Putin na Waandishi wa Habari | Matukio ya Kisiasa | DW | 14.02.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Putin na Waandishi wa Habari

Mkutano wa mwisho wa Putin na waandishi wa habari

Rais Vladimir Putin akiuhutubia mkutano wa waandishi wa habari.

Rais Vladimir Putin akiuhutubia mkutano wa waandishi wa habari.

Rais Vladimir Putin wa Russia leo amesema yuko tayari kuyaelekeza maroketi ya nchi yake kwendea nchi ambazo zamani zilikuwemo katika Mkataba wa Kujihami wa Warsaw, ikiwemo nchi jirani ya Ukraine, pindi nchi hizo zitajiunga na Umoja wa Kujihami wa NATO au kukaribisha vituo vya kijeshi vya nchi za Magharibi. Pia katika mkutano wake wa mwaka na waandishi wa habari alisifu namna Russia inavonawiri, kiuchumi, chini ya uongozi wake.

Rais Putin alisema Russia italazimika kuyaelekeza makombora yake kwendea malengo ambayo wao Warussia wanahisi yanahatrisha usalama wao wa taifa.

Ukraine inaomba hivi sasa ijiunge na Shirika la Kujihami la nchi za Magharibi, NATO. Pia Russia imekasirishwa na mipango ya Jamhuri za Cheki na Poland kukaribisha mfumo wa ulinzi wa kukabiliana na maroketi uweko katika ardhi zao.

Vladimir Putin alisema, ´Inaonesha watu wanataka kupandisha nchini Poland hisia za kuipinga Russia. Kisingizio ni kwamba Poland inahitaji kulindwa kutokana na maroketi yatokayo Iran. Lakini Iran haina maroketi. Kutokana na mipango ya Marekani, wizani wa kijeshi utafujwa na kiwango cha usalama barani Ulaya kitapungua. Sifahamu, kwanini?'

Akizungumza wiki mbili kabla ya kufanyika uchaguzi wa urais ambapo mtu aliyemtaka kuwa mrithi wake ana hakika ya kushinda, Vladimir Putin alisisitiza kwamba Russia ni nchi ya kidemokrasia, na akasema yeye hajawi kuwa na uchu wa madaraka, licha ya mashambulio ya wahakiki kwamba ameunda dola ya kiimla.

Alisema miaka yote minane aliyokuwa yeye madarakani amefanya kazi kama mtumwa, kutoka asubuhi hadi usiku. Hata hivyo, alisema hajawahi kutamani kukaa madarakani zaidi ya awamu mbili mfululizo, kipindi kirefu kabisa kinachoruhusiwa chini ya katiba. Alisema wahakiki wanasema uraibu mkubwa kabisa ni kupenda madaraka, lakini yeye hajahisi hivyo.

Kiongozi huyo wa Russia aliipaka picha nzuri juu ya kipindi chake cha miaka minane madarakani, akiashiria namna uchumi unavongara na dola kuwa na nguvu zaidi. Alitaja kwamba yeye haoni makosa yeyote makubwa yaliofanywa, kwani malengo yote yaliowekwa yamefikiwa. Hata hivyo, alikiri kwamba Russia inakabiliana na tatizo la ughali wa maisha unaopanda, ambapo sasa mfumko wa bei unafikia asilimia 12. Aliyaelezea yale alioyafikia kuwa ni ya kihistoria:

' Hapo kabla hatukuwa na dola ilioungana, hatujawa na wimbo wa taifa. Katika baadhi ya jamhuri za Shirikisho la Russia kulikuweko katiba zilizoifunika katiba ya Russia nzima. Ilitulazimu kwanza kuirejesha dola.'

Vladimir Putin alikuwa akizungumza mjini Mosko mbele ya mamia ya waandishi wa habari katika mkutano wake wa kila mwaka- mkutano wa mwisho wa aina hiyo kabla ya yeye kuwacha madaraka baadae mwaka huu.

Hapo Machi 2, makamo wa kwanza wa waziri mkuu, Dmitry Medvedev, ana hakika ya kushinda uchaguzi wa urais unaowaniwa pia na watetezi wengine watatu. Wahakiki nchini Russia na ngambo wameuelezea uchaguzi huo kuwa ni wa udanganyifu unaokusudia kuhakikisha ushindi wa Dmitry Medvedev, na jumuiya muhimu za nchi za magharibi za kufuatiliza chaguzi zimeamuwa kutopeleka wachunguzi wao.

Rais Putin amesema yuko tayari kutumika kama waziri mkuu chini ya Dmitry Medvedev, lakini wachunguzi wengi wanamtarajia kwamba atabakia na madaraka zaidi kuliko yale ambayo kwa kawaida huwa nayo waziri mkuu.

 • Tarehe 14.02.2008
 • Mwandishi Miraji Othman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/D7aR
 • Tarehe 14.02.2008
 • Mwandishi Miraji Othman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/D7aR
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com