Rais wa Ujerumani ziarani Amerika Kusini | Matukio ya Kisiasa | DW | 12.05.2008
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Rais wa Ujerumani ziarani Amerika Kusini

Leo Kansela Angela Merkel wa Ujerumani anaanza ziara ndefu ya nchi za Amerika Kusini.Anatazamia kuzitembelea nchi nne kabla ya kuhudhuria mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya na Amerika Kusini mjini Lima nchini Peru.

Bundeskanzlerin Angela Merkel laechelt am Donnerstag, 8. Mai 2008, im Bundestag in Berlin

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel.

Ziara ya Merkel inaanzia Brazil ambako kwanza atatembelea mji mkuu Brasilia na baadae atafika jiji la kibiashara la Sao Paolo.Baada ya mkutano wa kilele wa nchi za Umoja wa Ulaya na Amerika Kusini katika mji mkuu wa Lima,Peru,Kansela Merkel atazitembelea pia Colombia na Mexico.

Muda mfupi kabla ya ziara hiyo kuanza,Kansela Merkel ameshambuliwa na Rais Hugo Chavez wa Venezuela aliyefika hadi ya kumlinganisha na Adolf Hitler.Kiongozi huyo wa Venezuela,maarufu kwa ulimi wake mkali, amesababisha fadhaa.Chanzo cha matamshi makali ya rais huyo wa Venezuela ni mahojiano ya Kansela Merkel pamoja na shirika la habari la Ujerumani-DPA ambapo Merkel alisema,Rais Hugo Chávez anaefuata siasa za kizalendo za mrengo wa shoto hazisemei nchi zote za Amerika Kusini.

Siku ya Jumapili,mjini Caracas,Rais Chavez alisema, "Kansela Angela Merkel anatokana na mrengo wa kulia, kama ule wa Adolf Hitler,unaounga mkono ufashisti."Merkel hajataharuki na anashikilia hoja zake zile zile. Msemaji wa serikali kuu mjini Berlin amesema,msimamo wa Chavez haukumshtua mtu.

Katika mahojiano pamoja na shirika la habari la Ujerumani-DPA,Kansela Merkel akimulika mkutano ujao wa kilele kati ya nchi za Umoja wa Ulaya na Amerika Kusini,alitoa mwito wa kuanzishwa aina mpya ya ushirikiano katika kupambana na umaskini.Amesema,"Siasa za kizalendo za mrengo wa shoto,mfano wa zile zinazofuatwa na Chavez,sio mfano bora unaostahiki kufuatwa,ili kurahisisha hali ya mambo katika nchi nyingi za Amerika Kusini." Akasema,ili kuweza kuwepo ushirikiano wa kina pamoja na Cuba,kiongozi mpya Raul Castro anabidi kufanya mageuzi zaidi ya kidemokrasi."Katika mahojiano hayo yaliyotafsiriwa pia kwa lugha ya Kihispania,Kansela Angela Merkel aliulizwa kama siasa kali za kizalendo za mrengo wa shoto zinazofuatwa na Rais Hugo Chavez wa Venezuela zimeathiri uhusiano kati ya nchi za Amerika Kusini na Umoja wa Ulaya.Merkel alijibu kuwa nchi moja pekee haiwezi kuathiri uhusiano kati ya Umoja wa Ulaya na Amerika Kusini.Akasema,Rais Chavez hazungumzi kwa niaba ya nchi za Amerika Kusini-kila nchi inazungumza kwa sauti yake na kuambatana na maslahi yake.

Kwa upande mwingine,Rais Chavez wa Venezuela amesema kuwa kupitia kipindi maalum cha televisheni,atamjibu Kansela Merkel wakati wa mkutano wa kilele wa May 16 hadi 17 mjini Lima.Viongozi wa serikali za Latin Amerika hawajataka kusema chochote kuhusu matamshi hayo makali ya Rais Chavez wa Venezuela.

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com