1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump asema Ulaya ni dhaifu na inaelekea kuporomoka

10 Desemba 2025

Rais wa Marekani Donald Trump ameikosoa Ulaya na kuitaja kuwa "inayoporomoka na dhaifu" katika masuala ya uhamiaji na vita vya Ukraine. Ametoa shutuma hizo katika mahojiano yake aliyoyafanya Jumanne na jarida Politico.

https://p.dw.com/p/553ds
Donald Trump ameishutumu Ulaya kuwa ni dhaifu na inazidi kuporomoka
Rais wa Marekani Donald TrumpPicha: Jonathan Ernst/REUTERS

Katika mahojiano yaliyofanyika Jumatatu na jarida hilo la Marekani, Trump amesema sera za mataifa ya Ulaya kuhusu uhamiaji ni janga kubwa. Ameongeza kuwa licha ya nchi hizo kutaka kuwa sahihi kisiasa kupitia sera hizo matokeo yake yake zinazidi kuwa dhaifu.

Trump pia ameyakosoa mataifa ya Ulaya kuhusu mzozo wa Ukraine wakati tofauti zikizidi kuongezeka kuhusu mpango wa Marekani wa kuvimaliza vita hivyo.

Katika mpango wa Trump unaolenga kuvimaliza vita dhidi ya Ukraine, Ulaya ina hofu kuwa Ukraine italazimika kuipa Urusi iliyoanzisha vita dhidi yake mwaka 2022 sehemu ya eneo lake.

Hayo yanaendelea wakati viongozi wa Ulaya wakikaribia kupata suluhisho la namna ya kuifadhili Ukraine katika suala la ulinzi dhidi ya Urusi kwa mwaka 2026 na 2027. Kulingana na Rais wa Baraza la Ulaya Antonio Costa makubaliano kuhusu ufadhili huo yatapaswa kuungwa mkono na asilimia kubwa ya mataifa wanachama.

Ulaya, inatafuta namna ya kutumia dola bilioni 244 zinazotokana na mali za Urusi zilizo Ulaya kwa ajili ya kuisaidia Kyiv.

Mjadala wa kuzitumia mali za Urusi zinazoshikiliwa Ulaya

Makubaliano ya namna ya kuzitumia mali hizo yanahitaji hakikisho la wanachama wote wa Ulaya kwamba watahusika katikatika athari zozote zitakazojitokeza kama Urusi itafanikiwa kushinda kesi kama itaushtaki Umoja wa Ulaya.

Umoja wa Ulaya unafanya jitihada za namna ya kuisaidia zaidi Ukraine
Makao makuu ya Umoja wa Ulaya, UbelgijiPicha: Nicolas Economou/NurPhoto/IMAGO

Ukraine inakabiliwa na upungufu wa misaada ya kijeshi tangu mwanzoni mwa nusu ya pili ya mwaka huu baada ya michango ya Ulaya kushindwa kujaza mwanya uliotokana na Marekani kusitisha misaada yake kwa Kyiv.

Katika hatua nyingine, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema yuko tayari kuitisha uchaguzi ndani ya siku 60 hadi 90 hata wakati huu taifa lake likiwa vitani. Amesema yuko tayari kufanya hivyo iwapo Mrekani na Ulaya zitamuhakikishia usalama.

Akizungumza na waandishi wa habari Jumanne, Zelensky ameongeza kuwa hata hivyo hatua hiyo itahitaji mabadiliko ya sheria ya uchaguzi. Ameeleza kuwa ameshawaomba wabunge wa chama chake kuandaa mabadiliko yoyote yatakayohitajika Ukraine haijafanya uchaguzi wowote tangu ilipovamiwa na Urusi mwaka 2022.