1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mzozo wa kibiashara kati ya Marekani na Umoja wa ulaya

Oumilkheir Hamidou
21 Februari 2018

:Mzozo wa kibiashara kati ya Umoja wa Ulaya na Marekani, vuta nikuvute kati ya Hungary na Umoja wa ulaya na zoezi la uchaguzi wa SPD kuhusu makubaliano ya kuunda serikali ya muungano ni miongoni mwa mada magazetini

https://p.dw.com/p/2t2gC
USA Donald Trump
Picha: Getty Images/W. McNamee

 

Tunaanzia njia panda inayoiunganisha Marekani na Umoja wa Ulaya. Sera za rais wa Marekani Donald Trump  za kupigania kwa kila hali masilahi ya Marekani au kama mwenyewe anavyoiita "America First" zinatishia kuuponza uhusiano wa kibiashara kati ya nchi hiyo na mataifa takriban yote mengine ya dunia. Gazeti la " Nordwest-Zeitung" linaandika: "Marekani na Umoja wa Ulaya , kila mmoja anamtunushia misuli mwenzake na hali hiyo inaweza kusababisha mzozo wa kibiashara. Kwamba vitisho kutoka Washington, viongozi wa mjini Brussels hawawezi kuvinyamazia , ni jambo linaloeleweka. Sera ya America First isimaanishe,"Ulaya iwe mwisho". Hata kama inaeleweka pale Marekani inapokataa  kuridhia bei za chini kwa bidhaa za chuma cha pua kutoka China, lakini hatua za serikali ya Marekani kutaka kuwaadhibu watu wote  kwa pamoja hazikubaliki na pengine haziambatani pia na kanuni za shirika la kimataifa la biashara WTO. Kimkakati ni sawa kwamba Umoja wa Ulaya unaendeleza vizuwiizi kwa bidhaa ambazo zinaathiri zaidi masilahi ya kisiasa na sio ya kiuchumi."

Visa vya Orban vinawachosha viongozi wa Umoja wa Ulaya

Malumbano kati ya waziri mkuu wa Hungary Viktor Orban na Umoja wa Ulaya yanazidi makali na hakuna dalili ya chochote kubadilika. Cha kufanya ni kipi? Linajiuliza gazeti la "Weser-Kurier" na kuandika: "Suala linazuka upya: Umoja wa Ulaya ufanye nini? Uendelee tu na hatua dhidi ya wanaokwenda kinyume na makubaliano? Mbona zaidi ya elfu zimeshachukuliwa na Orban bado hajali yeye? Vitisho vya kuipokonya Hungary haki ya kupiga kura, navyo pia haviogopi. Kwa hivyo imesalia njia moja tu: Pesa. Hungary inapokea msaada mkubwa kabisa wa Umoja wa ulaya, kati ya mwaka 2010 hadi mwaka 2017 imeshapokea jumla ya Euro bilioni 30. Halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya inabidi ibadilishe hali hiyo haraka-isiachie kuchezewa na kiburi cha Orban."

SPD waamua kuhusu hatima ya serikali ya muungano wa vyama vikuu GroKo

Mada yetu ya mwisho magazetini inaturejesha Ujerumani ambako tokea jana wanachama wa SPD wameanza kupiga kura kuamua kama wanaunga mkono au la makubaliano ya kuunda serikali ya muungano wa vyama vikuu pamoja na CDU/CSU au GroKo kama inavyoitwa. Gazeti la "Südwest Presse" linaandika: "Kilichoandikwa na gazeti la Bild ni upuuzi mtupu. Zoezi la kupiga kura miongoni mwa wanachama wa SPD si kichekesho kwasababu linaweza kusababisha hatari. Pindi matokeo ya zoezi hilo yakiwa ya kubanana, na mengi yanaashiria hivyo, basi itategemea kama matokeo hayo yatatambuliwa na pande zote mbili; walioshinda na walioshindwa. Hilo halitowezekana kama kutafanyika hila. Mbinu hizo viongozi wanabidi wahakikishe zitakuwa miko."

 

Mwandishi:Hamidou Oumilkheir/Inlanadspresse

Mhariri:Yusuf Saumu