1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapambano yaendelea Zawiyah magharibi mwa Libya

Abdu Said Mtullya13 Juni 2011

Majeshi ya Gaddafi yapambana na wapinzani katika mji wa Zawiyah

https://p.dw.com/p/11ZD6
Helikopta ya NATO ikitua baada ya mashambulioPicha: picture-alliance/dpa

Mapambano baina ya wapinzani na majeshi ya Kanali Gaddafi yanazidi kulemea katika mji wa Zawiyah magharibi mwa Libya.

Kwa mujibu wa tarifa ya wapinzani, mapigano makali yametokea siku ya pili mfulululizo kwenye mji huo muhimu wa Zawiyah karibu na mji mkuu,Tripoli. Mwakilishi wa wapinzani amearifu kuwa waasi 13 pamoja na raia waliuawa mwishoni mwa wiki iliyopita.

Barabara za miji ya pwani, kati ya Tripoli na Tunisia zimefungwa kutokana na mapigano, lakini serikali ya Libya, kwa upande wake imesema hakuna mapigano makubwa katika mji wa Zawiyah.

Hata hivyo Shirika la Televisheni la Al- jazeera limeripoti kwamba waasi waliyashambulia majeshi ya Gaddafi , kati ya miji ya Jafran na Sintan umbali wa kilometa mia moja kusini magharibi, ya mji mkuu wa Libya, Tripoli.

Wakati huo huo Kanali Gaddafi kwa mara nyingine amesema kuwa hatang'atuka. Aliyasisitiza hayo kwenye mazungumzo yake na Rais wa Shirikisho la Sataranji Duniani, Kirsan Illumshinov mjini Tripoli. Gaddafi alimwambia bwana Illumshinov alietembelea Libya kwamba yeye hataondoka Libya. Gaddafi ameeleza kuwa yeye hana wadhifa wowote na kwa hiyo hawezi kujiuzulu.

Katika tukio lingine muhimu kuhusu Libya Umoja wa Falme za Kiarabu umelitambua Baraza la Mpito la wapinzani, kuwa mwakilishi halali wa watu wa Libya. Wizara ya mambo ya nje ya nchi hiyo imesema, hivi punde tu itafungua ofisi yake ya uwakilishi katika ngome kuu ya wapinzani mjini Benghazi.