Mawaziri wa fedha wa G7 kujadili hali ya nishati
9 Machi 2026
Mawaziri wa fedha wa nchi tajiri za kundi la G7 wanakutana baadae leo kujadili uwezekano wa kuruhusu kutumiwa kwa akiba ya dharura ya mafuta, kukabiliana na ongezeko la bei ya mafuta kutokana na vita vinavyoendelea Mashariki ya kati.
Hayo yameelezwa na vyanzo vya serikali ya Ufaransa, ikiripotiwa na gazeti la Financial Times kwamba shirika la kimataifa la kusimamia usalama wa nishati duniani, lijajiunga kwenye mazungumzo hayo.
Gazeti hilo pia limeripoti kwamba nchi tatu za kundi la G7 ikiwemo Marekani mpaka sasa zimeonesha kuunga mkono fikra hiyo.
Mkutano huo umeitishwa katikati ya ongezeko la bei za mafuta kwa zaidi asilimia 25 hivi leo Jumatatu, wakati baadhi ya wazalishaji wakubwa wakisitisha usambazaji pamoja na kuweko khofu ya kuendelea kutatizwa kwa shughuli za usafirishaji bidhaa hiyo kutokana na vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran.