1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Sheria na HakiUjerumani

Nicaragua:Ujerumani isitishe kupeleka silaha Israel

8 Aprili 2024

Nicaragua imeitaka mahakama ya Kimataifa ya haki, ICJ, kuiamuru Ujerumani kusitisha upelekaji wa silaha kwa Isreal na kurejesha ufadhili kwa shirika la UNRWA, ikisema kuna hatari kubwa ya mauaji ya kimbari Gaza.

https://p.dw.com/p/4eYTC
Uholanzi | Wakili wa Ujerumani Tania von Uslar-Gleichen akiwa na jopo la mwakili wengine.
Wakili wa Ujerumani Tania von Uslar-Gleichen akiwa na jopo la mwakili wengine wakati wakisikiliza wasilisho la Nicaragua .Picha: Robin van Lonkhuijsen/ANP/picture alliance

Nicaragua imeiburuza Ujerumani katika mahakama ya kimataifa ya haki ikiwataka majaji wa mahakama hiyo kuweka hatua za dharura kuizuwia Berlin kutoa silaha zaidi kwa Israel pamoja na msaada mwingine.

Mawakili wa Nicaragua wamehoji kuwa Ujerumani inakiuka Mkataba wa mwaka 1948 wa Umoja wa Mataifa dhidi ya mauaji ya kimbari, ulioundwa kufuatia mauaji ya Wayahudi ya Holocaust, kwa kuipatia Israel silaha.

Wakili wa Nicaragua Daniel Mueller, ameiambia mahakama kuwa "kwa hakika ni kisingizio cha kusikitisha kwa watoto wa Kipalestina, wanawake na wanaume walioko Gaza kutoa misaada ya kibinadamu," Muller alisema katika wakilisho lake katika mahakama ya haki ya ICJ.

Soma pia:Wapalestina warejea Khan Younis baada ya Israel kuondoka

Ameongeza kuwa "kupitia udondoshaji wa angani, kwa upande mmoja, na kutoa silaha na zana za kijeshi zinazotumiwa kuwaua na kuwaangamiza na kuua pia wafanyakazi wa misaada ya kibinadamu kama ilivyothibitishwa hivi karibuni na shambulio la kombora dhidi ya magari na wafanyakazi wa World Central Kitchen, kwa upande mwingine."

Balozi wa Nicaragua nchini Uholanzi, Carlos Jose Arguello Gomez, ameiambia mahakama ya ICJ  kuwa Ujerumani inaonekana kutoweza kutofautisha kati ya dhana ya kujilinda na mauaji ya kimbari. Nicaragua imeitaka mahakama hiyo kutoa amri ya dharura wakati ikizingatia kesi pana. 

Wakili mwingine wa Nicaragua Alain Pellet, amesema Ujeurmani inaelewa vyema kwamba silaha ilizozitoa na inazoendelea kuzitoa kwa Israel zinaweza kutumika kufanya mauaji ya halaiki. Ameongeza kuwa ni muhimu hasa kwa Ujerumani kusitisha msaada wake wa kijeshi kwa Israel.

Ujerumani kujibu kuhusu tuhuma hizo

Ujerumani itatoa majibu yake kikamilifu mbele ya mahakama hiyo, lakini tayari wakili wake Tania von Uslar-Gleichen, amesema kesi ya Nicaragua imeegemea pakubwa upande mmoja.

Uholanzi |Majaji wa Mahakama ya ICJ wakiwa katika vikao vya mahakama.
Majaji katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki ICJ wakiwa kwenye shauri la Nicaruaga dhidi ya Ujerumani.Picha: Robin van Lonkhuijsen/ANP/AFP/Getty Images

Ujerumani haikiuki na haijawahi kukiuka Mkataba wa Mauaji ya Kimbari wala sheria ya kimataifa ya kibinadamu, iwe moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja.

Wasilisho la Nikaragua lina upendeleo mkubwa na tutakuwa tukiwaambia kesho jinsi tunavyotimiza majukumu yetu kikamilifu.

ICJ iliundwa kuamua mizozo kati ya mataifa na imegeuka mdau muhimu katika vita kati ya Israel na Hamas vilivyozuka baada ya mashambulizi ya Oktoba 7.

Katika kesi tofauti, Afrika Kusini Iliishutumu Israel kufanya mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Gaza, madai ambayo Israel iliyakanusha vikali.

Soma pia:Netanyahu asema Israel iko karibu kushinda vita vyake dhidi ya Hamas

Nicaragua imeiomba mahakama kuamuru hatua tano za dharura, ikiwemo Ujerumani, kusitisha mara moja msaada wake kwa Israel, hasa msaada wa kijeshi ikiwemo zana za kijeshi.

Pia inataka mahakama kuiamuru Ujerumani kubatilisha uamuzi wake wa kusitisha msaada kwa shirika la UNRWA, iliyouchukuwa kufuatia tuhuma za Israel kwamba wafanyakazi wa shirika hilo la Umoja wa Mataifa walishiriki shambulio la Oktoba 7.

Wakili Daniel Mueller amefafanua kwamba Nicaruaga imeamua kuishtaki Ujerumanibadala ya mshirika mkuu wa Israel, Marekani, kwa sababu Washington haitambui mamlaka ya mahakama hiyo. 

Hakuna matumani katika mazungumzo ya Cairo

Wakati haya yakijiri, afisa wa Hamas amesema mazungumzo yalioanza tena mjini Cairo jana, kujaribu kutafuta muafaka wa kusitisha vita yameendelea kukwaa kisiki licha ya ripoti za kuwepo na maendeleo.

Afisa huyo ambaye hakutaka jina lake litajwe, ameliambia shirika la habari la Uingereza Reuters, kwamba hakujawa na mabadiliko ya msimamo kwa upande wa Israel na hivyo hakuna jipya katika mazungmzo hayo. 

Soma pia:Wapatanishi kukutana tena Misri kwa ajili ya makubaliano ya kusitisha vita kati ya Israel na Hamas

Awali maafisa wa Misri waliarifu kuwepo na hatua kuelekea mapatano, katika mazungumzo hayo ambayo yanahudhuriwa pia na wawakilishi wa Marekani, Israel, na Qatar.

Israel epusheni mauaji ya halaiki Gaza