1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkuu mwingine wa Siemens ajiuzulu

Maja Dreyer26 Aprili 2007

Siemens ni moja kati ya makampuni makubwa zaidi nchini Ujerumani, na pia ni kampuni kubwa duniani kote. Lakini sasa, shirika hilo limebanwa katika visa vya rushwa ambayo pia ni kubwa zaidi nchini Ujerumani. Hivi karibuni, mwenyekiti wa baraza la wenye hisa, Heinrich von Pierer amejiuzulu kutokana na visa vya rushwa. Jana usiku, mkurugenzi wa Siemens, Klaus Kleinfeld pia amejiuzulu.

https://p.dw.com/p/CHFR
Siemes iko katika hali ngumu
Siemes iko katika hali ngumuPicha: AP

Baadaye leo, kampuni ya Siemes itachapisha takwimu zake za miezi sita iliyopita, na habari hizo kwa kweli ni nzuri sana. Kwa mara ya kwanza, sehemu zote za kampuni hiyo zimeweza kufikia malengo yaliyowekwa na uongozi. Lakini idadi hizo hazitawavutii sana waandishi wa habari, kwani habari motomoto kabisa ni kuhusukujiuzulu kwa mkurugenzi Klaus Kleinfeld, ambaye jana usiku aliarifu ataacha cheo chake wakati mkataba wake utakapomalizika mwezi wa Septemba mwaka huu. Taarifa yake inafuatia mvutano katika bodi ya wakurugenzi juu ya kurefushwa mkataba wa Kleinfeld.

Ikiwa uamuzi huu ungecheleweshwa, shirika la Siemens lingeathirika alisema Kleinfeld pale alipotoa sababu ya kujiuzulu. Amesema:
“Kutojua nini kitakachotokea ni hali ambayo kwangu mimi siwezi kuikubali, wala wafanyakazi, wateja na wenye hisa. Hatua hii ninaichukua wakati kampuni inaendelea vizuri kiuchumi na pia tunafanikiwa katika kuchungua kesi za rushwa. Hapa nataka kusisitiza kuwa sina kosa kuhusiana na jambo hili.”

Wadadisi wa mambo wanasema kuwa kampuni ya Siemens ambayo ina wafanyakazi laki tano duniani kote ina matatizo ya uongozi. Baada ya mwenyekiti wa baraza la wenye hisa, Heinrich von Pierer, kujiuzulu wiki iliyopita imekuwa ni kama kampuni imekatwa kichwa. Baraza la wenye hisa sasa inaongozwa na Gerhard Cromme, lakini mrithi wa wadhifa wa mkurugenzi bado hajatafutwa. Inatarajiwa kutafanyika mjadala hadharani nani ataiongoza Siemens siku za usoni lakini baraza la wenye hisa lina muda hadi mwezi wa Septemba kumteua mkurugenzi mpya.

Kashfa ya rushwa katika kampuni ya Siemens imegonga vichwa vya habari tangu mwezi wa November mwaka jana. Baada ya kuzipekua ofisi kadhaa za Siemens mjini Munich mameneja mbali mbali wamekamatwa na polisi. Kumegunduliwa kuwepo mtandao mkubwa wa malipo ya rushwa. Kwa mujibu wa ofisi ya mwendesha mashtaka wa serikali, kwa ujumla Euro millioni 200 zililipwa kama rushwa na kuwekwa kwenye akauti za siri. Tangu wakati huo, visa vingine vimejulikana kama kwa mfano kuhusiana na malipo kwa wawakilishi wa wafanyakazi. Alipojiuzulu wiki iliyopita, mkuu wa baraza la wenye hisa, Heinrich von Pierer, hakuungama kuwa alifanya kosa.