Uchaguzi FIFA leo, Blatter ′aandamwa′ | Michezo | DW | 01.06.2011
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Michezo

Uchaguzi FIFA leo, Blatter 'aandamwa'

Licha ya uchaguzi wa Shirikisho la Kandanda Duniani (FIFA) kutazamiwa kufanyika leo (01.06.2011) na Sepp Blatter anayegombea tena wadhifa wa urais kuzidi kujipapatua, tuhuma za rushwa zazidi kulielemea Shirikisho hilo.

Rais wa FIFA, Sepp Blatter

Rais wa FIFA, Sepp Blatter

Kila dakika inayopita panatolewa madai dhidi ya wajumbe wa Bodi ya Utendaji ya FIFA. Madai haya juu ya rushwa yamekuwa yanakikiandama chama hicho cha mpira duniani kwa miaka kadhaa sasa.

Matukio ya hivi karibuni yameonyesha kwamba viongozi wa FIFA hawaujali mchezo wa mpira au hadhi ya Shirikisho lao, bali wanajali maslahi yao kibinafsi.

Lakini licha ya madai hayo kutolewa ndani na nje ya Shirikisho hilo, Blatter amesema kuwa FIFA haikabiliwi na mgogoro wowote na juzi aliwapa waandishi habari changamoto ya kulifasili neno mgogoro.

Blatterr aliwaambia waandishi hao kwenye makao makuu ya FIFA mjini Zürich kwamba hamna mgogoro ndani ya FIFA. Ameeleza kuwa yeyote aliyeiona fainali ya Kombe la Mabingwa wa Ulaya, basi atapaswa kutoa sifa.

Makamo Rais wa FIFA na Rais wa CONCACAF, Jack Warner

Makamo Rais wa FIFA na Rais wa CONCACAF, Jack Warner

Rais huyo wa FIFA alisisitiza kwa waandishi habari kwamba FIFA inakakabiliwa na matatizo, lakini haina mgogoro.

Hata hivyo, Blatter aliyakwepa maswali ya waandishi wa habari juu ya madai ya rushwa yaliyotolewa dhidi ya FIFA. Baada ya mgongano na waandishi wa habari, aliamua kuondoka na kuwaacha waandishi wakiduwaa.

Hata hivyo, wachunguzi wanaamini kwamba FIFA imo katika dimbwi la mgogoro. Viongozi wake wawili wa ngazi za juu, Mohammed Bin Hamman, ambaye ni rais wa Chama cha Kandanda cha Asia, na makamu wa rais wa FIFA, Jack Warner, wamesimamishwa. Uchaguzi wa rais unatarajiwa kufanyika akiwapo mgombea mmoja tu - Blatter mwenyewe.

Viongozi hao wamesimamishwa kwa madai kwamba wamewahonga wajumbe wa Carrebean ili wamuunge mkono Bin Hamman ambaye kabla ya kusimamishwa alitaka kugombea urais wa FIFA.

Mkuu wa Shirikisho la Soka la Asia, Mohammed bin Hammam

Mkuu wa Shirikisho la Soka la Asia, Mohammed bin Hammam

Kwa upande wao, Bin Hamman na Warner, wanadai kwamba Blatter alikuwa anajua kwamba makosa yalikuwa yanatendeka ndani ya FIFA, lakini hakuchukua hatua zozote.

Warner amedai kwamba Chama cha Kandanda cha Marekani na Karibian kilipewa dola milioni moja za kuzitumia jinsi kilivyotaka .

Madai juu ya rushwa yanayoikabili FIFA yamewafanya wafadhili muhimu wa Shirikisho hilo waingiwe wasiwasi. Msemaji wa kampuni ya Coca-Cola ameeleza kuwa madai yanayotolewa sasa dhidi ya FIFA yanahuzunisha na yanaathiri sifa ya michezo.

Hii siyo mara ya kwanza kwa FIFA kukabiliwa na kashfa kama hii.

Mwandishi: Sarah Faupel/ZAR
Tafsiri: Abdu Mtullya
Mhariri: Josephat Charo