Msako Luton kuhusiana na shambulio la Sweden | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 13.12.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Timu Yetu

Msako Luton kuhusiana na shambulio la Sweden

Hakuna mtu aliyekamatwa wala hakuna bidhaa za mripuko zilizogunduliwa katika msako huo

default

Taharuki ilitanda Stockholm kufuatia mashambulio ya kigaidi

Polisi ya Uingereza imefanya msako katika nyumba moja kwenye mji wa Luton,Bedfordshire jana usiku chini ya sheria inayosimamia masuala ya ugaidi. Kwa mujibu wa maafisa hao hakuna mtu yoyote aliyekamatwa kutokana na hatua hiyo na wala hakuna bidhaa yoyote inayoweza kutengeneza mripuko iliyogunduliwa katika nyuma hiyo. Aidha huko Sweden kwenyewe polisi nchini humo imearifu kwamba miripuko iliyotokea jumamosi inaangaliwa kama kitendo cha kigaidi kilichofanywa na mshambuliaji mmoja wa kujitoa muhanga.

Inasemekana kwamba mtu huyo alijiripua katika eneo lenye shughuli nyingi za kibiashara katikati ya mji mkuu Stockholm muda mfupi baada ya kutolewa taarifa za kitisho cha kutokea mashambulio hayo kupitia barua pepe,kitisho ambacho kiligusia suala la nchi ya Sweden kuwa na wanajeshi wake nchini Afghanistan pamoja na katuni za mtume Mohammad.

Stockholm Explosionen

Wataalamu wa kuchunguza maiti,wanaangalia mabaki ya mtu aliyejiripua karibu na Drottninggatan,eneo la biashara

Mtaalamu wa masuala ya usalama wa ndani nchini Sweden Magnus Ramberg akizungumzia kulengwa kwa Sweden na magaidi anasema.

''Hakuna sababu ya msingi ya kuelezea kwanini Sweden imekuwa shabaha ya kushambuliwa na magaidi.Kuhusiana na kuhusika kwetu Afghanistan hakuna mjadala mkubwa na katuni zilizochorwa na Lars Vilks haziwezi kulinganishwa na alichokifanya mchora katuni wa Denmark''

Hii leo mchambuzi mkuu wa masuala ya usalama nchini Sweden Malena Remberg amekiambia kituo cha redio nchini humo kwamba polisi inaamini mtu huyo aliyejitoa muhanga katika mashambulio hayo alihusika pia katika kutuma barua pepe zenye vitisho kwa  shirika la habari la Sweden la TT pamoja na kituo cha maafisa wa usalama dakika 10 kabla ya kufanya shambulio hilo jioni. Mpaka sasa bado jina la mtu huyo halijatangazwa hadi jamaa zake watakapoarifiwa ingawa maafisa wa Sweden wanatarajiwa kuwa na mkutano na waandishi wa habari hivi punde.

Katika matukio hayo mawili ya jumamosi,gari liliripuka katikati ya barabara za Drottnigatan na Olof Palmes Gata na watu wawili walijeruhiwa.shambulio la pili likatokea karibu na barabara ya Brygargatan ambako huko mwanamme mmoja alikutikana amefariki.Mtu huyo kwa hivyo inasemekana aliuwawa na mripuko wa bomu  alilokuwa anakusudia kuliripua katika ya umma wa watu lakini liliripuka kabla ya muda wake. Kwa mujibu wa polisi ya Sweden bado uchunguzi unaendelea kubaini ikiwa mtu huyo alishirikiana na watu wengine au alikuwa akifuata maagizo au alihusika peke yake.

Katika barua pepe iliyotumwa kabla ya mashambulio hayo kuna pia sauti iliyoambatanishwa na barua hiyo ya Email sauti ambazo zina ujumbe uliotolewa kwa lugha kadhaa ukiishutumu Swden kwa kujiingiza katika vita vya Afghanistan,pamoja na msanii aliyechora katuni ya mtume Mohammad.  Mshukiwa wa mashambulio hayo anasaidikiwa kuwa ni mzaliwa wa Iraq raia wa Sweden aliyesoma katika chuo kikuu cha Bedfordshire nchini Uingereza ana umri wa kati ya miaka 28 na 29.

Mwandishi :Saumu Mwasimba/DPE/ RTRE

Mhariri : Abdul-Rahman.

 • Tarehe 13.12.2010
 • Mwandishi Saumu Ramadhani Yusuf
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/QWp5
 • Tarehe 13.12.2010
 • Mwandishi Saumu Ramadhani Yusuf
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/QWp5

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com