1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa kilele mjini Washington

Oumilkher Hamidou13 Aprili 2010

Rais Barack Obama awahimiza viongozi wenzake hatua thabiti zichukuliwe kuepusha silaha za kinuklea zisiingie mikononi mwa magaidi

https://p.dw.com/p/MvTN
Rais Barack Obama na kiongozi mwenzake wa Urusi Dmitri MedvedevPicha: picture alliance / dpa

Rais Barack Obama wa Marekani amewatolea mwito viongozi wenzake 46 wanaohudhuria mkutano wa kilele kuhusu usalama wa kinuklea wapitishe hatua zinazostahiki kuzuwia silaha za kinuklea zisiangukie mikononi mwa magaidi.

Akiwahutubia viongozi wenzake wa kutoka ma taifa 46 na wakuu wa mashirika ya kimataifa ,rais Barack Obama amesema:

"Hii leo fursa tuliyo nayo sio ya kuzungumza tuu bali pia ya kivitendo"- "Sio tuu kuahidi,bali pia kupiga hatua muhimu mbele ili kudhamini usalama wa raia wetu"

"Panahitajika mtazamo wa aina mpya,na wa kina unaochanganya nia,kuanzia nchi moja moja hadi kufikia daraja ya washirika kuweza kukidhi kile ambacho kinahitajika katika enzi hii ya historia." Amesema rais wa Marekani hii leo siku ya pili na ya mwisho ya mkutano wa usalama wa kinuklea.

Rais Barack Obama amehakikisha kwamba miongo miwili baada ya kumalizika vita baridi ,ulimwengu unakabiliwa na kizungumkuti kikubwa kabisa;Kwa upande mmoja anasema rais wa Marekani Barack Obama na hapa tunamnukuu" kitisho cha kuzuka mapambano ya kinuklea kati ya nchi na nchi kimepungua lakini kwa upande wa pili kitisho cha kutokea shambulio la kinuklea kimezidi."

"Makundi ya kigaidi,mfano wa Al Qaida yanajaribu kujipatia vyenzo vya kutosha kuweza kutengeneza silaha za kinuklea,na wakifanikiwa,basi bila ya shaka wataitumia."Na ikiwa hivyo,basi hali hiyo itazusha balaa katika dunia na kusababisha hasara ya maisha ya binaadam pamoja na kuvuruga vibaya sana amani na utulivu duniani."Mwisho wa kumnukuu rais Barack Obama wa Marekani

Nuklear Konferenz Obama und Angela Merkel
Rais Barack Obama na kansela Angela Merkel wa UjerumaniPicha: AP

Maoni kama hayo yametolewa pia na kansela Angela Merkel aliposema:

"Magaidi mfano wa al Qaida,wasiachiwe kwa vyovyote vile kumiliki vyenzo kama hivyo vya hatari wasije wakazidisha hatari iliyopo."

Suala la kuwekewa vikwazo ziada Iran inayotuhumiwa kutengeneza silaha za kinuklea linaonyesha kugubika mkutano huo wa kilele.Hata hivyo afisa mmoja wa ngazi ya juu wa Ujerumani amesema pembezoni mwa mkutano huo wa mjini Washington kwamba kuna dalili za kutia moyo kutoka Moscow na Beijing kuhusu uwezekano wa kuunga mkono vikwazo hivyo.

Jana usiku rais Barack Obama alikuwa na mazungumzo pamoja na kiongozi mwenzake wa China kuhusu suala hilo hilo la vikwazo dhidi ya Iran.

Mwandishi:Hamidou,Oummilkheir/ AP/Reuters/afp

Mpitiaji:Mohammed Abdul-Rahman