Papa Benedicto wa XVI na njia ya amani kuisuluhisha mizozo | Masuala ya Jamii | DW | 18.07.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Masuala ya Jamii

Papa Benedicto wa XVI na njia ya amani kuisuluhisha mizozo

Kiongozi wa kanisa la kikatoliki duniani, Baba Mtakatifu Benedicto wa XVI, amewahotubia maelfu ya waumini katika Siku Kuu ya Vijana Duniani mjini Sydney Australia juu ya umoja wa dini na njia ya amani kuisuluhisha mizozo

Papa Benedicto wa XVI mbele ya waumini

Papa Benedicto wa XVI mbele ya waumini

Katika dunia ambayo imehatarishwa na majanga na aina nyingi tu ya machafuko, viongozi wa kidini kwa kauli moja wanatoa mwito kwa viongozi wa nchi na jamii kuisuluhisha mizozo kwa njia za amani na kwa lengo la kuheshimu binaadamu, amesema Papa Benedicto wa XVI. Baba Mtakatifu ametoa mfano wa hapo hapo nchini Australia, mwenyeji wa Siku Kuu ya Vijana Duniani mwaka huu ambako amesema serikali hatimae ilikiri unyonge uliyotendewa raia asilia hapo zamani na kuanza kuchukuwa hatua kwa lengo la kufikia maridhiano chini ya msingi wa kuheshimiana na kwa maoni yake, huo ungefaa kuwa mfano:

´´Kwa sasa mnaelekea kuziba pengo lililokuwapo kati ya raia asilia na raia wengine wa Australia kwa kutilia maanani tu matarajio, elimu na maendeleo. Mfano huu unawapa matumaini raia wengine kote duniani ambao wanasubiri kuona haki zao zimeheshimiwa na jukumu lao katika jamii limetambuliwa na kuendelezwa´´.

Papa Benedicto wa XVI ameyatamka hayo baada ya kukutana kwa mazungumzo na wawakilishi wa dini za kiislamu na kiyahudi huko Australia. Amesema kwamba katika maswala yote hayo yanaohusiana na maisha ya binaadamu, dini ni kiungo na wala sio kiini cha mgawanyiko. Dini inaweza kupelekea watu wenye asili tofauti kuishi pamoja kwa amani na kujenga urafiki na majirani.

Baba Mtakatifu ameendelea kusema kuwa kanisa la kikatoliki lipo tayari kupokea maoni kutoka makanisa mengine juu ya maswala yanayotatanisha. Ni hivyo, Papa Benedicto wa XVI ameelezea wasi wasi wake juu ya mgogoro unaolikabili kanisa la kianglikana juu ya swala la kutatanisha la kuwaruhusu wanawake na mashoga kuwa padri vile vile.

Swala jingine linalomshughulisha pia kiongozi wa kanisa la kikatoliki na ambalo huenda akaliombea tena radhi katika hotuba yake nyingine iliyopangwa hapo kesho, ni tabia mbaya ya ukatili wa ngono kwa kuwashirikisha watoto ambapo baadhi ya mapadri walihusika akiwemo moja mjini Sydney Australia ambako kunafanyika shughuli kuhusiana na Siku Kuu hiyo ya Vijana duniani.

Mbali na tukio hilo la ngono, Australia inaelekea kumpata Mtakatifu wake wa kwanza, MacKillop ambae anajulikana sana kwa shughuli zake za kibinaadamu kwa ajili ya watoto katika maeneo ya vijijini nchini Australia katika karene iliyopita na jina lake kupewa kanisa moja hapo mjini Sydney. Baba Mtakatifu amesema akilitembelea kanisa hilo kuwa kunafanyika uchunguzi wa mwisho kumtangaza MacKillop mtakatifu.

 • Tarehe 18.07.2008
 • Mwandishi Nijimbere, Gregoire
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/EetX
 • Tarehe 18.07.2008
 • Mwandishi Nijimbere, Gregoire
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/EetX
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com