Timu za Marekani na Ukraine zakutana kwa mazungumzo
22 Machi 2026
Juhudi zinazoongozwa na Marekani za kusitisha mgogoro huo mbaya zaidi barani Ulaya, tangu kumalizika kwa vita vya pili vya dunia, zimekwama tangu Marekani na Israeli zilipoanzisha mashambulizi ya pamoja dhidi ya Iran mwezi Februari na kusababisha mvutano mkubwa katika eneo zima la Mashariki ya kati.
Hata hivyo wapatanishi wa Urusi na Ukraine hawajawahi kukutana tangu Februari wakati wa mkutano uliofanyika Geneva. Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema timu yake ya wapatanishi ilikwenda Florida itaendelea na mazungumzo hayo hii leo, akisisitiza kuwa wanataka kuelewa utayari wa Urusi katika kuvimaliza vita hivyo.
"Tuna mkutano wa pande mbili, Ukraine na Marekani unaofanyika Florida Marekani. Masuala yote yatajadiliwa. Hii inajumuisha maandalizi ya mkutano wa pande tatu ujao. Tunahitaji tarehe zilizo wazi. Kila mtu anaelewa kwamba hali katika Mashariki ya Kati, vita vinavyoendelea huko vinaathiri mazungumzo haya na kuahirishwa kwa tarehe ya mazungumzo. Hii si mara ya kwanza mkutano wa pande tatu umeahirishwa. Tungependa ufafanuzi zaidi kuhusu hili," alisema Zelensky
Mjumbe maalum wa Marekani Steve Witkoff na mkwe wa Rais Donald Trump Jared Kushner waliwakilisha upande wa Marekani, huku katibu wa baraza la usalama la Ukraine Rustem Umerov na msaidizi mkuu wa Zelensky Kyrylo Budanov wakiwakilisha upande wa Ukraine.