Mkutano wa kimataifa juu ya usalama mjini Munich. | Matukio ya Kisiasa | DW | 05.02.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Mkutano wa kimataifa juu ya usalama mjini Munich.

Mkutano huo unawakusanya maafisa wa ngazi ya juu wa kijeshi na kidiplomasia kutoka sehemu mbalimbali duniani.

Waziri wa nchi za nje wa China Yang Jiechi atakayeufungua mkutano huo .

Waziri wa nchi za nje wa China Yang Jiechi atakayeufungua mkutano huo .

Mkutano wa kimataifa juu ya usalama, unafunguliwa jioni hii katika mji wa kusini mwa Ujerumani wa Munich, huku mawaziri wa mambo ya nchi za nje wa China na Iran wakiwa ni miongoni mwa watakaoshiriki katika mkutano huo ambao unawakusanya kiasi ya maafisa 300 wa ngazi ya juu wa kijeshi, diplomasia na wanasiasa kutoka sehemu mbali mbali duniani.

Mkutano huo wa usalama mjini Munich ambapo Waziri wa mambo ya nchi za nje wa China Yang Jiechi na mwenzake wa Iran Manouacher Mottaki watahutubia, unatajwa kama "Davos ya sera ya usalama " baada ya lile jukwaa la kiuchumi duniani lililofanyika mwezi uliopita katika mji wa mlimani nchini Uswisi.

Mkutano huo wa siku tatu unafuatia siku kadhaa za kuzorota haraka uhusiano wa Marekani na China pamoja na ishara kutoka Iran kwamba huenda ikalikubali pendekezo la nchi za Magharibi kutuma madini ya Uranium nchi za nje ili kurutubishwa.

Hali hiyo inaweza kwa kiasi fulani kuondoa wasi wasi kwamba Iran ina mpango wa kutengeneza silaha za kinuklea. Marekani imemtaka rais Mahmoud Ahmadinejad wa Iran atowe pendekezo madhubuti kwa shirika la nishati ya atomiki la Umoja wa Mataifa.

Mkuu wa mkutano huo wa Munich Wolfgang Ischinger aliiambia televisheni ya umma ARD kwamba amefurahi kuona Iran inatuma ujumbe wa wa ngazi ya juu.

Kwa upande wa China, uungaji wake mkono utahitajika katika kuishinikiza Iran, lakini China imekasirishwa na hatua ya Marekani ya kufikia mkataba wa kuiuzia silaha Taiwan ambayo China inaichukulia kuwa ni sehemu yake na pia tangazo la Marekani la uwezekano wa Rais Obama kukutana na kiongozi wa dini ya Budha wa Tibet Dalai Lama ikulu mjini Washington baadae mwezi huu. China inasema Dalai Lama ni mtu hatari anayepigania kujitenga kwa jimbo hilo la Tibet.

Wakati hutuba ya waziri wa nje wa China ikiwa ni miongoni mwa zile zinazosubiriwa kwa makini,Waandalizi wa mkutano huo wa kimataifa juu ya usalama wa kila mwaka , ukiwa wa 46 , wanataka pia kuzingatia ukuaji wa uchumi wa Asia na umuhimu wake katika jukwaa la kimataifa .

India na Pakistan zinatuma pia wajumbe wa ngazi ya juu katika mkutano huo wa usalama wa Munich. Marekani itawakilishwa na Seneta John Kerry, mshauri wa usalama wa taifa James Jones na mjumbe maalum anayehusika na Afghanistan na Pakistan Richard Holbrooke.

Wengine wanaotarajiwa ni Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Urusi Sergei Lavrov na rais hamid Karzai wa Afghanistan.

Miongoni mwa mada kuu ni uhusiano kati ya Urusi na Marekani na pia wajumbe wanatarajiwa kugusia mkutano wa mwezi uliopita kuhusu Afghanistan mjini London , matarajio ya siku za usoni ya Umoja wa kujihami wa NATO na mizozo inayotokana vyanzo vya maji na matumizi yake pamoja na mali asili nyengine.

Mwandishi:Mohammed Abdul-Rahman

Mhariri: Josephat Charo

 • Tarehe 05.02.2010
 • Mwandishi Nina Markgraf
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/LtwU
 • Tarehe 05.02.2010
 • Mwandishi Nina Markgraf
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/LtwU
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com