1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi mkuu wafanyika nchini Kenya

Josephat Charo28 Desemba 2007

Raila Odinga amkaba koo rais Mwai Kibaki

https://p.dw.com/p/ChSv
Kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila OdingaPicha: dpa - Report

Kuhusu uchaguzi huko nchini Kenya, gazeti la Neuer Zürcher Zeitung lilisema licha ya machafuko ya hapa na pale wakati wa kampeni, uchaguzi nchini Kenya umefanyika kwa amani. Foleni ndefu wa wapigaji kura waliosubiri kwa muda mrefu kuwachagua viongozi wanaowataka zilidhihirisha wazi idadi kubwa ya wapigaji kura iliyojitokeza kushirikia katika zoezi zima la uchaguzi.

Gazeti la Frankfurter Allgemeine Zeitung lilisema siasa nchini Kenya imekabiliwa na ufisadi. Mhariri wa gazeti hilo alisema aliyedhani kwamba mgombea wa chama cha PNU, bwana Mwai Kibaki, angeweza kushinda alikuwa akijihadaa kwa kuwa kiongozi huyo hakutimiza ahadi alizozitoa kabla kuchaguliwa rais. Alichofaulu kukifanya ni kuongeza mishahara ya walimu na marupurupu ya viongozi wa serikali kwa asilimia 16.

Wakenya milioni 14 walitakiwa kumchagua rais mpya, bunge na madiwani katika kinyang´anyiro kikali ambacho rais Kibaki hakuwa na uhakika wa kushinda.

Gazeti la Die Welt kuhusu uchaguzi wa Kenya lilisema ulikuwa mashindano kati ya chungwa na ndizi. Mgombea wa chama cha PNU, Mwai Kibaki, alikabwa koo na mgombea wa chama cha ODM bwana Raila Odinga. Nalo gazeti la Berliner Zeitung likasema kwamba Wakenya hawakutaka kuwachagua wabunge wazee na mafisadi. Mhariri wa gazeti la Tageszeitung alisema upinzani wa chungwa ulikuwa mkali dhidi ya rais Mwai Kibaki.

Mada ya pili inahusu hukumu ya miaka minane na kazi ngumu dhidi ya wafanyakazi wa shirika la misaada la Zoe´s Arch la Ufaransa waliokabiliwa na kesi ya kutaka kuiba watoto. Gazeti la Neuer Zürcher Zeitung lilisema kesi iliyowakabili wafanyakazi wa kampuni hiyo sasa imemalizika huko mjini Ndjamena Chad. Mahakama ya mjini Ndjamena iliwahukumu wafanyakazi hao wa kampuni ya Zoe´s Arch kwa kuwa na njama ya kuwateka nyara watoto 103 wa Chad. Raia mmoja wa Chad na mmoja wa Sudan waliohusika katika njama hiyo walihukumiwa kifungo cha miaka minne kila mmoja. Washukiwa wengine wawili raia wa Chad waliachiwa.

Mhariri wa gazeti la Neuer Zürcher Zeitung lilisema shirila la Zoe´s Arch ambalo lilikuwa halijulikani, lilieleza kuwa lilijaribu kuwaokoa watoto mayatima kutoka eneo linaliokabiliwa na vita la Darfur kuwapeleka Ufaransa. Polisi wa Chad mjini Abeche waliowapeleka watoto hao katika uwanja wa ndege wa mjini Ndjamena ambako ndege ilikuwa ikiwasubiri kuwapeleka nchini Ufaransa walishuku. Na baada ya kukamatwa wafanyakazi wa shirika la Zoe´s Arch ilidhihirika kwamba watoto wengi walitokea Chad na wala sio Darfur na wengi wao walikuwa na wazazi.

Gazeti la Frankfurter Allgemeine Zeitung liliripoti juu ya kuuwawa kwa watalii wanne raia wa Ufaransa nchini Mauratania mkesha wa kuamkia sikukuu ya Krismasi. Familia ya kifaransa ya watu watano ilishambuliwa wakati ilipokuwa ikifurahia mandhari karibu na mji wa Aleg. Wanne kati yao waliuwawa lakini baba wa familia hiyo akaponea chupuchupu huku akipata majeraha ya risasi mguuni mwake. Baba huyo alisafirishwa hadi hopitali ya mjini Dakar nchini Senegal mnamo Jumatano iliyopita. Maafisa wa Mauritania walidokeza Jumatano iliyopita kwamba mauaji ya wafaransa hao yalifanywa na kundi la salafisti, GSPC, ambalo ni kitengo cha kundi la al Qaeda katika eneo la Maghreb. Mnamo mwaka wa 2003 kundi hilo liliwateka nyara watalii 32 kutoka Ujerumani, Uholanzi na Uswisi hatua ambayo ilizusha hisia kali katika ngazi ya kimataifa.

Nalo gazeti la Neuer Zürcher Zeitung kuhusu mada hii lilisema wanamgambo waliwaua watalii wa kifaransa kusini mwa Mauritania Jumatatu iliyopita, yapata kilomita 70 kutoka mpaka wa Senegal. Watalii hao walikuwa ndani ya gari wakisafiri kuelekea Burkina Faso kupitia Mali. Walishambuliwa na wanaume watatu wakati walipokuwa ufuoni na kuuwawa isipokuwa baba watoto, ambaye alipigwa risasi mguuni. Baadaye baba huyo alisafirishwa Ufaransa kwa matibabu kupitia Senegal.