Marekani imealikwa katika mkutano wa Ulaya kuijadili Ukraine
11 Desemba 2025
Trump hakueleza wazi Iwapo Marekani itashiriki mkutano huo utakaojadili vita vya Ukraine.
Rais huyo wa Marekani amesema amezungumza kwa njia ya simu na Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz, Waziri Mkuu wa Uingereza Kier Starmer na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron kuhusu hali katika taifa hilo linalokabiliwa na vita.
"Tumezungumza na viongozi wa Ufaransa, Ujerumani na Uingereza. Wote hawa ni viongozi wazuri sana na marafiki zangu na tulijadili Ukraine kwa maneno mazito kidogo, kwa hiyo tutaona kitakachotokea. Namaanisha tunasubiri kusikia majibu."
Trump amegusia kuwa katika mazungumzo yao kulikuwepo na mvutano kidogo lakini hakufafanua zaidi huku akitoa wito wa Uchaguzi kufanyika Ukraine.
Hapo jana Rais Zelensky alisema yuko tayari kuitisha uchaguzi ndani ya siku 60 hadi 90, hata wakati nchi yake ikiwa vitani, iwapo Mrekani na Ulaya zitamuhakikishia usalama katika mazingira yaliyopo.