1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mzozo katika uchumi wa Nigeria

Sekione Kitojo15 Septemba 2010

Nchi zinazoendelea zimebaki kuwa salama kutokana na mzozo wa kiuchumi ulioikumba dunia, mtizamo ulioenezwa katika sehemu mbali mbali ulimwenguni kwa sehemu fulani sio sahihi.

https://p.dw.com/p/PCU7
Wafanyakazi wa kampuni ya kuchimba mafuta nchini Nigeria wakiwa kazini. Mafuta yanachangia kwa kiasi kikubwa uchumi wa Nigeria.Picha: picture-alliance/dpa/dpaweb

► "Nchi zinazoendelea zimebaki kuwa salama kutokana na mzozo wa kiuchumi ulioikumba dunia" - Mtizamo huu ulioenezwa katika sehemu mbalimbali za ulimwengu kwa sehemu fulani sio sahihi, kwani katika kipindi kirefu kufilisika kwa benki ya Lehman Brothers ya Marekani miaka miwili iliyopita, ambako kulisababisha kutokea mgogoro mkubwa wa kiuchumi nchini Marekani, kumesababisha pia athari kwa nchi zinazoendelea. Mfano ni Nigeria, ambayo uchumi wake umekuwa ukiimarika sana. Nchi hii sasa inakabiliana na mgogoro wake wa kiuchumi.

Mji wa Lagos katika pwani ya bahari ya Atlantik ni uti wa mgongo wa uchumi wa Nigeria, na hata kwa bara zima la Afrika. Sio tu kwa kuwa idadi ya raia inaongezeka kwa kasi kubwa na sasa imefikia milioni 10. Mara kwa mara makampuni mengi zaidi ya kimataifa yamekuwa yakiendesha shughuli zao mjini Lagos. Soko la hisa la Nigeria mjini Lagos ni la pili kwa ukubwa barani Afrika, huku soko la hisa la Afrika Kusini mjini Johannesburg likishikilia nafasi ya kwanza. Lakini kuanzia mwaka 2008 miaka ya neema ya kiuchumi imekwisha, anasema Emanuel Okoh, mfanyabiashara wa kuuza hisa.

"Wakati mambo yalipokuwa mazuri, kulikuwa na shughuli nyingi katika masoko ya hisa. Watu walikuwa wakijadiliana na kucheka, lakini siku hizi ukumbi unakuwa umejaa nusu kwa kuwa hakuna shughuli nyingi zinazoendelea. Ni wakati mgumu sana kwetu. Wafanyabiashara wenzangu wana matatizo ya kulipa mishara ya wafanyakazi wao."

Kati ya mwaka 2008 na 2009 soko la hisa la Nigeria lilipoteza asilimia 70 ya thamani yake. Hali hii ilitokana na migogoro miwili ya kiuchumi: mmoja wa ndani ya nchi na mwingine wa kimataifa. Wanigeria wengi walikuwa na matumaini kuwa kuporomoka kwa mabenki kulikoikumba Marekani kungelikwepa bara la Afrika. Mfumo wa fedha wa Nigeria hauna mafungamano sana na ule wa Marekani, lakini hali iliyojitokeza ilikuwa tofauti kabisa.

Chanzo kikubwa cha mgogoro wa ndani wa kiuchumi nchini Nigeria ni mfumo wa zamani uliokuwepo. Mabenki yalitoa mikopo bila kuchunguza na kuthibitisha uwezo wa mtu kuweza kulipa mikopo hiyo au kuwa na dhamana. Kwa njia hiyo wanasiasa wote na wafanyakazi mafisadi wa benki walinufaika. Walijaza mifuko yao na kutumia fedha hizo kununua hisa kwa kubahatisha wangepata faida, au walishindwa kulipa mikopo hiyo. Jaiye Doherty wa muungano wa makapuni ya Ujerumani na Nigeria mjini Lagos anasema:

"Hakuna aliyejali kuhusu hilo kwa sababu mtu aliyepata pesa aliziwekeza tena, kwani viwango tulivyopata katika soko la fedha hungeweza kuvipata mahala popote. Watu walinunua hisa na kupata faida mara tano ya thamani yake katika kipindi kifupi. Lakini swali lilikuwa: Je, hali hiyo inaweza kudumu kwa muda gani?"

Wateja wengi wa mabenki walitoa kiwango kikubwa cha fedha zao kutoka kwenye masoko ya fedha na kwa njia hiyo mabenki yalipoteza faida kubwa. Serikali iliingilia kati na kuunda kile kilichoitwa mabenki yaliyokabiliwa na madeni na hatari ya kufilisika na kuunzisha mipango ya kuyaokoa.

Bila shaka serikali inaposadia inakuwa na ushawishi mkubwa zaidi. Kwa maana hiyo enzi ya masoko ya fedha kutosimamiwa vizuri na sheria madhubuti umeshapita. Aliyekuwa na ujasiri wa kunufaiki kutokana na ulegevu wa serikali sasa hana nafasi tena; lazima sasa kubeba dhamana. Ndio maana mkurugenzi wa soko la hisa la Nigeria alifutwa kazi mwezi Agosti mwaka huu na wakuu kadhaa wa mabenki wanasubiri kujibu kesi zinazowakabili mahakamani. Vita dhidi ya rushwa na usimamizi mbaya vinaweza kuwa somo muhimu zaidi linalotokana na mgogoro huu wa kiuchumi.

Mwandishi: Kriesch, Adrian (HA Afrika) /Josephat Charo

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman