Mkataba wa Kyoto watimiza miaka kumi | Matukio ya Kisiasa | DW | 10.12.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Mkataba wa Kyoto watimiza miaka kumi

Je ni kitu gani kitakachofuata baada ya mkataba huo kumalizika hapo mwaka wa 2012.

default

Mkataba wa Kyoto unapigania kupunguza gesi chafu za viwandani

Macho yote yanazikodolea siku za mkutano kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa unaoendelea katika kisiwa cha Bali nchini Indonesia. Wajumbe wa mkutano huo wanataka kufikia makubaliano yatakayosaidia kupiga hatua mbele katika juhudi za kuyalinda mazingira.

Je uchafuzi wa mazingira kupitia gesi ya carbon dioxide utakabiliwa vipi baada ya mwaka wa 2012 wakati mkataba wa Kyoto utakapomalizika? Je ni sheria gani zilizojumulishwa katika mkataba huo wa Kyoto?

Mkataba wa kimaitaifa unaoshughulikia kuyalinda mazingira wa Kyoto ulianza kutekelezwa mnamo mwaka wa 1997. Katika mkutano uliofanyika mjini Kyoto nchini Japan, Umoja wa Mataifa kwa mara kwanza ulifaulu kufikia makubaliano ya kisheria kuhusu njia za kuyalinda mazingira.

Kwanza kabisa mkataba wa Kyoto unazitaka nchi zilizoendelea zaidi kiviwanda duniani zibebe jukumu kubwa la kupunguza kwa kiwango kikubwa gesi zinazotoka viwandani. Mwaka unaotumiwa kama kigezo cha kulinganisha ufanisi katika juhudi hizo ni mwaka wa 1990. Kufikia mwaka wa 2012 Umoja wa Ulaya unataka kuwa chini ya kiwango cha carbon dioxide mwaka wa 1990 kwa asilimia nane.

Canada na Japan kwa upande wao zinataka kuwa asilimia sita chini ya kiwango hicho, huku Marekani ikiwa imeahidi kufikia kiwango cha asilimia saba kufikia mwaka wa 2012. Rais wa zamani wa Marekani, Bill Clinton, alitia saini mkataba wa Kyoto lakini bunge la Marekani na baraza la senate likakataa kuuidhinisha uamuzi wa kiongozi huyo.

Inavyoonekana hivi sasa nchi zilizoendelea zaidi kiviwanda duniani hazijafaulu kupitia uwezo wao kufikia viwango vya kupunguza gesi za viwandani. Lakini tayari zimeshiriki kwenye mazungumzo kuhusu mkataba wa Kyoto hivi kwamba zinalazimika kulipia gharama ili ziondokane na lawama. Kuna uwezekano mbalimbali. Miongoni mwa mambo mengine nchi zilizoendelea zaidi kiviwanda duniani zinaweza kulipia gharama ya teknolojia ya kisasa inayotumika katika kuyalinda mazingira. Kwa kufanya hivyo nchi hizo zinaweza kupata manufaa makubwa.

Mkataba wa Kyoto pia unaelezea adhabu dhidi ya nchi zitakazoshindwa kutimiza majukumu yao kuhusiana na kupunguza gesi za viwandani katika juhudi nzima ya kuyalinda mazingira. Hilo ni jambo la kusisimua sana katika sekta ya mazingira.

Nchi zinazoinukia haraka kiuchumi kama vile China na India pia zimefungamanishwa katika mkataba wa Kyoto. Lakini kufikia sasa nchi hizo hazijajiwekea viwango maalumu vya kupunguza gesi za viwandani. Kwa hiyo hazilamiziki kupunguza gesi hizo kwa kiwango fulani. Mjadala mkubwa ulikuwa kwanza nchi zilizoendelea kiviwanda ziondoe uchafu ambao zimekuwa zikiulimbikiza katika miongo iliyopita.

Kufikia sasa nchi 175 zimeuidhinisha mkataba wa Kyoto. Lakini mkataba huo utaendelea kufanya kazi hadi mwaka wa 2012. Ndio maana mkutano unaofanyika katika kisiwa cha Bali nchini Indonesia unatakiwa kujadili hatua zitakazochukuliwa wakati muda wa mkataba wa Kyoto utakapomalizika mwaka wa 2012. Mkataba wa Kyoto ndio sababu msingi ya mkutano huo wa Bali.

 • Tarehe 10.12.2007
 • Mwandishi Josephat Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CZja
 • Tarehe 10.12.2007
 • Mwandishi Josephat Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CZja
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com