Nafasi ya pesa katika uchaguzi wa Marekani | Matukio ya Kisiasa | DW | 16.10.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Nafasi ya pesa katika uchaguzi wa Marekani

Wakati kampeni za kinyang’anyiro cha uchaguzi wa Rais nchini Marekani zikiwa katika hatua za mwanzo, suala la uwezo wa wagombea kipesa limekosha watu wengi duniani

Wagombea wa Urais Bibi Hillary Clinton (kushoto) na Barack Obama

Wagombea wa Urais Bibi Hillary Clinton (kushoto) na Barack Obama

Suala la utajiri na uwezo kipesa limekuwa gumzo miongoni mwa wagombea wa nafasi ya kurithi kiti cha Rais George W. Bush wa Marekani hapo Novemba mwakani.

Taarifa zilizopatikana hadi sasa zinaeleza kwamba mgombea wa nafasi ya urais kupitia chama cha Demokrat Bibi Hillary Clinton akaunti yake inaonesha kwamba ana jumla ya dola za kimarekani milini 35, wakati Bwana Barack Obama kutoka chama hicho pia amejilimbikizia dola milioni 32.

Bibi Hillary Clinton ambaye ni seneta wa Jimbo la New York, pia akiongoza katika kura ya maoni, ana kiasi kingine cha dola milioni 15 zitakazotumika ikiwa atasimama kuwakilisha chama chake cha Demokrat katika uchaguzi huo.

Wakati mgombea huyo akiwa na jumla ya dola milioni 50 kwa ajili ya kuhakikisha kwamba anashinda uchaguzi wa rais wa Marekani hapo mwakani, tume ya uchaguzi ya nchi hiyo imesema Bwana Barack Obama ana kiasi cha dola milioni 4 za kutumia kwenye kampeni kubwa ikiwa atapata bahati ya kuwakilisha chama chake, kwa hiyo jumla kuu ya pasa zake ni dola milini 36.

Ama kwa upande wa wagombea wa chama tawala cha Republican, Rudy Giuliani anayeongoza kwa kura za maoni ana kiasi cha dola milioni 16.7 huku Bwana Mitt Romney anayechukua nafasi ya pili akiwa ameshajikusanyia dola milioni 21 ili kuhakikisha kwamba kila kitu kinakwenda sawa katika kampeni zake.

Mgombea anayeshika nafasi ya tatu kupitia chama cha Republican ni mcheza sinema wa zamani wa Hollywood Bwana Fred Thompson ambaye hadi sasa ana jumla ya dola milioni 7.1 katika akaunti yake.

Kiasi cha pesa kinachomilikiwa na kila mgombea ndiyo hicho kitakachotumika kulipia matangazo na mahitaji mengine ikiwemo posho za waratibu wanaowasaidia kufikia malengo yao.

Wakati Bibi Hillary Clinton akishika nafasi ya juu katika kura za maoni kwa kuwaacha wagombea wawili katika majimbo waliyokwishapita, hali inaelekea kuwa tofauti kidogo katika jimbo la Iowa ambalo limekuwa na upinzani mkubwa.

Akiwa katika kampeni zake, mgombea huyo ambaye ni mke wa Rais wa zamani wan chi hiyo-Bill Clinton, Bibi Hillary ameweza kujikusanyia pesa taslimu dola milioni 28 katika kipindi cha miezi tisa iliyopita, ikiwemo kiasi cha dola milioni 24 alizokuwanazo hapo awali.

Aidha, kinyang’anyiro hicho cha uchaguzi wa Novemba mwaka 2008 kimekuwa gumzo kubwa ndani na nje ya Marekani kutokana na mpango wa Rais George Bush wa kuendeleza vita nchini Iraq pamoja na kukabiliana na vitendo vya kigaidi katika nchi kadhaa duniani.

Kuhusu nani atawakilisha chama gani kati ya Republican na Demokrat katika uchaguzi wa Marekani, mambo yatajulikana mnamo miezi mitatu ijayo, baada ya kukamilisha mchakato wa wagombea katika kampeni za awali.

Hata hivyo siku zote Chama cha Demokrat kimekuwa kikipinga hatua ya kuendelea kuwepo kwa majeshi ya Marekani nchini Iraq, kufuatia kile kinachoelezwa kwamba ni matumizi mabaya ya fedha pamoja na vifo vya askari wao.

Pia Wamarekani wengi wanakiri kwamba wamechoshwa na vita ya Iraq iliyoanza tangu mwaka 2003.

 • Tarehe 16.10.2007
 • Mwandishi Tuma Provian Dandi
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/C7hV
 • Tarehe 16.10.2007
 • Mwandishi Tuma Provian Dandi
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/C7hV

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com