Mwito kusaidia mchakato wa amani Mashariki ya Kati
24 Septemba 2010Katika hotuba yake mbele ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York, Rais Obama alisema kuwa ni muhimu kwa pande zote kushirikiana ili katika kipindi cha mwaka mmoja ujao, kuweze kupatikana taifa huru la Palestina na Israel inayoweza kuishi kwa usalama.
Akifafanua alisema kuwa Waisrael na Wapalestina wanapaswa kuleta amani, lakini kila mmoja wetu anawajibika pia kutoa mchango wake.
Baadae Rais Mahmoud Ahmedinejad wa Iran alihotubia baraza hilo. Lakini dakika chache baadae wajumbe wa Marekani walitoka kwenye ukumbi huo,wakifuatwa na wajumbe wengine wa nchi za Ulaya ya Magharibi.
Ahmedinejad alizungumzia juu ya nadharia kuwa serikali ya Marekani ndio iliyohusika na shambulio la Septemba 11 ili iweze kujiimarisha zaidi katika Mashariki ya Kati pamoja na kuimarisha uchumi wake.
Hapo awali Rais Obama alieleza waziwazi kuwa ataendelea kutafuta suluhisho la amani kwa mzozo unaohusika na mradi wa nyuklia wa Iran. Lakini serikali ya Iran mjini Tehran yapaswa kuthibitisha kuwa mradi huo ni kwa ajili ya matumizi ya amani tu.