Msukosuko wa mabaenki na suluhisho. | Magazetini | DW | 15.10.2008
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Magazetini

Msukosuko wa mabaenki na suluhisho.

Safu za wahariri leo zachambua mapendekezo ya kukabiliana na msukosuko wa fedha duniani na nchini.

Uchambuzi wa safu za wahariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo, umetuwama mno juu ya mada tatu: Mpango uliopitishwa na serikali ya Ujerumani kukabiliana na msukosuko wa mabanki; ripoti juu ya njaa ulimwenguni na uwezekano wa kuzorota uchumi kutokana msukosuko wa fedha duniani .

Kwanza, safu ya mhariri wa gazeti la MUNCHNER MERKUR juu ya mada hii imeandika:

"Kwa kuyakarimu mabenki kwa vitita vya fedha na kutoa ishara ya sura njema ,hakutasaidia kupambana na msukosuko uliozuka.Mawaziri wa fedha waweza tena na tena kupigia upatu dhamana walizotoa za mabilioni ya fedha kuwaokoa mameneja wa mabanki walioshindwa kuendesha kazi zao barabara na wale wahalifu waliofanya biashara ya uvumi, ni wazi mzigo huo unabebwa na walipakodi.

Na baada ya serikali na pamoja na raia kwishatoa mchango wao na mapema kutatua msukosuko huu,sasa ni jukumu la mabanki kufanya hivyo.Mabenki yana wajibu sasa kubainisha wazi hatari zilizojificha katika shughuli zao na kuwataja wale waliohusika katika kuzusha balaa hili lote .

Nalo gazeti la Neue Presse kutoka Hannover linasema kwamba, kutekelezwa haraka hatua hizo za kuyaokoa mabanki ni muhimu mno, kwavile msukosuko huu zamani unatishia kuenea na kuathiri matawi mengine ya uchumi. Gazeti laongeza:

"Mara tu kazi ya kutunga mpango huo wa kuyaokoa mabenki kifedha kukamilika, itapaswa hatua nyengine zaidi zichukuliwe kuutia jeki uchumi."

Likiendeleza mada hii ya kuufufua uchumi unaoanza kuzorota, gazeti la SUWEST PRESSE-laandika:

"....Kustawi uchumi ulimwenguni sasa kumekwama.Na hii haikusababishwa na msukosuko huu wa sasa wa fedha, bali kule kupanda mno kwa bei ya petroli.Kupanda kwa thamani ya Euro kumezidisha mzigo kuumiza uchumi wa nchi za Umoja wa Ulaya.

Kwa jicho hili ,zaweza kusema ni bahati ikiwa makisio ya kuzorota uchumi yaliotolewa majira haya karibuni yakithibitika......Hivi sasa serikali ya muungano ya Ujerumani haiwezi kutenda jengine bali kuridhia kubeba mzigo iliotaka kuutua wa madeni .

FINANCIAL TIMES DEUTSCHLAND lazungumzia pendekezo la Taasisi muhimu za kiuchumi humu nchini zilizodai kuwa, kwa jicho la kuzorota uchumi,raslimali zilizopangwa kutiwa zisiahirishwe .Linadai ada mbali mbali wanazotozwa wananchi na kodi za mapato zipunguzwe.

Gazeti laongeza:

"Ni sawa kabisa kuutia jeki uchumi katika kipindi hiki kigumu. Ingawa kuwapunguzia wananchi mzigo huo kama taasisi za uchumi zinavyodai hakutaonesha haraka maajabu yake kwa kuwa wakati ni mdogo,hatahivyo,zitasaidia kupunguza shida ziliopo wakati huu mgumu.

Gazeti la AUGSBUGER ALLGEMEINE-laandika:

"Hakuna alietia shaka kuwa msukosuko wa fedha ulimwenguni ungeiathiri pia Ujerumani.Lakini, uchumi wa Ujerumani, umemudu hadi wakati huu kuvumilia vishindo vyake.

Hatahivyo, wingu jeusi lililotanda sehemu kubwa ya kambi ya magharibi ,halikuikwepa Ujerumani. Ripoti ya hali ya uchumi iliotoka hivi punde,haitoi matumaini mema kuwa baada ya "dhiki si dhiki,bali faraji".

FLENSBURGER TAGEBLATT linageukia njaa ulimwenguni wakati huu wa msukosuko wa fedha.Laandika:

"Ili kupiga vita njaa ulimwenguni,kunahitaji mkakati wa muda mrefu.Shirika la Umoja wa Mataifa linalopigana na njaa duniani linasema ni aibu kwa ubinadamu hali iliopo.Kupigana na njaa sio tu kuna upande wake wa kiadilifu,kwani kila watu wengi zaidi wakiwa hana neema ya maisha bora, wakati nchi nyengine zinaishi bora tena kupita kiasi,ndipo mifumo ya kiuchumi na kisiasa inavyozidi kupepesuka na kuyumbayumba.Sio tu mabaneki,bali njaa na ufukara kunautosa ubepari katika msukosuko wa kujihalalisha kuwa ni mfumo babara .Ndio maana kuwasaidia wenye njaa kwa sababu za busara tu ni muhimu seuze kwa ubinadamu na uadilifu ".

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com