1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mivutano ingalipo kati ya Ujerumani na Uturuki

Oumilkheir Hamidou
28 Septemba 2018

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan anaendelea na ziara yake Ujerumani. Baada ya mazungumzo pamoja na rais wa shirikisho Frank-Walter Steinmeier, amekutana na kansela Angela Merkel

https://p.dw.com/p/35f0y
Berlin Staatsbesuch Erdogan PK mit Kanzlerin Merkel
Picha: picture-alliance/dpa/M. Kappeler

Mizizi ya fitina ni mingi mno katika uhusiano kati ya Ujerumani na Uturuki. Na licha ya azma ya kupunguza mivutano, hali hiyo haikufichika wakati wa mkutano na waandishi habari kati ya kansela Angela Merkel na rais wa Uturuki Erdogan. Kansela Merkel amekiri baada ya mazungumzo yao "hitilafu za maoni" ni kubwa mno . Kansela Merkel amezitaja hitilafu hizo kuwa ni pamoja na kuwekewa vizuwizi uhuru wa vyombo vya habari na haki za binaadam. Mabishano makubwa zaidi yanatuwama katika kadhia ya mwandishi habari wa kituruki, mharriri mkuu wa zamani wa gazeti la Jumhuria anaeishi Ujerumani Can Dündar na hali wanayokabiliana nayo raia wa Ujerumani wanaoshikiliwa jela nchini Uturuki.

Rais Recep Tayyip Erdogan na kansela Angela Merkel wakizungumza na waandishi habari
Rais Recep Tayyip Erdogan na kansela Angela Merkel wakizungumza na waandishi habariPicha: Reuters/F. Bensch

Erdogan anaitaka Ujerumani iwarejeshe wafuai wa Vuguvugu la Gülen

Rais Erdogan anashikilia Dündar arejeshwe Uturuki akihoji mwandishi habari huyo ni jasusi, amefichua siri za taifa kwa hivyo lazima arejeshwe Uturuki. Rais Erdogan anaitaka Ujerumani pia iwaandame magaidi. Anasema maelfu ya wafuasi wa chama cha PKK anaowaita magaidi pamoja na mamia ya wafuasi wa vuguvugu la Gülen wanaishi nchini Ujerumani. Serikali ya Uturuki inamtuhumu shekhe wa kituruki anaeishi Marekani Fethullah Gülen kuwa nyuma ya njama iliyoshindwa ya mapinduzi ya july 2016.

Kwa upande mwingine kansela Angela Merkel ametilia mkazo masilahi ya pamoja yaliyoko kati ya Uturuki na Ujerumani. Ametaja kwa mfano ushirikiano katika jumuia ya kujihami ya NATO, wahamiaji na mapambano dhidi ya ugaidi. Kansela Angela Merkel ameendelea kusema: "Kwa jumla tunaweza kusema, kwa upande mmoja kuna mkakati wa kuendeleza uhusiano kwa masilahi ya pamoja. Na kwa upande wa pili  sintofahamu au hitilafu za maoni ni kubwa mno na hasa katika mada zinazohusiana na mfumo wa demokrasia,uhuru na jamii ya uwazi. Na hilo linabainika sio tu kwa kua baadhi ya raia wa Ujerumani wangali bado wanashikiliwa korokoroni. Kwa hivyo ziara kama hii ni muhimu kwasababu tutaweza tu kuzipatia ufumbuzi tofauti zilizoko kupitia njia ya mazungumzo."

Maandamano ya wanaharakati wa haki za binaadam dhidi ya ziara ya Erdogan nchini Ujerumani
Maandamano ya wanaharakati wa haki za binaadam dhidi ya ziara ya Erdogan nchini UjerumaniPicha: Reuters/C. Mang

Erdogan azungumza na wanauchumi

Jioni  rais wa Uturuki amepangiwa kukutana na wawakilishi wa sekta za kiuchumi kwa lengo la kuimarisha uhusiano kati ya makampuni hayo na Uturuki. Zaidi ya makampuni 6500 na watumishi 120.000 wa Ujerumani wanaendesha shughuli zao Uturuki. Usiku rais Erdogan na mkewe Amina watahudhuria karamu rasmi ya chakula iliyoandaliwa kwa hishma yao na rais wa shirikisho Frank-Walter Steinmeier.

Mwandishi:Hamidou/KNA/Reuters/dpa

Mhariri: Gakuba, Daniel