Misri na msukosuko wa Kiuchumi | Masuala ya Jamii | DW | 02.06.2011
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Masuala ya Jamii

Misri na msukosuko wa Kiuchumi

>Maafisa wa Misri wanaonya kwamba nchi hiyo iliyotoka kwenye mkondo wa vuguvugu la kudai demokrasia lililosababisha kuondolewa madarakani Hosni Mubarak inaweza kukabiliwa na mgogoro mkubwa wa kiuchumi,

default

Watalii wengi wanaogopa kuitembelea Misri baada ya machafuko ya karibuni

Wasiwasi huo umetolewa na Generali Mahmoud Nasar mwanachama wa baraza kuu la kijeshi linaloiendesha serikali ya mpito ya Misri kwa hivi sasa.Mapema wiki iliyopita aliuambia mkutano wa kiuchumi mjini Cairo kwamba uwekezaji kutoka makampuni ya kigeni umesimama wakati mashirika ya nchi za Magharibi  yanayotathmini hali za kiuchumi  yakijaribu kuweka katika kiwango cha chini uchumi wa taifa hilo.Aidha hali ya umaskini nchini humo imeongezeka zaidi na kufukia asilimia 70. Mwanauchumi John Sfakianakis kutoka Misri akizungumzia juu ya kuendelea kuzorota kwa hali ya uchumi katika taifa hilo anasema.

''Hali itakuwa mbaya zaidi kuliko hivi sasa ikiwa tutaendelea kuwa na wasiwasi wa kisiasa,ghasia na watalii kutotakiwa kutembelea Misri.Biashara ya kigeni na Misri inaendelea kwenda chini.Hali hii ikiendelea basi bila shaka itasababisha athari kubwa katika uchumi wa Misri.''

        Kupungua kwa uwekezaji wa makampuni ya Kigeni

Ägypten Scharm El-Scheich Haiattacke

Utalii ni mojawapo ya sehemu kubwa ya kuingiza pato nchini Misri

Mamlaka inayosimamia uwekezaji na maeneo huru ya kibiashara GAFI ambayo kazi kubwa ni kuvutia biashara za kigeni nchini Misri inasema kwamba uwekezaji wa kigeni katika taifa hilo umepungua kwa dolla millioni 500 katika kipindi cha robo ya kwanza ya kiuchumi ya mwaka 2011.Waziri wa fedha wa nchi hiyo pia amebashiri kwamba kutakuweko na alau asilimia 9 ya nakisi ya bajeti mwaka huu wakati ukuaji wa kiuchumi ukipungua kwa 2 asilimia kutoka asilimia 5 iliyokuwa imebashiriwa kabla ya kutokea vuguvugu la kudai demokrasia ambalo kwa kiasi kikubwa lilichangiwa na hali ya umaskini inayowakabili wananchi wengi wa Taifa hilo. Foud Riad mkuu wa baraza la kitaifa la  haki za binadamu nchini Misri anasema.

''Anafikiri adui mkubwa hivi sasa atakuwa ni umaskini na njaa,Ikiwa watu watakumbwa na njaa basi wanaweza kufanya kitu chochote,na kutakuweko na janga na balaa na vuguvugu jingine lakini nafikiri maendeleo ndio kitu muhimu kinachotakiwa hivi sasa.''

                              Matumizi ya Misri

Serikali ya Misri imesema kwamba kiwango cha matumizi ya Taifa hilo  katika Chakula na Nishati kitaongezeka kwa asilimia 40 mwaka huu ikilinganishwa na mwaka jana na kuifanya hali kuwa ngumu zaidi katika suala la bajeti.

Juu ya hilo wasiwasi mwingine ni pamoja na suala la nchi hiyo kuchukua dolla billioni 8 kutoka  hazina yake iliyoko nje katika kipindi cha miezi mitatu pekee iliyopita hiyo inamaana kwamba sasa imebakisha dola billioni 28 kutoka kiwango cha dolla billioni 36 ilizokuwa nazo kama akiba mwezi Desemba.Kiwango hicho kinaweza kuisaidia kwa muda mfupi sana katika kuagiza vitu muhimu kama vile Sukari,ngano na mafuta.Misri iliyo na wakaazi millioni 86 inategemea zaidi vyakula vya kuagiza kutoka nje.Tangu mwanzoni mwa mwaka huu sarafu ya Misri iliteremka thamani kwa asilimia 2.

                            Fedha za kigeni

Taifa hilo pia linakabiliwa na tatizo la kupungua kwa mapato na hasa katika sekta ya utalii na fedha za kigeni zilizokuwa zinaingizwa na wamisri wanaofanya kazi nje.Kabla ya kuanza kwa machafuko katika nchi jirani ya Libya mamilioni ya Wamisri waliokuwa wakifanya kazi Libya walikuwa wakituma nyumbani mamilioni ya Dolla kila mwaka.Sekta ya utalii ya Misri iliyokuwa ikifanya vizuri katika kipindi cha nyuma sasa inapoteza dola Bilioni Moja kila mwezi kutokana na watalii wengi kuogopa kutembelea nchi hiyo tangu kuzuka kwa vuguvugu la mapinduzi.

Mwandishi Saumu Mwasimba

Mhariri Josephat Charo.

 • Tarehe 02.06.2011
 • Mwandishi Saumu Ramadhani Yusuf
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/11T5u
 • Tarehe 02.06.2011
 • Mwandishi Saumu Ramadhani Yusuf
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/11T5u
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com