1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mvutano kati ya Marekani na Pakistan

4 Mei 2011

Siku mbili baada ya kuuawa kwa kiongozi wa ugaidi Osma bin Laden nchini Pakistan, habari zaidi zinajulikana kuhusu operesheni ya Marekani. Ukweli ni kwamba serikali ya Pakistan ilikujajua baadae.

https://p.dw.com/p/RLwV
A Pakistani soldier stands near a compound where it is believed al-Qaida leader Osama bin Laden lived in Abbottabad, Pakistan on Monday, May 2, 2011. Bin Laden, the glowering mastermind behind the Sept. 11, 2001, terror attacks that killed thousands of people was slain in his luxury hideout in Pakistan early Monday in a firefight with U.S. forces, ending a manhunt that spanned a frustrating decade.(Foto:Anjum Naveed/AP/dapd)
Nyumba ambako inasemekana Osama bin Laden alikuwa akiishiPicha: dapd

Wakati ambapo habari zaidi zinajulikana kuhusu operesheni ya Marekani dhidi ya Osama bin Laden, kuna suala moja ambalo bado halikujibiwa. Nani aliemlinda na aliemsaidia kiongozi wa Al-Qaeda, miaka hii yote iliyopita? Wanasiasa wa Kimarekani wamehamakishwa. Kwani bin-Laden alikuwa akiishi Abbottabad katika nyumba inayoenekana wazi kabisa, kwa takriban miaka sita na serikali mjini Islamabad inasema kuwa haikujua cho chote? Kwa maoni ya Carl Levin mbunge wa chama cha Democrat nchini Marekani, hiyo haiwezekani. Amesema:

" Inawezekanaje kwamba jeshi la Pakistani, polisi na idara ya upelelezi hawakujua kuhusu makaazi ya Bin-laden? Kwa miaka mitano ameishi katikati ya mji bila ya kuwasiliana na wengine na alizungukwa na kuta ndefu. Hakuwa na simu wala mawasaliano ya mtandao wa internet."

Kwa maoni ya mbunge Levin, mambo kama hayo lazima yangejulikana. Anasema, sasa serikali ya Pakistan, lazima ijieleze. Hakuna yeyote nchini Marekani anaeweza kuamini kuwa miaka hii yote Osama bin Laden alikuwa akisaidiwa na wafuasi wake tu. Dhana zinazidi kwamba waakilishi wa serikali na jeshi la Pakistan walisaidia kumficha kiongozi wa mtandao wa ugaidi bin-Laden.Lakini, serikali ya Marekani, kamwe haitotamka hivyo rasmi, hata kama tangu muda mrefu imekuwa na wasiwasi kuhusu serikali ya Pakistan mjini Islamabad.

Washirika wasioaminiana

Kwa upande mmoja, Pakistan ni mshirika wa Marekani. Kila mwaka inapokea msaada wa kijeshi wa dola bilioni tatu kutoka Washington. Lakini Marekani haiiamini Pakistan tangu miaka mingi. Na hiyo ndio hali iliyokuwepo, hapo tarehe mosi mwezi huu wa Mei, kikosi maalum cha Marekani "Navy Seals" kilipokwenda kutekeleza operesheni yake dhidi ya Osama bin-Laden.

Mtaalamu wa masuala ya kupiga vita ugaidi wa Rais wa Marekani Barack Obama, John Brennan amesema:

"Sisi hatukuiarifu Pakistan kuhusu operesheni hiyo mpaka watu wetu wote na ndege zetu zote walipoondoka katika anga ya Pakistan."

Ni dhahiri kuwa operesheni hiyo, kisheria inazusha mabishano. Rais wa zamani wa Pakistan, Pervez Musharraf ameikosoa vikali operesheni hiyo. Amesema, ni jambo lisilokubalika kwa vikosi vya kigeni kuvuka mipaka na kufanya operesheni yao. Hiyo ni kukiuka mamlaka ya Pakistan. Kwa maoni yake, ingekuwa bora zaidi kama operesheni hiyo ingetekelezwa na vikosi maalum vya Pakistan.

Mwandishi: Kastan,Klaus/ZPR/P.Martin

Mhariri:M.Abdul-Rahman