Serikali ya Sri Lanka yaapa kuwaangamiza waasi wa Tamil Tigers | Matukio ya Kisiasa | DW | 27.04.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Serikali ya Sri Lanka yaapa kuwaangamiza waasi wa Tamil Tigers

Maelfu ya watu bado wakwama kwenye eneo la mapigano nchini Sri Lanka

default

Waasi wa Tamil Tiger nchini Sri Lanka.

Baada ya Sri Lanka kukabiliwa na shinikizo za kuitaka isitumie silaha nzito dhidi ya waasi wa Tamil Tigers kaskazini mashariki mwa nchi hiyo imeamrisha wanajeshi wake kutotumia silaha nzito pamoja na ndege za kivita, huku waasi wakidai kuwa serikali bado inaendesha mashambulizi ya angani.

Kulingana na ripoti iliyotolewa na afisi ya rais ni kuwa, vikosi vya Sri Lanka vilishauriwa kutotumia siala nzito kama vile ndege za kivita dhidi ya waasi wa Tamil Tigers, kama njia ya kuepusha mauaji ya raia wasio kuwa na hatia.

Ripoti hiyo pia ilisema kuwa uamuzi huo uliafikiwa kwa kuwa oparesheni za kukabiliana na waasi hao zinaelekea kukamilika na kuongeza kuwa vikosi vya usalama vitandelea na juhudi za kuwaokoa raia ambao wanashikiliwa na waasi wa Tamil Tigers.

Wakati huo huo mawaziri wa masuala ya nje kutoka nchi za jumuiya ya ulaya wamelikaribisha tangazo la serikali ya Sri Lanka la kutotumia silaha nzito na kutoendesha oparesheni kali dhidi ya waasi wa Tamil, lakini pia wakatoa wito wa kusitishwa kwa mapigano hayo ili kutoa fursa kwa raia kulihama eneo la mapigano.

Kwenye mkutano uliofanyika nchini Luxembourg mawaziri hao walitaka kusitishwa kwa mapigano mara moja ili kuruhusu umoja wa mataifa kuwaondoa raia waliokwama katika maeneo ya mapigano kaskazini mashariki mwa Sri Lanka.

Hata hivyo msemaji wa waasi hao alisema kuwa, mashambulizi mawili yalifanywa na ndege za kivita hii leo na kuishutumu serikali kwa kuihadaa jamii ya kimataifa, madai ambayo yalikanushwa na kamanda wa jeshi la wanahewa wa Sri Lanka Janaka Nanayakara.

Waasi wa Liberation Tigers of Tamil Eelam (LTTE) walirejea kwenye mapigano baada ya serikali kukataa ombi la kusitisha mapigano hayo.

Sri Lanka Japen Bürgerkrieg Präsident Mahinda Rajapaksa mit Vermittler Yasushi Akashi

Rais wa Sri Lanka Mahinda Rajapaksa.

Akiongoea na waandishi wa habari kutoka eneo la mapigano mmoja wa madaktari wanaohudumu katika eneo hilo alisema kuwa, vikosi vya serikali viliendesha oparesheni ya kuiteka wilaya ya Mullativu iliyo umbali wa kilomita 395 kaskazini mashariki mwa mji mkuu Colombo.

Waasi wa LTTE wanasema kuwa raia 160,000 wamekwama katika eneo la pwani kaskazini mashariki mwa Sri Lanka, lakini serikali inasema kuwa ni watu 20,000 waliokwama katika eneo hilo.

Shirika moja linalosimamiwa na waasi wa Tamil lilinukuliwa likisema kuwa, ikiwa oparesheni hizo za serikali zitaendelea huenda zaidi ya watu 10,000 wakafa kwa kuwa kuna msongamano mkubwa wa watu waliokwama kwenye eneo la mapigano.

Wiki iliyopita karibu raia 109,000 walilitoroka eneo la mapigano kwenda maeneo yaliyo chini ya vikosi vya serikali, na kufanya idadi ya wakimbiizi wote waliotoka mapigano kufikia 170,000 tangu mwezi Januari mwaka huu.

Vikosi vya serikali vilisema kuwa viliwaokoa zaidi ya watu 3000 kutoka eneo la mapigano jana Jumapili huku wapiganaji 53 wakiwemo watoto 23 waliosajiriwa hivi majuzi wakijisalimisha.

Waasi wa Tamil jana jumapili pia walitangaza kusitishwa kwa mapigano, tangazo lilililokataliwa na waziri wa ulinzi wa Sri Lanka Gotabaya Rajapaksa. Rajapaksa ambaye ni nduguye rais wa Sri Lanka Mahinda Rajapaksa aliapa kendelea na mapigano hadi pale waasi wote watakapoangamizwa.

Mwandishi: Jason Nyakundi/DPAE

Mhariri: Mohammed AbdulRahman

 • Tarehe 27.04.2009
 • Mwandishi Jason Nyakundi
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/HfJR
 • Tarehe 27.04.2009
 • Mwandishi Jason Nyakundi
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/HfJR
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com