NATO na Uingereza zaijadili upya operesheni ya Libya | Matukio ya Kisiasa | DW | 15.06.2011
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

NATO na Uingereza zaijadili upya operesheni ya Libya

Ndege za NATO zimeendelea na mashambulizi yake mjini Tripoli, huku Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo, Fogh Anders Rasmussen, akikutana na viongozi wa serikali ya Uingereza kujadiliana operesheni yao ya wiki 11 sasa.

Helikopta ya jeshi la NATO

Helikopta ya jeshi la NATO

Mkutano wa leo kati ya Rasmussen, Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron, na Waziri wa Mambo ya Nje, William Hague, mjini London, unakuja mara tu baada ya mashambulizi mapya ya NATO dhidi ya maeneo kadhaa ya mji mkuu wa Tripoli, ambayo NATO inasema yamezipinguza kwa kiasi kikubwa nguvu za vikosi vya Kanali Muammar Gaddafi.

Mjini Tripoli, miripuko ilisikika kiasi ya saa 5.30 usiku wa jana, na mashahidi wanasema waliona wingu zito la moshi likitokea mjini humo. Televisheni ya Shirika la Habari la Libya, Jana, imeripoti vifo na majeruhi kadhaa kwa upande wa raia na nyumba kuunguwa moto katika wilaya ya Al-Ferjan ambayo ililengwa na makombora ya NATO.

Mazungumzo haya pia yanakuja siku moja tu baada ya viongozi wa ngazi za juu wa Uingereza na Ufaransa kuelezea hadharani wasiwasi wao juu ya kurefuka kwa muda wa vita vya anga ya NATO, ambayo kwa kiasi kikubwa yamewasaidia waasi kusonga mbele dhidi ya vikosi vya Gaddafi.

Waasi wamefanikiwa kukitwaa kijiji cha Al-Rayaniya, kilicho mashariki ya mji wa mashariki wa Zintan, katika eneo la milima ya Berber Nafusa, kusini magharibi ya mji mkuu wa Tripoli.

Katibu Mkuu wa NATO, Anders Fogh Rasmussen

Katibu Mkuu wa NATO, Anders Fogh Rasmussen

Kijiji hiki chenye wakaazi wapatao 10,000, kiko katika eneo muhimu kwa mkakati wa kivita, kwani linaunganisha miji ya Zintan na Yefren, ambayo inagombaniwa sana na pande zote mbili.

Vikosi vya Gaddafi vilitumia maroketi ya masafa ya mbali kukilenga kijiji hicho, na imeripotiwa kuwa wapiganaji wawili wa waasi wameuawa. Hata hivyo, mpiganaji mmoja wa waasi amesema kwamba wanaendelea kusonga, wakitumaini kufika Tripoli.

"Mwenyezi Mungu akipenda tutafika ikulu ya Bel-Aziziyah kumtoa Gaddafi. Kwa idhini yake Mungu, vijana wetu wamejitolea hadi mwisho wa mapambano haya, na inshallah tutashinda." Amesema mpiganaji huyo.

Rais Barack Obama wa Marekani

Rais Barack Obama wa Marekani

Katika hatua nyengine, wanasiasa nchini Marekani wameanza kupoteza uvumilivu kuhusiana na kasi ya operesheni ya NATO nchini Libya.

Spika wa bunge la Congress, John Boehner, amempa Rais Barack Obama hadi Ijumaa hii, awe ameshaiomba Congress idhini ya hatua kijeshi nchini Libya, vyenginevyo aviondoe vikosi na rasimali za Marekani kwenye operesheni hiyo.

Boehner ameuonya utawala wa Rais Obama kwamba utawajibika, ikiwa itafika Jumapili, ambayo ni siku ya mwisho ya 90 iliyowekwa na Sheria ya Nguvu za Vita ya Mwaka 1973 inayomruhusu Rais wa Marekani kutuma wanajeshi nje ya nchi bila ya ruhusa ya Congress.

Ikulu ya Marekani imesema itajibu shutuma hizi za Boehner. "Tupo katika hatua za mwisho za kutayarisha taarifa yenye ufafanuzi kwa ajili ya mabaraza ya Congress na Senate, ambayo itaeleza kila kitu kuhusu jitihada zetu zinazoendelea nchini Libya." Amesema msemaji wa masuala ya usalama, Tommy Vietor.

Masuala ya muda wa operesheni hii na gharama za kuiendeshea yanaonekana kuwagawa nchi wanachama wa NATO.

Wakati hayo yakiendelea, Baraza la Mpito la Kitaifa linaloongozwa na waasi wa Libya limepata uungwaji mkono mwengine kutoka jumuiya ya kimataifa, baada ya Panama kutangaza kuwa nchi ya 15 duniani na ya kwanza Amerika ya Kusini kulitambua kama wawakilishi halali wa Walibya.

Kwa upande wa Afrika, Tunisia imesema kwamba iko tayari kulitambua Baraza hilo, huku Liberia ikivunja mahusiano yake ya kibalozi na utawala wa Gaddafi hapo jana. Hadi sasa ni Senegal na Gambia pekee katika mataifa ya Afrika, ambayo tayari yamewatambua rasmi waasi wa Libya kuwa wawakilishi halali wa watu wa Libya.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/Reuters
Mhariri: Othman Mirajji

DW inapendekeza

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com