Obama awataka viongozi wa Afrika kuzingatia uthabiti wa kisiasa | Matukio ya Kisiasa | DW | 10.07.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Obama awataka viongozi wa Afrika kuzingatia uthabiti wa kisiasa

Obama aipongeza Ghana kwa demokrasia

Rais wa Marekani Barack Obama

Rais wa Marekani Barack Obama

Rais wa Marekani, Barack Obama, anatarajiwa kuwasili hii leo nchini Ghana katika ziara yake ya kwanza barani Afrika tangu alipoingia madarakani mnamo Januari 20 mwaka huu. Kiongozi huyo wa Marekani amewataka viongozi wa Afrika wafanye juhudi kukomesha vitendo vya rushwa na kuyumba kwa hali ya kisiasa ili kuvutia uwekezaji unaohitajika kwa ajili ya maendeleo.

Akizungumza kabla ziara yake, rais Barack Obama wa Marekani amesema kuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya utawala bora na maendeleo na hivyo kuwataka viongozi wa Afrika kuongeza bidii zaidi. "Tunajua hilo litachukua muda. Tulichokiona hadi sasa ni kuendelezwa kwa mifano mizuri ya utawala barani Afrika na nadhani huu ndio wakati wa kuanza," amesema rais Obama. Kiongozi huyo wa Marekani amesema ni muhimu viongozi wa Afrika kuwajibika na kubeba dhamana kwa makosa yanayotokea. Ameongeza kusema kwamba kitu ambacho kwa mtazamo wake kimekwamisha maendeleo barani Afrika ni sababu nyingi zisizokuwa na maana ambazo zimekuwa zikitolewa kueleza vitendo vya rushwa na utawala mbovu.

Rais Obama amechagua kuitembelea Ghana akiileza kuwa mfano mzuri wa demokrasia kwa kuwa imefaulu kufanya chaguzi kwa ufanisi mkubwa ambapo madaraka yamekabidhiwa kwa amani kwa viongozi walioshinda uchaguzi, ingawa kwa idadi ndogo ya kura. Amesema ana matumaini rais wa Ghana John Atta Mills amejidhihirisha kuwa mtu aliyejitolea kuhakikisha kuna utawala wa sheria na misingi ya demokrasia inayohakikisha uthabiti wa taifa.

Alipoulizwa iwapo anayapendelea maeneo au nchi fulani za Afrika, kwa mfano Afrika Magharibi ambako ni muhimu kwa sababu ya mafuta au Afrika Mashariki kama eneo muhimu kwa masilahi ya Marekani, rais Obama amesema.

"Nadhani bara zima la Afrika ni muhimu. Ingawa naitembelea Ghana katika ziara hii, tayari waziri mkuu wa Zimbabwe Tsvangirai na rais wa Tanzania Jakaya Kikete wamenitembelea ofisini mwangu na kila mara najaribu kutoa ujumbe ule ule. Serikali ya Tanzania inafanya kazi nzuri kutoa huduma kwa wanachi wake na mahala popote watu wanapotaka kujisaidia sisi tunataka kushirikiana nao. Na nadhani tuna uongozi ulio imara barani Afrika ulio tayari kusonga mbele na tunataka kuwa pamoja nao."

Akizungumza kuhusu misaada ya maendeleo barani Afrika rais Obama amesema sera za utawala wake kuhusu utoaji wa misaada zimegawanyika miongoni mwa wakala mbalimbali kwani mawazo yanatofautiana kulingana na utawala au chama kilicho madarakani kwa wakati fulani. Amesema utakuwa uamuzi wa maana kujaribu kuunda sera zitakazofaa badala ya kushikilia mifumo ya kizamani ambayo imeshindwa kuzaa matunda. Na teknolojia itakuwa na jukumu muhimu katika kuanisha utoaji wa misaada kwa nchi mbalimbali na kufuatilia vipi misaada hiyo inavyotumiwa ili kuhakikisha inawafikia walengwa.

"Moja kati ya maswala yanayonitia wasiwasi kuhusu sera yetu ya misaada kwa ujumla ni kwamba watalaam wa nchi za magharibi na hagharama za usimamizi hatimaye hutumia asilimia kubwa ya msaada jumla tunaoutoa. Kwa maoni yangu, tunachotakiwa kufanya ni kujaribu kupunguza udhibiti wetu na kuongeza uwezo wetu wa kutoa mafunzo kwa watu waweze kujitegemea. Kwa hiyo nadhani kutumia mtandao wa intaneti na teknolojia ya kisasa ni muhimu. "

Rais Obama amesisitiza umuhimu wa uwekezaji badala ya kutegemea tu misaada. Amesema hakuwezi kuwepo uwekezaji mzuri pasipo utawala bora na kuongeza kuwa ipo haja ya nchi za Afrika kuchanganya uwekezaji wa kigeni na ujenzi wa viwanda vinavyoweza kutoa bidhaa zinazoweza kuongeza uuzaji wa bidhaa katika nchi za kigeni. Amesisitiza pia umuhimu wa kuwekeza katika elimu ili kuimarisha nguvu kazi.

Rais Obama anazuru Ghana akitokea nchini Italia ambako alihudhuria mkutano wa nchi nane tajiri kiviwanda duniani, G8.

Mwandishi: Josephat Charo

Mhariri: Miraji Othman


 • Tarehe 10.07.2009
 • Mwandishi Charo Josephat
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Il66
 • Tarehe 10.07.2009
 • Mwandishi Charo Josephat
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Il66
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com