Nchi tajiri zachelewa kiasi kutimiza ahadi za misaada Afrika | Masuala ya Jamii | DW | 17.06.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Masuala ya Jamii

Nchi tajiri zachelewa kiasi kutimiza ahadi za misaada Afrika

Nchi tajiri zaidi duniani zimechelewa kiasi kutekeleza ahadi zilizozitoa kuongeza mara mbili misaada kwa bara la Afrika kufikia mwaka 2010.

Kofi Annan, mwanachama wa Africa Progress Panel

Kofi Annan, mwanachama wa Africa Progress Panel

Katika ripoti ya Shirika linalohusika na maswala ya maendeleo la Africa Progress Panel, nchi tajiri zimeshachelewa kutoa bilioni 40 za dolla kulingana na mipango zilizokuwa nayo wakati zilipotoa ahadi hizo za misaada. Shirika hilo la Africa Progress Panel lilianza kukadiria ahadi zilizotolewa na kundi la nchi 8 tajiri zaidi duniani ama G8 katika mkutano wake mwaka 2005 mjini Gleneagles nchini Scotland.

Hata rais wa Marekani George W Bush akiwa ziarani nchini Uingereza, amekiri kuwa hali imezidi kuwa mbaya barani Afrika na kwamba nchi hizo tajiri zikumbuke kuwa kuna watu wengi barani Afrika ambao watafariki dunia ikiwa nchi hizo zitaendelea kupoteza muda. Bush anasema: "tunawategemea kufanya zaidi mbali na kutoa ahadi, tunawategemea kuwa wepesi kutoa fedha kwa sababu za kibinaadamu".


Katibu mkuu wa zamani wa Umoja wa mataifa Kofi Annan, naye pia aliwasihi viongozi wa nchi za Ulaya na nchi 8 tajiri zaidi duniani kuweka ahadi zao kwa vitendo. Kofi Annan, ni miongoni mwa wanachama wa shirika hilo la Africa Progress Panel pamoja na waziri mkuu wa zamani wa Uingereza Tony Blair, kiongozi wa zamani wa Fuko la fedha la kimataifa Michel Camdessus na mwanaharakati mkuu katika kampeni ya kupambana na umasikini Bob Geldof.

Africa Progress Panel limesema madeni yaliofutwa katika mkutano wa kilele wa G8 wa mwaka 2005 yalisaidia kwani nchi masikini zilitumia fedha hizo katika sekta za afya na elimu.

Lakini ikiwa mfumko mkubwa wa bei hautosimama au kupungua, bila shaka kutakuwa na ongezeko dhahiri la njaa, utapia mlo na vifo vya watoto. Mgogoro huo wa chakula ndiwo umesababisha kwa sehemu kubwa kuweko na hali ya dharura, imezidi kusema ripoti ya shirika hilo la Africa Progress Panel.


Hatua za kusimamisha mfumko wa bei za mafuta na chakula, zitatiliwa kipaumbele kwenye mkutano wa nchi tajiri zaidi duniani G8 nchini Japan kwa sehemu fulani kutokana na hali kwamba bei hizo huchangia kupunguza uchumi katika nchi tajiri na kusababisha upinzani kutoka kwa raia wao wasioridhika. Kwa hiyo serikali zimekuwa zikikabiliwa na shinikizo za kifedha kiasi kwamba hazitotimiza ahadi zao za misaada kwa nchi za kiafrika. Ingekuwa bora viongozi hao wakaweka katika mkutano wao sera mpya za kuongeza misaada. Kwa mfano sera hizo zingehusu ushuru wa biashara na nchi nyingine, kodi ya usafiri wa ndege na gharama za usafirishaji wa mizigo.


Kulingana na ripoti hiyo ya Africa Progress panel, kuna haja ya kubadili sera za kibiashara ili Afrika nayo ifike kwenye masoko iwe na mapato ya kununua chakula. Shirika hilo limependekeza pia biashara ya mbolea kuwa huru na nchi tajiri zitowe ruzuku kwa ujenzi wa nishati mbadala.

Itakuwa vizuri pia nchi tajiri zikatoa gharama zaidi kwa ajili ya nishati inayoweza kurudiwa kwa sababu mabadiliko ya hali ya hewa husababisha hasara kubwa zaidi katika uzarishaji wa kilimo barani Afrika kuliko sehemu nyingine yoyote ya dunia.

 • Tarehe 17.06.2008
 • Mwandishi Nijimbere, Gregoire
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/EKtI
 • Tarehe 17.06.2008
 • Mwandishi Nijimbere, Gregoire
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/EKtI
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com