1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Mubashara
MigogoroKimataifa

Trump akutana na washauri kuamua kuhusu makubaliano ya Iran

Iddi Ssessanga AP, DPA, RTRE, AFP
Imechapishwa 28 Mei 2026ilisahihishwa mwisho 29 Mei 2026

Rais Donald Trump amesema anakutana na wasaidizi wake ili kufanya uamuzi wa mwisho kuhusu makubaliano ya kuongeza muda wa usitishaji mapigano na Iran huku mazungumzo ya nyuklia yakiwa mezani. DW na taarifa za hivi punde.

https://p.dw.com/p/5ES6E
Marekani, Washington D.C. 2026 | Donald Trump akiongoza kikao cha Baraza la Mawaziri katika Ikulu ya White House
Trump amesema amekutana na washauri wake katika Chumba cha Dharura cha Ikulu ya White House kujadili makubaliano hayo.Picha: Samuel Corum/AdMedia/IMAGO
Ruka sehemu inayofuata Unachohitaji kujua

Unachohitaji kujua

  • Rais Donald Trump anakutana na washauri kuamua kuhusu makubaliano ya Iran
  • Ripoti ya UN yavituhumu vikosi vya usalama vya Israel kwa ukatili wa kingono Gaza
  • Maafisa wa Lebanon na Israel wanatarajiwa kufanya mazungumzo katika makao makuu ya Pentagon nchini Marekani
  • Mkutano huo unafanyika baada ya Israel na Lebanon kukubaliana kusitisha mapigano mwezi Aprili
  • Israel imeongeza mashambulizi yake ya anga dhidi ya maeneo ya Hezbollah mashariki na kusini mwa Lebanon wiki hii
  • Makamu wa Rais wa Marekani JD Vance amesema makubaliano kati ya Washington na Tehran bado
  • Wajumbe wa Marekani na Iran wanaripotiwa kukubaliana kuhusu masharti ya makubaliano ya usitishaji mapigano

Haya ndiyo maendeleo ya hivi punde kutoka Mashariki ya Kati

Ruka sehemu inayofuata Rais Trump anakutana na washauri wake kuamua kuhusu makubaliano ya Iran
29 Mei 2026

Rais Trump anakutana na washauri wake kuamua kuhusu makubaliano ya Iran

Rais wa Marekani Donald Trump amesema yuko katika hatua ya kufanya uamuzi wa mwisho kuhusu iwapo ataidhinisha makubaliano ya kuongeza muda wa usitishaji mapigano kati ya Marekani na Iran.

Trump amesema amekutana na washauri wake katika Chumba cha Dharura cha Ikulu ya White House kujadili makubaliano hayo, ambayo kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari vya Marekani, tayari yamekubaliwa kwa kiwango cha awali na wajumbe wa pande zote mbili.

Makubaliano hayo yanatarajiwa kuongeza muda wa usitishaji mapigano kwa siku 60 na kufungua njia kwa mazungumzo mapya kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran.

Katika ujumbe wake, Trump amesisitiza kuwa Iran lazima ikubali kutotengeneza silaha za nyuklia na kufungua tena njia za usafirishaji wa meli katika Mlango Bahari wa Hormuz.

Aidha amesema hakuna fedha zitakazotolewa kwa Iran kwa sasa, huku akiongeza kuwa baadhi ya masuala muhimu bado hayajakubaliwa kikamilifu. Hata hivyo, hadi sasa haijabainika wazi iwapo Tehran imekubali masharti yote yaliyowekwa na Washington.

Marekani, Washington D.C. 2026 | Rais Donald Trump akiongoza kikao cha Baraza la Mawaziri katika Ikulu ya White House
Rais Trump amesema Marekani itakabidhiwa urani ya Iran iliyorutubishwa kwa ajili ya kuharibiwaPicha: Samuel Corum/CNP/ZUMA/IMAGO
https://p.dw.com/p/5EYgf
Ruka sehemu inayofuata Netanyahu: Jeshi la Israel limevuka Mto Litani nchini Lebanon
29 Mei 2026

Netanyahu: Jeshi la Israel limevuka Mto Litani nchini Lebanon

Lebanon, Qasmiyeh 2026 | Shambulizi la anga la Israel dhidi ya daraja juu ya Mto Litani
Mnamo Machi 23, 2026, ndege za kivita za Israel zilishambulia Daraja la Qasmiyeh juu ya Mto Litani kusini mwa Lebanon, daraja linalochukuliwa kuwa muhimu kimkakati katika eneo hiloPicha: Ali Hashisho/Xinhua/picture alliance

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema jeshi la nchi hiyo limevuka Mto Litani kusini mwa Lebanon, umbali wa takriban kilomita 30 kutoka mpaka wa Israel na Lebanon.

Akizungumza wakati wa ziara katika kambi ya jeshi kaskazini mwa Israel, Netanyahu amesema vikosi vya Israel vinaendesha operesheni si tu kusini mwa Lebanon bali pia mjini Beirut na katika Bonde la Beqaa, huku akidai kuwa jeshi lake linaishambulia Hezbollah kwa nguvu kubwa.

Hatua hiyo ina maana kuwa jeshi la Israel sasa linafanya operesheni nje ya eneo lililoainishwa katika makubaliano ya usitishaji mapigano yaliyofikiwa mwezi Aprili 2026 kati ya Israel na Lebanon.

Licha ya makubaliano hayo, Israel na Hezbollah wameendelea kushambuliana, huku kila upande ukiutuhumu mwingine kwa kukiuka usitishaji mapigano.

Serikali ya Netanyahu imekuwa ikikabiliwa na shinikizo la ndani kutokana na mashambulizi ya kila siku ya ndege zisizo na rubani za Hezbollah kaskazini mwa Israel, hali iliyomsukuma kuahidi kuongeza operesheni za kijeshi dhidi ya kundi hilo katika siku za karibuni.

https://p.dw.com/p/5EYNg
Ruka sehemu inayofuata Ghalibaf aonya: Iran haina imani na maneno ya Marekani
29 Mei 2026

Ghalibaf aonya: Iran haina imani na maneno ya Marekani

Msemaji rasmi wa Iran na mmoja wa wajumbe wakuu katika mazungumzo na Marekani, Mohammad Bagher Ghalibaf, amesema Tehran haina imani na ahadi zozote zinazotolewa na Washington.

“Kutokana na uzoefu wetu, hatuna imani na dhamana zinazotolewa kwa maneno. Matendo pekee ndiyo kipimo chetu,” ameandika kwenye mtandao wa X.

Ghalibaf ameongeza kuwa washindi wa kweli katika mazungumzo yoyote ni wale wanaojiandaa kwa vita siku inayofuata baada ya mazungumzo hayo.

Kauli yake imekuja wakati taarifa zikionyesha kuwa Marekani na Iran zinakaribia kufikia makubaliano kuhusu kumaliza mzozo uliopo, ingawa bado kuna mashaka kuhusu hatua za mwisho za utekelezaji na kiwango cha uaminifu kati ya pande hizo mbili.

https://p.dw.com/p/5EYN5
Ruka sehemu inayofuata Lebanon yasema mapigano yanatishia maeneo ya urithi wa dunia
29 Mei 2026

Lebanon yasema mapigano yanatishia maeneo ya urithi wa dunia

Lebanon, Burj al-Shamali 2026 | Mwanaume akiwa juu ya jengo lililoharibiwa baada ya shambulizi la Israel
Mji wa Tyre kusini mwa Lebanon umekumbwa na mashambulizi makali ya anga ya Israel katika wiki iliyopitaPicha: Mohammed Zaatari/AP Photo/picture alliance

Waziri wa Utamaduni wa Lebanon Ghassan Salame ameonya kuwa maeneo ya urithi wa kihistoria nchini humo yako katika “hatari kubwa” kutokana na mashambulizi ya Israel kusini mwa nchi.

Salame amesema mabomu yameanguka karibu sana na magofu ya Tyre, mji wa kale uliotambuliwa na UNESCO kama eneo la Urithi wa Dunia mwaka 1984. Pia amesema ngome ya kihistoria ya Beaufort Castle imeguswa moja kwa moja na mashambulizi hayo.

“Kuzidi kwa mapigano kunamaanisha maeneo haya yako katika hatari kubwa,” amesema.

Licha ya kuwepo kwa makubaliano ya kusitisha mapigano, Israel na Hezbollah wanaoungwa mkono na Iran wameendelea kushambuliana, huku kila upande ukiutuhumu mwenzake kwa kukiuka makubaliano hayo.

Lebanon imeweka maeneo 79 ya urithi nchini humo chini ya ulinzi maalum wa UNESCO, hatua inayomaanisha kuwa uharibifu wowote wa maeneo hayo unaweza kuwa msingi wa hatua za kisheria za kimataifa.

https://p.dw.com/p/5EYMm
Ruka sehemu inayofuata Utafiti: Waisraeli wengi wanaunga mkono kuongezwa kwa operesheni za kijeshi nchini Lebanon
29 Mei 2026

Utafiti: Waisraeli wengi wanaunga mkono kuongezwa kwa operesheni za kijeshi nchini Lebanon

Lebanon Tyros 2026 | Athari za mashambulizi ya Israel
Israel imeongeza mashambulizi yake ya anga kusini mwa Lebanon wiki hiiPicha: REUTERS

Utafiti mpya umeonyesha kuwa Waisraeli wengi wanaunga mkono kuongezwa kwa operesheni za kijeshi dhidi ya Hezbollah kusini mwa Lebanon.

Kwa mujibu wa utafiti wa Mei 2026 uliofanywa na Taasisi ya Israel ya Mafunzo ya Usalama wa Taifa (INSS), asilimia 58 ya Waisraeli wanaamini serikali inapaswa kuongeza mashambulizi dhidi ya kundi hilo linaloungwa mkono na Iran. Miongoni mwa Wayahudi wa Israel, idadi hiyo inapanda hadi asilimia 69.5.

Utafiti huo pia umebaini kuwa asilimia 57 ya Waisraeli wanaunga mkono kuanzishwa kwa eneo la usalama kusini mwa Lebanon, ambapo wanajeshi wa Israel wangekaa kwa kudumu ili kulinda miji ya mpakani dhidi ya mashambulizi ya makombora na ndege zisizo na rubani za Hezbollah.

Takribani nusu ya waliohojiwa, asilimia 48, wamesema hali ya usalama kati ya Israel na Lebanon imezorota, huku asilimia 28 pekee wakiamini imeimarika.

Matokeo hayo yanakuja wakati serikali ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ikikabiliwa na shinikizo la ndani la kuchukua hatua kali zaidi dhidi ya mashambulizi ya Hezbollah, huku maafisa wa kijeshi wa Israel na Lebanon wakitarajiwa kukutana Pentagon nchini Marekani kwa mazungumzo ya usalama.

https://p.dw.com/p/5EYJ6
Ruka sehemu inayofuata Ripoti ya UN yashutumu vikosi vya usalama vya Israel kwa ukatili wa kingono
29 Mei 2026

Ripoti ya UN yashutumu vikosi vya usalama vya Israel kwa ukatili wa kingono

Ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa imeibua madai mazito dhidi ya wanajeshi na maafisa wengine wa usalama wa Israel, ikiwatuhumu kufanya vitendo vya ukatili wa kingono dhidi ya Wapalestina. Ripoti hiyo ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, inataja madai ya ubakaji, ubakaji wa makundi, majaribio ya ubakaji na ukatili uliolenga sehemu za siri za waathiriwa.

Umoja wa Mataifa unasema umethibitisha visa kadhaa vya ukatili wa kingono vilivyohusiana na mzozo huo mwaka 2025, vikihusisha wanaume, wanawake na watoto katika Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi.

Hata hivyo, Israel imekanusha vikali tuhuma hizo, ikizitaja kuwa hazina msingi wa ukweli na kuushutumu Umoja wa Mataifa kwa kujaribu kuweka usawa wa uongo kati ya vitendo vinavyodaiwa kufanywa na vikosi vya Israel na ukatili wa kingono unaodaiwa kufanywa na Hamas wakati wa mashambulizi ya Oktoba 7, 2023.

Kutokana na mvutano huo, ujumbe wa Israel katika Umoja wa Mataifa umetangaza kusitisha mawasiliano na Katibu Mkuu Antonio Guterres, huku balozi wa Israel katika umoja huo, Danny Danon, akisema Israel “imemalizana” na Guterres.

Marekani, New York 2025 | Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel Gideon Sa'ar mbele ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa
Balozi wa Israel katika Umoja wa Mataifa Danny Danon ameutaja uamuzi wa UN kuwa fedheha.Picha: Michael M. Santiago/Getty Images/AFP
https://p.dw.com/p/5EYH5
Ruka sehemu inayofuata Netanyahu asema Israel itachukua maeneo zaidi Ukanda wa Gaza
29 Mei 2026

Netanyahu asema Israel itachukua maeneo zaidi Ukanda wa Gaza

Israel, Sderot 2025 | Mizinga na magari ya kijeshi ya Israel karibu na mpaka wa Gaza baada ya usitishaji mapigano.
Israel kwa sasa inadhibiti zaidi ya nusu ya eneo la Ukanda wa Gaza wa Wapalestina (Picha ya Maktaba, Oktoba 2025)Picha: Mostafa Alkharouf/Anadolu Agency/IMAGO

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema nchi yake inalenga kuongeza udhibiti wake katika Ukanda wa Gaza, akieleza kuwa kwa sasa Israel inadhibiti takriban asilimia 60 ya eneo hilo.

Akizungumza katika mkutano wa Bonde la Jordan uliofanyika katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu, Netanyahu amesema Israel inalenga kufikia udhibiti wa asilimia 70 ya Gaza ili kuongeza shinikizo kwa kundi la Hamas.

“Jambo muhimu zaidi ni kuendelea kutumia nguvu zetu na kuziongeza zaidi,” amesema Netanyahu.

Wakati huo huo, Waziri wa Ulinzi wa Israel Israel Katz amesema mpango anaouita wa “uhamiaji wa hiari” wa Wapalestina kutoka Gaza “utatekelezwa.”

Hata hivyo, mashirika ya kutetea haki za binadamu yameonya kuwa hatua ya kuwahamisha Wapalestina kutoka Gaza inaweza kutafsiriwa kama utakaso wa kikabila.

https://p.dw.com/p/5EYDE
Ruka sehemu inayofuata Wajumbe wa majeshi ya Israel na Lebanon wakutana Marekani
29 Mei 2026

Wajumbe wa majeshi ya Israel na Lebanon wakutana Marekani

Lebanon, Sidon 2026 | Wakazi wakichunguza vifusi baada ya shambulizi la anga la Israel
Mazungumzo hayo katika makao makuu ya Pentagon yanafanyika baada ya siku kadhaa za mashambulizi makali ya anga ya Israel na mashambulizi ya ndege zisizo na rubani za HezbollahPicha: Mahmoud Zayyat/AFP

Maafisa wa kijeshi wa Israel na Lebanon wanatarajiwa kufanya mazungumzo ya usalama katika makao makuu ya Pentagon nchini Marekani Ijumaa, wakati mashambulizi ya kuvukana mpaka na operesheni za Israel nchini Lebanon zikiendelea kuongezeka.

Mazungumzo hayo yanayosimamiwa na Marekani yatakuwa ya kwanza ya moja kwa moja kati ya pande hizo mbili tangu kuzuka kwa mzozo wa hivi karibuni kati ya Israel na Hezbollah. Duru ya nne ya mazungumzo mapana yanayopatanishwa na Marekani inatarajiwa kufanyika mapema wiki ijayo.

Kabla ya mkutano huo, mashambulizi ya anga ya Israel yalilenga vitongoji vya kusini mwa Beirut na mji wa Tyre kusini mwa Lebanon, huku mamlaka za Lebanon zikisema watu wasiopungua 14 waliuawa.

Jeshi la Israel limesema lilishambulia zaidi ya malengo 135 ya Hezbollah katika maeneo ya kusini na mashariki mwa Lebanon, yakiwemo maeneo ya kurushia makombora na miundombinu ya kijeshi mjini Tyre.

Msemaji wa serikali ya Israel David Mencer amesema Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu ameagiza jeshi “kuongeza operesheni zake nchini Lebanon” huku mazungumzo ya kuiondolea Hezbollah silaha na kufikia makubaliano ya amani yakiendelea.

Mapema wiki hii, Netanyahu aliapa “kuisambaratisha” Hezbollah, kundi linaloungwa mkono na Iran.

Kwa upande wake, Hezbollah imekosoa mazungumzo hayo, ikidai viongozi wa Lebanon wanajadiliana “kwa gharama ya damu ya wananchi wao,” na kusema Beirut haina uwezo wa kuilazimisha Israel kuondoa majeshi yake au kusitisha vita.

https://p.dw.com/p/5EXIO
Ruka sehemu inayofuata Jeshi la Marekani lapinga madai ya Iran kuwa ndege yake ilidunguliwa
29 Mei 2026

Jeshi la Marekani lapinga madai ya Iran kuwa ndege yake ilidunguliwa

Jeshi la Marekani limekanusha madai yaliyotolewa na vyombo vya habari vya serikali ya Iran kwamba ndege ya Marekani ilidunguliwa karibu na mkoa wa Bushehr nchini Iran.

Afisa mmoja wa Marekani amesema hakuna ndege yoyote ya Marekani iliyopigwa au kuangushwa, akipinga taarifa zilizorushwa na televisheni ya taifa ya Iran kuhusu tukio hilo.

Mapema, vyombo vya habari vya Iran vilidai kuwa vikosi vya ulinzi wa anga viliharibu “ndege adui” katika eneo la Jam, mkoani Bushehr, lakini havikutoa maelezo ya kina kuhusu aina ya ndege hiyo.

Madai hayo yanajiri wakati mvutano kati ya Washington na Tehran ukiendelea kuongezeka licha ya juhudi za kidiplomasia za kufikia makubaliano kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran na usalama wa Mlango Bahari wa Hormuz.

https://p.dw.com/p/5EXFB
Ruka sehemu inayofuata Vance: Bado hatujafikia makubaliano na Iran
29 Mei 2026

Vance: Bado hatujafikia makubaliano na Iran

Makamu wa Rais wa Marekani JD Vance amesema Washington “bado haijafikia hatua hiyo” kuhusu makubaliano ya usitishaji mapigano na Tehran, lakini akaongeza kuwa wajumbe wa majadiliano wako karibu kufikia mwafaka.

Amesema Marekani iko katika nafasi ya kuweza kudhoofisha kwa kiwango kikubwa mpango wa nyuklia wa Iran.

Iran imeendelea kusisitiza kuwa mpango wake wa nyuklia unalenga matumizi ya kiraia pekee.

https://p.dw.com/p/5EVDC
Ruka sehemu inayofuata Iran yadai kudungua ndege ya Marekani
29 Mei 2026

Iran yadai kudungua ndege ya Marekani

Iran imesema mifumo yake ya ulinzi wa anga imeharibu “ndege adui” katika jimbo la Bushehr kusini mwa nchi hiyo, kwa mujibu wa vyombo vya habari vya serikali.

“Kilichotokea usiku huu kinahusiana na kuangamizwa kwa ndege adui,” shirika la habari la Tasnim liliripoti likimnukuu kiongozi wa wilaya ya Jam, Masoud Tangestani. “Hali katika mji huo sasa imerejea kuwa ya kawaida.”

Hata hivyo, hakuna uthibitisho uliotolewa na Marekani kuhusu madai hayo.

https://p.dw.com/p/5EVDB
Ruka sehemu inayofuata Iran na Marekani zaripotiwa kufikia makubaliano, yasubiri idhini ya Trump
28 Mei 2026

Iran na Marekani zaripotiwa kufikia makubaliano, yasubiri idhini ya Trump

Wawakilishi wa Marekani na Iran wamekubaliana kuongeza muda wa usitishaji mapigano wa sasa kwa siku nyingine 60, kwa mujibu wa vyanzo ambavyo havikutajwa majina vilivyonukuliwa na Axios pamoja na mashirika ya habari ya AP, Reuters na AFP.

Hata hivyo, makubaliano hayo bado yanasubiri idhini ya Rais wa Marekani Donald Trump.

Kwa mujibu wa ripoti hizo, makubaliano hayo yatawezesha kuanza tena kwa mazungumzo kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran na kuruhusu usafirishaji wa meli kupitia Mlango wa Hormuz kurejea katika hali ya kawaida.

Ikulu ya White House haikutoa maoni mara moja kuhusu taarifa hizo.

https://p.dw.com/p/5EVCh
Ruka sehemu inayofuata Iran yakosoa “uonevu” wa Donald Trump dhidi ya Oman
Imechapishwa 28 Mei 2026ilisahihishwa mwisho 28 Mei 2026

Iran yakosoa “uonevu” wa Donald Trump dhidi ya Oman

Marekani, Washington D.C. 2026 | Donald Trump akiongoza kikao cha Baraza la Mawaziri katika Ikulu ya White House
Trump alirudia madai yake kwamba Wairani “wanataka sana kufikia makubaliano” wakati wa matamshi yake siku ya JumatanoPicha: Samuel Corum/CNP/ZUMA/IMAGO

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmail Baghaei, amevitaja vitisho vya Rais wa Marekani Donald Trump dhidi ya Oman kuwa vya “hatari” na vya “kiuonevu.”

Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa kikao cha baraza la mawaziri Jumatano, Trump alisema Marekani itasaidia “kusimamia” Mlango wa Hormuz, uliopo kati ya Iran na Oman, pamoja na sehemu za Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE). Iran imeufunga kwa kiasi kikubwa mlango huo tangu muda mfupi baada ya kuzuka kwa vita, hali iliyotikisa uchumi wa dunia.

“Lakini hakuna mtu atakayeudhibiti. Oman itatii kama wengine au tutalazimika kuishambulia,” Trump alisema.

Alhamisi, Baghaei alikosoa matamshi hayo akisema Oman “daima imekuwa na mchango wa kujenga, wenye ufanisi na wa kuwajibika katika amani na usalama wa kikanda.”

Oman imekuwa mpatanishi katika duru mbalimbali za mazungumzo kati ya Marekani na Iran, hasa kuhusu mpango wa nyuklia wa Tehran.

Baghaei alisema vitisho vya Trump dhidi ya Oman ni “ishara nyingine hatari ya kuhalalishwa kwa uvunjaji wa sheria za kimataifa na siasa za uonevu katika mahusiano ya kimataifa.”

https://p.dw.com/p/5EVCb
Ruka sehemu inayofuata Israel yaanzisha mashambulizi dhidi ya Beirut
28 Mei 2026

Israel yaanzisha mashambulizi dhidi ya Beirut

Lebanon, Choueifat 2026 | Wahudumu wa uokoaji baada ya shambulizi la anga la Israel kusini mwa Beirut
Israel ilishambulia Beirut na maeneo mengine ya LebanonPicha: Ibrahim Amro/AFP

Wimbi la mashambulizi ya anga ya Israel dhidi ya Lebanon katika kipindi cha saa 24 zilizopita sasa limefika hadi mji mkuu Beirut, ambapo jeshi la Israel limesema “limeshambulia kwa usahihi” malengo kadhaa.

Vyanzo vya Lebanon vinasema shambulizi hilo lililenga eneo la makazi katika vitongoji vya kusini mwa Beirut, eneo linalojulikana kuwa ngome ya Hezbollah.

Israel haijabainisha ilichokuwa ikilenga, lakini imeongeza mashambulizi yake dhidi ya maeneo ya Hezbollah katika siku za hivi karibuni.

Hili ni shambulizi la kwanza kulenga mji mkuu wa Lebanon tangu Israel ilipomuua afisa wa kijeshi wa Kikosi cha Radwan cha Hezbollah mapema mwezi Mei.

https://p.dw.com/p/5EVCa
Ruka sehemu inayofuata Kiongozi Mkuu wa Iran asema Marekani na Israel zinataka “kuipigisha Iran magoti”
28 Mei 2026

Kiongozi Mkuu wa Iran asema Marekani na Israel zinataka “kuipigisha Iran magoti”

Iran, Tehran 2026 | Maandamano ya Siku ya Al-Quds yenye picha za Ayatollah Khamenei
Wairani wakiwa wameshika picha za Mojtaba Khamenei na marehemu baba yake Ali KhameneiPicha: Vahid Salemi/AP Photo/picture alliance

Marekani na Israel zinataka kuivuruga jamii ya Iran, Kiongozi Mkuu wa Iran Mojtaba Khamenei amesema.

Katika ujumbe uliochapishwa kupitia vyombo vya habari vya serikali, Khamenei alisema: “Mpango wa kipofu wa adui, baada ya vita walivyolazimisha, shinikizo la kiuchumi na kuzingirwa kisiasa pamoja na propaganda, ni kuanzisha mgawanyiko na kusambaratika kwa taifa ili kufidia kushindwa kijeshi na kulifanya taifa kupiga magoti.”

Khamenei hajaonekana hadharani tangu kabla ya kuingia madarakani mwezi Machi baada ya kuuawa kwa baba yake na aliyekuwa Kiongozi Mkuu wa Iran, Ali Khamenei, katika mashambulizi ya Marekani na Israel yaliyochochea vita vya sasa.

Waziri wa Ulinzi wa Marekani Pete Hegseth alisema mwezi Machi kuwa Mojtaba Khamenei “alijeruhiwa” na “huenda alipata ulemavu wa kudumu” katika mashambulizi hayo.

https://p.dw.com/p/5ETew
Onesha matokeo zaidi