mpaka sasa limeinufaisha serikali. Hoja nyengine inayotajwa kuwa itainufaisha katika uchaguzi huo ni kwamba huenda wakosoaji wake wengi wakajizuwia kupiga kura na kubaki majumbani.

Ahmedinejad pia ana wapinzani upande wa wahafidhina wanaowania nafasi ya urais na kuwania kuungwa mkono na kiongozi mkuu Ayatollah Ali Khamenei kwa ajili ya uchaguzi ujao wa rais 2009. Ni uungaji mkono wa Khamnei kwa Ahmadinejad unaoangaliwa uliokua muhimu katika ushindi wa kushangaza wa rais huyo 2005.

Hivi karibuni Ayatollah Khamenei amemwagia sifa hadharani Ahmedinejad mwenye umri wa miaka 51 kwa msimamo wake katika mgogoro na nchi za magharibi kuhusu mradi wa nuklea wa Iran, ingawa baadhi ya wahafidhina wameukosoa msimamo mkali uliosababisha umoja wa mataifa kuweka sehemu ya tatu ya vikwazo dhidi ya Iran mnamo mwezi huu.

Ni Kiongozi mkuu wa Iran Khamenei mwenye usemi wa mwisho kuhusu rais panapohusika na masuala kama nuklea, mafuta na sera ya kigeni na sio bunge.

Wakati anacheza karata ya kuwa kama mpatanishi, lakini kiongozi huyo aliwasaidia wahafidhina kuchukua tena mamlaka waliyoyapoteza wakati wa mihula miwili ya uongozi wa Mohamed Khatami, mwanasiasa wa msimamo wa wastani,aliyependelea zaidi kuweko na uhuru zaidi wa kijamii na kisiasa nyumbani na pia mazungumzo na ulimwengu wa nje.

Mbali na uchaguzi wa leo kutazamwa kama ishara ya kupima umashuhuri wa rais Ahmadinejad, iwapo unafifia au la, lakini pia utaashiria imani walionayo wa Iran kama kweli anatimiza ahadi alizotoa kuhakikisha mafuta ya Iran yanaunufaisha umma wa nchi hiyo.

Kundi la wahafidhina United Front lina wanaomuunga mkono bna wanaomkosoa Ahmadinejad, lakini wote wasisitiza juu ya uaminifu wao mbele ya maadili ya mapinduzi ya Kiislamu. Kundi hilo linaungwa mkono na wanasiasa wawili walioshindwa na Ahmedinejad 2005-Ali Larijani aliyiuzulu kama mjumbe mkuu katika mzungumzo kuhusu mradi wa nuklea mwaka jana kutokana na tafauti za maoni na rais huyo, na meya wa jiji la Teheran Mohamed Baqer Qaliabaf.

Bila shaka ughali wa maisha ukielezwa rasmi kufikia asili mia 19.2 na ukosefu wa kazi katika kiwango cha 10.7 asili mia, serikali ya Ahmadinejad inahofia huenda ikaadhibiwa na wapiga kura.


 • Tarehe 13.03.2008
 • Mwandishi Abdulrahman, Mohamed
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/DNvW
 • Tarehe 13.03.2008
 • Mwandishi Abdulrahman, Mohamed
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/DNvW
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com