Saudi Arabia yaapa kuwaangamiza magaidi | Matukio ya Kisiasa | DW | 27.11.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Saudi Arabia

Saudi Arabia yaapa kuwaangamiza magaidi

Viongozi kutoka nchi 40 za Kiislamu wanakutana kwa kwa mara ya kwanza mjini Riyadh, Saudi Arabia kujadili juu ya ushirikiano wa kijeshi wa nchi hizo katika juhudi za kupamabana na ugaidi.

Katika mkutano huo wa kwanza kufanyika, mawaziri wa ulinzi na viongozi wengine waandamizi kutoka kwenye muungano wa kijeshi wa mataifa ya Kiislamu unaopambana na ugaidi, rasmi unahesabila kuwa ni nchi 41ukijumlisha na Marekani ambayo ni mshirika mkubwa wa Saudi Arabia. Kwa ushirikiano kundi hilo lina msimamo wa pamoja dhidi ya ukatili unaosababishwa na makundi au watu wenye itikadi kali.

Mohammed bin Salman (picture-alliance/AP Photo)

Mwana mfalme wa Saudi Arabia Mohammed bin Salman

Umoja huo ulianzishwa mnamo mwaka 2015 chini ya uongozi wa mwana mfalme Mohammed bin Salman wa Saudi Arabia, ambaye hadi sasa amepanda kwa kasi mno tangu kuteuliwa kwake kuwa mrithi wa kiti cha enzi mnamo mwezi Juni hali ambayo imetikisa jukwaa la kisiasa katika kanda yote ya Mashariki ya Kati.

Mohamed bin Salman ambaye pia ndiye waziri wa ulinzi wa Saudi Arabia katika hotuba yake ya ufunguzi ameapa kuwafuatilia magaidi mpaka watakapomalizika kabisa duniani. Katika mkutano huo Luteni jenerali Abdallah al Saleh wa jeshi la Saudi Arabia ameteuliwa kuwa katibu mkuu wa Umoja huo wa kijeshi wa nchi za Kiarabu dhidi ya Ugaidi( IMCTC) naye kwa upande wake amesema ushirikiano huo wa kijeshi utakuwa wazi kwa nchi nyingine ambazo zitataka kujiunga nao.

Saleh amesema mataifa yanayounga mkono yatakuwa na fursa, kuwa na makubaliano rasmi ya pande mbili, nchi hizo zitaweza kuwa na wawakilishi wao ndani ya muungano pia watakuwa na haki ya kutoa mipango yao wenyewe na vilevile kutathmini baadhi ya mipango inayojadiliwa na wanaweza kuchangia mipango hiyo kifedha au kitaalam.

Washiriki katika mkutano (Reuters/A. Abdallah Dalsh)

Washiriki katika mkutano

Mkutano huo ulioanza jana Jumapili unafanyika wakati ambapo ushirikiano wa kijeshi pamoja na mshirika mkuu wa Saudi Arabia ambaye ni Marekani, wamo katika vita dhidi ya kundi linalojiita dola la Kiislam IS kutoka kwenye ngome zao za mwisho zlizobaki huko Iraq na Syria.

Mkutano huo ambao kwa kiasi kikubwa hauzingatii nchi zinazofuata madhehebu ya Sunni pekee hata hivyo umeitenga Iran nchi inayofuata madhehebu ya Shia ambayo ni hasimu na mpinzani wa Saudi Arabia. 

Syria na Iraq pia zimetengwa kutokana na viongozi wake kuwa na uhusiano wa karibu na Iran. Hali hiyo inadhihirisha juu ya kuongezeka kwa mvutano kati ya Saudi Arabia na Iran, hususan juu ya vita katika nchi za Syria na Yemen pamoja na hali ya kisiasa ya nchini Lebanon.

Mwandishi:Zainab Aziz/AFPE

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com