Rais wa Urusi Dmitri Medvedev ziarani nchini Syria | Matukio ya Kisiasa | DW | 11.05.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Rais wa Urusi Dmitri Medvedev ziarani nchini Syria

Viongozi wa Urusi na Syria wasisitiza umuhimu wa kufumbuliwa mzozo wa Mashariki ya kati na kulitakasa eneo hilo na silaha za kinuklea

default

Rais Assad wa Syria

Rais Dmitri Medvedev wa Urusi amemaliza ziara yake ya siku mbili nchini Syria ambako ameshadidia azma ya nchi yake ya kuchangia kufikia amani Mashariki ya kati na uwezekano pia wa kujenga kinu cha nishati ya kinuklea nchini Syria.

Rais Medvedev amewasili jana usiku mjini Damascus kwa ziara yake ya kwanza rasmi iliyolengwa kuimarisha mafungamano pamoja na mshirika wa jadi wa enzi za Usovieti.

Rais Dmitri Medvedev aliyefuatana na ujumbe mkubwa wa wana uchumi na waziri wa nishati Sergei Shmatko alizungumza mara mbili na mwenyeji wake rais Bashar el Assad kabla ya kuondoka Damascus hii leo kuelekea Uturuki.Mada kuu ilihusu juhudi za amani ya mashariki ya kati na mvutano uliozuka kuhusu mradi wa kinuklea wa Iran.

Kuhusu Mashariki ya kati,rais Medvedev na rais Bashar Al Assad wameelezea azma ya kuzidishwa juhudi ili kuupatia ufumbuzi mzozo wa waarabu na Israel.Wameitolea mwito Israel iyahame maeneo ya mlima wa Golan wa Syria pamoja na maeneo yote inayoyakalia tangu mwaka 1967.Viongozi hao wawili wamesisitiza umuhimu wa kuundwa dola ya Palastina.

Akizungumza na waandishi habari pamoja na kiongozi mwenzake wa Syria,rais Dimtri Medvedev ameitolea mwito Marekani izidishe juhudi zake ili kuupatia ufumbuzi mzozo wa Mashariki ya kati.

Itafaa kusema hapa kwamba Urusi ni mojawapo wa kundi la pande nne zinazosimamia utaratibu wa amani ya Mashariki ya kati-ambazo ni pamoja na Marekani,Umoja wa mataifa na Umoja wa Ulaya.

Kuhusu mzozo uliosababishwa na mradi wa kinuklea wa Iran marais Medvedev na Bashar al Assad wamesema wanapendelea ufumbuzi wa amani na wa kidiplomasia kwa suala la mradi wa kinuklea wa Iran na kusisitiza umuhimu wa eneo la Mashariki ya kati kutakaswa na silaha za kinuklea na kuishinikiza Israel ijiunge na mkataba wa kutosambaza silaha za kinuklea.

Medvedev TV

Rais Dmitri Medvedev wa Urusi

Urusi inazingatia uwezekano wa kujenga vinu vya nishati ya kinuklea nchini Syria-amesema hayo waziri wa nishati wa Urusi Serguei Chmatko aliyeongeza kusema Damascus wakati huo italazimika kuheshimu mkataba wa kutosambaza silaha za kinuklea.

Urusi inaamini kila nchi ina haki ya kumiliki miradi ya kinuklea kwa matumizi ya kiraia.Wao ndio waliojenga kinu cha kinuklea cha Bouchehr nchini Iran ambacho kinatazamiwa kuanza kufanya kazi msimu huu wa kiangazi.

Mmarekani na nchi nyengine za Magharibi zinaituhumu Iran kutaka kumiliki silaha za kinuklea-hoja zinazobishwa na vviongozi wa mjini Teheran.

Ziara ya rais Medvedev imesadif siku chache tuu baada ya serikali ya Marekani kurefusha vikwazo vya kiuchumi dhidi ya Syria inayotuhumiwa pamoja na Iran kuyaunga mkono makundi ya kigaidi.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/afp/Reuters

Imepitiwa na:Mohammed Abdul-Rahman

 • Tarehe 11.05.2010
 • Mwandishi Oumilkher Hamidou
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/NLPX
 • Tarehe 11.05.2010
 • Mwandishi Oumilkher Hamidou
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/NLPX

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com