Rais Barrack Obama aangazia sera zake za kigeni | NRS-Import | DW | 28.05.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

NRS-Import

Rais Barrack Obama aangazia sera zake za kigeni

Rais wa Marekani Barack Obama ametoa hotuba inayoshughulikia sera zake za kigeni kwa kuangazia juhudi za kukabiliana na makundi ya misimamo mikali, ugaidi na uwezekano wa Marekani kujihusisha zaidi Syria

Katika hotuba yake kuhusu sera za kigeni ambazo atazizingatia katika kipindi cha miaka miwili iliyosalia kabla ya kumaliza hatamu yake ya uongozi rais wa Marekani Barack Obama amesema Marekani inapaswa kuongoza katika safu ya kimataifa lakini pia inafaa kujizuia kabla ya kuchukua hatua za kuingilia nchi za kigeni kijeshi.

Akielezea mipango yake kuhusu sera za kigeni hii leo katika chuo cha mafunzo ya kijeshi mjini New York, Obama amesmea nchi yake inaiunukia kutoka kipindi kirefu cha vita na kuongeza kuwa kujitenga sio jambo linaloweza kutumika katika karne hii ya ishirini na moja.

Ushirikiano ni bora kuliko kutumia mabavu

Obama amesema Marekani itatumia nguvu za kijeshi ikihitajika lakini itakuwa na nguvu zaidi iwapo itashirikiana na wenzake badala ya kuchukua maamuzi kivyake na kuongeza kuwa ana mipango ya kushirikian na bunge la nchi hiyo kuongeza msaada kwa makundi ya wapigani wenye misimamo ya wastani nchini Syria.

Rais wa Marekani Barrack Obama katika gwaride la kufuzu wanajeshi

Rais wa Marekani Barrack Obama katika gwaride la kufuzu wanajeshi

Obama amewapuuzilia mbali wakosoaji wake wanaohoji kuwa Marekani haina nguvu tena au nguvu hizo zimeteterekea katika safu ya kimataifa kwasababu ya kutotumia nguvu za kijeshi na kuwashutumu kuwa wameifafanua visivyo historia.

Ugaidi ni kitisho kikubwa kwa Marekani na dunia nzima

Kiongozi huyo wa Marekani pia amegusia kitisho cha kundi la waasi la Boko Haram nchini Nigeria na kusema operesheni za kiusalama za Marekani haziwezi kuondoa kitisho hicho cha ugaidi lakini kwasasa Marekani inaangazia kuwaokoa wasichana wa shule waliotekwa nyara na waasi wa Boko Haram na kuwahamasisha vijana wa Nigeria.

Kiongozi wa kundi la waasi la Boko Haram Abubakar Shekau

Kiongozi wa kundi la waasi la Boko Haram Abubakar Shekau

Obama amesema kitisho kikubwa hivi sasa kwa Marekani na ulimwengu kwa jumla ni ugaidi hasa kutoka kwa makundi yenye misimamo mikali yenye mafungamano na mtandao wa kigaidi wa Al Qaeda.

Katika hotuba yake amegusia pia mzozo wa mipaka katika bahari ya China Kusini kati ya China na majirani zake na kuonya kuwa Marekani iko tayari kujibu uchokozi wa China lakini nchi yake inahitaji kuwa mfano mwema kwa kuzingatia mikataba muhimu.

Marekani ina mipango ya kuanzisha hazina ya dola bilioni tano kukabiliana na ugaidi kwa kutoa mafunzo na vifaa kwa nchi washirika ili kupambana na ghasia zinazotokana na makundi yenye misimamo mikali iliyo na mafungamano na mitandao ya kigaidi.

Obama amekuwa akitumia zaidi mfumo wa kutumia diplomasia katika masuala ya kigeni mtazamo ambao umeshutumiwa na wanasiasa wa chama cha upinzani Marekani cha Republican na wachambuzi kadhaa wa masuala ya kidiplomasia ambao wangependa kumuona Obama akitumia nguvu zaidi katika kukabiliana na mizozo.

Mwandishi:Caro Robi/Reuters/Ap

Mhariri: Josephat Charo

Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com