1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroIsrael

Israel, Urusi waongezwa kwenye orodha ya ukatili wa kingono

29 Mei 2026

Vikosi vya usalama vya Israel na Urusi vimeongezwa kwenye orodha ya marufuku ya Umoja wa Mataifa kwa tuhuma za kujihusisha na ukatili wa kingono katika maeneo ya migogoro.

https://p.dw.com/p/5EVHy
Lebanon Dibbin 2026 | Vikosi vya jeshi la Israel
Vikosi vya jeshi la IsraelPicha: IDF/GPO/SIPA/picture alliance

Orodha hiyo inayochapishwa kila mwaka na Umoja wa Mataifa, inajumuisha makundi ya serikali na yasiyo ya serikali yanayoshukiwa kufanya ukatili wa kingono "kwa mpangilio maalum” katika nchi kama Sudan, Haiti, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Myanmar, Syria na Mali.

Mwezi Agosti mwaka jana, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alizionya Israel na Urusi kuhusu uwezekano wa kujumuishwa kwenye orodha hiyo iwapo matukio ya ukiukwaji yangeendelea kuripotiwa.

Licha ya onyo hilo, ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa inaeleza kwamba "matukio na mifumo ya ukatili wa kingono iliendelea kurekodiwa” katika vita vinavyoendelea nchini Ukraine na maeneo ya Palestina yanayokaliwa kwa mabavu.

Ukiukwaji unaotajwa katika ripoti hiyo unajumuisha ubakaji kwa kutumia kitu chochote kisicho sehemu ya mwili wa binadamu, ubakaji wa makundi, ukatili wa kimwili dhidi ya sehemu za siri, kulazimishwa kuwa uchi, na upekuzi wa miili uliofanywa "bila sababu ya wazi ya kiusalama.”

Hata hivyo, Israel imeikosoa vikali ripoti hiyo na kuitaja kuwa ya aibu na ya kipuuzi, ikisema ni jaribio la kuonekana usawa wa bandia kati yake na kundi la Hamas ambalo tayari limo kwenye orodha hiyo.