1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Msafara wa mazishi ya Khamenei wawasili Iraq

8 Julai 2026

Shughuli za mazishi ya aliyekuwa Kiongozi Mkuu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei, zimeanza katika mji mtakatifu wa Najaf nchini Iraq, ambao ni muhimu kwa waislamu wa madhehebu ya Shia.

https://p.dw.com/p/5Gkk0
Irak Nadschaf 2026 | Trauerzug für Ajatollah Ali Chamenei am Imam-Ali-Schrein
Umati mkubwa wa watu waupokea mwili wa Kiongozi mkuu wa Iran, Ayatolla Ali Khamenei wakati wa shughuli za mazishi mjini NajafPicha: Thaier Al-Sudani/REUTERS

Msafara wa mazishi ulianza mapema siku ya Jumatano huku mamia ya maelfu ya waombolezaji wakikusanyika kumuaga kiongozi huyo aliyeuawa takriban miezi minne iliyopita. Rais wa Iran Rais Masoud Pezeshkian, pamoja na viongozi wa kidini na kisiasa kutoka Iraq, walihudhuria mazishi hayo.

Mwili wa Khamenei uliwasili Iraq Jumanne jioni na kupokewa na Waziri Mkuu wataifa hilo, Ali al-Saidi. Wakati uo huo wanamgambo wanaoungwa mkono na  Iran, wanaojulikana kama Popular Mobilization Forces (PMF) nchini Iraq, ambao wanapinga uwepo wa aina yoyote wa Marekani nchini humo, wamedai kuwa kuwa zaidi ya watu milioni mbili walishiriki msafara wa mazishi mjini Najaf, ingawa idadi hiyo haijathibitishwa na vyanzo huru.

Lakini picha zinazoonekana katika vidio huko Najaf zinaonesha  umati mkubwa wa watu wanaoshiriki mazishi hayo.

Iraq ina idadi kubwa ya waislamu wa kishia, na miji ya Najaf na Karbala inachukuliwa kuwa miongoni mwa maeneo yao matakatifu zaidi

Maelfu wamiminika Najaf kumuenzi Ayatollah Ali Khamenei

Baada ya Sala ya Mazishi mjini Najaf, shughuli nyingine za maombolezo zinatarajiwa kufanyika katika mji wa Karbala kabla ya mwili wa Khamenei kurejeshwa Iran. Ayatolla Ali Khamenei anatarajiwa kuzikwa Alhamisi katika mji wake wa kuzaliwa wa Mashhad baada ya siku kadhaa za maombolezo na misafara ya mazishi nchini Iran na Iraq.

Ayatollah Ali Khamenei aliuawa tarehe 28 Februari 2026 siku ya mwanzo kabisa ya mashambulizi ya angani yaliyofanywa na Israel na Marekani dhidi ya Jamhuri hiyo ya kiislamu.

Kifo chake kilisababisha mvutano mkubwa zaidi kati ya Iran, Israel na Marekani, uliogeuka kuwa vita vilivyodumu kwa zaidi ya wiki tano kabla ya kusitishwa kwa mapigano mwezi Aprili. Hata hivyo, ripoti zinaeleza kuwa mashambulizi ya hapa na pale yameendelea kutokea licha ya makubaliano  hayo ya usitishaji vita.

 

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi