1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Köhler arejea nyumbani toka kusini mashariki ya ulaya

Schwartz/ Oummilkheir6 Julai 2007

Ujerumani yasifiwa kama rafiki na mshirika wa kuaminika

https://p.dw.com/p/CHBS
Rais Köhler na mwenyeji wake wa Bulgaria
Rais Köhler na mwenyeji wake wa BulgariaPicha: AP

Rais wa shirikisho la jamhuri ya Ujerumani Horst Köhler amemaliza ziara yake ya siku nne kusini mashariki ya Ulaya.Alikua na mazungumzo ya kisiasa mijini Bukarest,Sofia na Sarajevo,alikutana na vijana na wawakilishi wa jamii, na kuyatembelea maeneo kadhaa mashuhuri ya kitamaduni -kwa hivyo ratiba ya ziara hiyo ilikua nono, ya maarifa na iliyokua na ujumbe maalum.

Wakaazi wa kusini mashariki ya Ulaya walikua pia wakisubiri matamshi bayana kutoka kwa rais wa shirikisho-na huo bila ya shaka ndio ujumbe mkubwa ambao Horst Köhler alirudi nao Ujerumani kutoka Rumania,Bulgaria na Bosnia Herzegovina.Matamshi bayana sio tuu kuhusu kuzidi kuungwa mkono juhudi za nchi za eneo hilo za kujiunga na umoja wa ulaya,bali pia matamshi bayana kuhusu walakini zote zilizoko .

Mijini Bukarest,Sofia na Sarajevo,rais wa shirikisho la jamhuri ya Ujerumani Horst Köhler sio tuu amefanikiwa kuwatanabahisha watu juu ya umuhimu wa kuendelezwa mageuzi, lakini pia hakuchelea kila wakati alipokutana na wanasiasa kudhukuru mambo ambayo yanabidi kutekelezwa ili kujiambatanisha na viwango vya Umoja wa Ulaya.

Matamshi bayana ya Köhler kuhusu maendeleo yaliyopatikana,matamshi mema ya kuwakaribisha wanachama wawili wepya wa umoja wa ulaya-Rumania na Bulgaria-maneno ya kutia moyo aliposema anaamini Bosnia Herzegovina inafuata njia ya maana-yote hayo yalifuatana sambamba na matamshi yaliyofichua dosari zilizoko pia.

Ni kweli kwamba wanachama wepya wa Umoja wa ulaya, Rumania na Bulgaria,wamesonga mbele katika kutia njiani hatua za mageuzi kuliko Bosnia Herzegovina iliyoathirika kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe.Lakini Bukarest na Sofia zimekosolewa vikali pia katika ripoti ya hivi karibuni ya halmashauri kuu ya umoja wa ulaya kwa kutoharakisha kutia njiani mageuzi katika vyombo vya sheria na uzembe katika kupambana na rushwa.

Rais Köhler amezungumzia kinaga ubaga matatizo hayo pamoja na viongozi wenzake Traian Basescu na Georgi Parvanov ,na aliyoyasema yamepokelewa vyema na wananchi.Wengi wa wananchi wa nchi hizi mbili wanahisi mfumo huru na madhubuti wa sheria,na mapambano ya nguvu dhidi ya rushwa,yanaweza tuu kufanikiwa ikiwa shinikizo litazidi kutoka nje.Risala hiyo rais Köhler ameipata zaidi alipokutana na vijana na wawakilishi wa mashirika ya jamii.

Mjini Sarajevo pia walikua vijana waliozidi kumpa moyo rais Köhler aendelee kuamini juu ya mustakbal mwema wa Bosnia Herzegovina,ikiwa jumuia ya kimataifa itaendelea kuwajibika.

Kuna jengine pia lililotokana na ziara ya rais wa shirikisho mjini Sarajevo-Horst Köhler alizungumza na wanajeshi,wake kwa waume wa jeshi la shirikisho Bundeswehr wanaotumikia vikosi vya Umoja wa ulaya EUFOR katika Bosnia na Herzegovina.Kuna mipango ya kupunguza idadi ya wanajeshi hao hatua baada ya hatua-lakini ratiba bado haijaandaliwa na kila kitu kitategemea hali ya utulivu namna ilivyo .Lakini dalili zinatia moyo,pengine wanajeshi hao wakaanza hivi karibuni kurejea nyumbani.Habari nzuri ambazo rais wa shirikisho amerejea nazo Ujerumani.

Kwa jumla ziara yake imedhihirisha Ujerumani inajivunia sifa nzuri katika eneo la kusini mashariki ya Ulaya .Kila alikopita,naiwe Sibiu/Hermannstadt,uliotangazwa kua mji mkuu wa utamaduni wa ulaya kwa mwaka 2007,naiwe katika mji mashuhuri wa kihistoria PLOVDIV au mji mkongwe wa Sarajevo,rais wa shirikisho la jamhuri ya Ujerumani Holrst Köhler alipokelewa kwa shangwe na furaha na wananchi.

Ujerumani,na hayo rais wa shirikisho amepata ushahidi kamili,haiangaliwi kama mshirika mkubwa wa kibiashara tuu wa eneo hilo,inajivunia sifa kubwa zaidi,inatajwa kua nchi rafiki na ya kuaminika.