Uamuzi wa Trump waendelea kulaaniwa Magazetini | Magazetini | DW | 31.01.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Magazetini

Uamuzi wa Trump waendelea kulaaniwa Magazetini

Uamuzi wa rais wa Marekani Donald Trump wa kuwazuwia baadhi ya waislam kuingia nchini humo, uchaguzi wa mchujo Ufaransa na homa ya uchaguzi Ujerumani ni miongoni mwa mada magazetini

Tunaanzia Marekani ambako uamuzi wa rais Donald Trump unaowazuwia kuingia nchini humo wakaazi wa nchi saba za Kiislamu kutoka mashariki ya kati na pia Afrika unaendelea kugonga vichwa vya habari humu nchini. Gazeti la "Der neue Tag" la mjini Weiden linaandika: "Suala kama uamuzi huo utalifikia lengo lake, au kama unakwenda kinyume na katiba au kama utaipatia madhara ya muda mrefu Marekani, Trump haoni kama ni muhimu. Kiongozi mpya wa Ikulu ya Marekani White House anajionyesha kuwa kiongozi mkakamavu. Cha hatari katika sera zake za kuweka saini, ni ile hali kwamba zinawavutia wengi wanaoamini majibu ya haraka yanawezekana katika siasa. Lakini matamshi si ufumbuzi. Hakuna kinachoonyesha kwamba marufuku ya kibaguzi ya kuingia Marekani yatapita katika korti za Marekani.

Mageuzi au hatua za kuirejesha nyuma Ufaransa?

Uchaguzi wa mchujo wa chama cha kisoshalisti nchini Ufaransa umempatia Benoît Hamon nafasi ya kugombea kiti cha rais uchaguzi mkuu utakapoitishwa mwezi April mwaka huu. Mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 49 ni miongoni mwa wakosoaji wakubwa wa rais Francois Hollande chamani. Gazeti la "Mannheimer Morgen" linachambua matokeo ya uchaguzi huo wa mchujo na kuandika: "Yadhihirika kana kwamba wapiga kura wa Ufaransa wanataka kitu kimoja tu: Mageuzi. Mfarakano haupo tena kati ya wafuasi wa mrengo wa kushoto na wale wa mrengo wa kulia, bali kati ya wazee na vijana. Suala watu wanalojiuliza ni kama Emmanuel Macron ndie atakaeleta mageuzi ya maana. Au kama mageuzi hayo yanaweza kupatikana kupitia Marine Le Pen mwenye kufuata sera za kibaguzi , mtengano na kero. Suala hapa ni jee  wapiga kura wa Ufaransa wanataka kusonga mbele au kurudi nyuma?

Nani kati ya Martin Schulz na Angela Merkel ataibuka na ushindi?

Mada yetu ya mwisho magazetini inaturejesha hapa hapa Ujerumani ambako homa ya uchaguzi mkuu imeshaanza kupanda. Baada ya chama cha Social Democratic-SPD kumchagua spika wa zamani wa bunge la Ulaya Martin Schulz kushindana na Angela Merkel, wahariri wanajiuliza eti nani ni nani kati yao ? Gazeti la "Rhein-Necker-Zeitung" linaandika: "Schulz anawika kule ambako Merkel amedhoofika. Schulz anaaminika-sawa na anavyoaminika kansela Merkel. Na ni mpya angalao kwa wale ambao hawakuwa wakifuatilizia siasa za Umoja wa Ulaya. Lakini hayo pekee yanatosha? Na yatoshe kwanini? SPD wameapa kukifikia upya kiwango cha asili mia 30. Ni lengo la fakhari lakini si rahisi kulifikia. Na ili kujikingia wingi wa kura kuvipita vyama ndugu vya CDU/CSU, SPD watahitaji sauti za wafuasi wa chama cha FDP na pia wa Chaguo Mbadala kwa Ujerumani AfD. Na hapo ndipo dhana zinapofikia kikomoni.

Mwndishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri: Iddi Ssessanga