Rais George W. Bush kukihotubia kwa mara ya mwisho kikao cha Umoja wa mataifa | Matukio ya Kisiasa | DW | 23.09.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Rais George W. Bush kukihotubia kwa mara ya mwisho kikao cha Umoja wa mataifa

Rais wa Marekani George W. Bush anakihotubia kikao cha mwaka cha Umoja wa mataifa hii leo kwa mara ya mwisho kukiwa na lawama ulimwenguni dhidi yake juu ya vita vya Irak na Afghansitan na mzozo wa kifedha wa sasa duniani

default

Rais wa Marekani, George W.Bush

Rais George W. Bush huenda yeye angependelea kusisitiza katika hotuba yake juu ya juhudi za pamoja ili kuzishinikiza nchi za Iran na Korea ya kaskazini kuacha mpango wao wa kinyuklia na kupitisha mpango wake wa biashara huru duniani.

Badala ya hayo, inaelekea atakabiliana na mgogoro wa kifedha wa sasa kukiwa na wasi wasi juu ya mpango wake wa kuzitolea benki na mashirika ya kifedha yaliyopo ukingoni kufilisika msaada wa bilioni 700 za dolla. 


Miongoni mwa viongozi walio na wasi wasi juu ya mpango huo, ni pamoja na Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-Moon.

Yeye anahofia kuwa  msaada huo na misaada mingine ya kifedha ambayo imekwisha tolewa au itatolewa juu ya mgogoro huo wa kifedha, itapunguza nia na utashi kwa nchi tajiri kuzisaidia nchi masikini.

Rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy ambae pia anatarajiwa kuuhotubia mkutano huo wa kilele wa Umoja wa mataifa, amesema ingefaa viongozi wa Benki na taasisi za kifedha waliyosababisha balaa hilo la kifedha duniani wachukuliwe hatua kali.


Wakati huo huo, viongozi wa nchi za Afrika, wanaonya kuwa mzozo huu wa kifedha duniani pamoja na mkwamo wa mazungumzo juu ya Mkataba wa biashara duniani, utauathiri mpango wa Umoja wa mataifa wa kuboresha maisha ya mamia ya mamilioni ya watu katika nchi masikini.


Nchi hizo masikini zinazakabiliwa na tatizo jingine la uharibifu wa mazingira na ambao unahitaji msaada wa Umoja wa mataifa katika kukabiliana nao. Makamu wa rais wa zamani wa Marekani Al Gore na mwanaharakati wa kimazingira kutoka Kenya, Wangari Maathai, wametayarisha mkakati ambao utawasilishwa katika mkutano huo wa kilele wa Umoja wa mataifa na ambao ungeweza kusaidia katika mazungumzo kwa lengo la kufikiwa Mkataba wa Umoja wa mataifa juu ya kupambana na ongezeko la joto duniani mwakani kwa kuhifadhi vyema misitu ya maeneo ya joto.


Na kama tulivyosema hapo awali, licha ya mzozo wa sasa wa kifedha kugubika mazungumzo ya viongozi na wataalamu na kugonga vichwa vya habari, rais Bush atazungumzia kwa upana suala la Iran na Korea ya kaskazini na wasaidizi wake watakuwa wanashughulika na mswada wa vikwazo vya kuwekewa nchi hizo mbili. Lakini wana hakika kuwa atakanushwa na rais wa Iran, Mahmoud Ahmadinejad ambae naye pia atakihotubia kikao hicho cha Umoja wa mataifa baada ya rais George W. Bush.

 • Tarehe 23.09.2008
 • Mwandishi Nijimbere, Gregoire
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/FNOL
 • Tarehe 23.09.2008
 • Mwandishi Nijimbere, Gregoire
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/FNOL
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com