Miaka minne tangu kuanguka kwa utawala wa Saddam. | Matukio ya Kisiasa | DW | 09.04.2007
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Miaka minne tangu kuanguka kwa utawala wa Saddam.

Tarehe 9 Aprili 2003 majeshi ya Marekani yaliliingia katikati ya mji mkuu wa Iraq Baghdad, na utawala wa Saddam Hussein ukaangushwa, dikteta akatupwa nje ya utawala wake, na pia baadaye alikamatwa akiwa amejificha katika shimo. Huo ulikuwa mwisho wa miaka 24 ya utawala wake wa kidikteta. Mwisho ambao hata hivyo ulijionyesha tangu mwanzoni mwa miaka ya 90. Marlis Shaum anaelezea matukio muhimu katika vita vya Marekani dhidi ya Iraq na hatimaye kungushwa kwa Saddam Hussein

Saddam Hussein akiwa kizimbani, wakati wa kesi yake mjini Baghdad.

Saddam Hussein akiwa kizimbani, wakati wa kesi yake mjini Baghdad.

Baada ya vita dhidi ya Iran katika miaka ya 80 akiba yake ya fedha ilipungua sana. Tarehe 2 August 1990 aliyaamuru majeshi yake kuingia katika nchi jirani yenye utajiri mkubwa wa mafuta ya Kuwait.

Siku moja tu baada ya majeshi hayo kuingia nchini Kuwait baraza la usalama la umoja wa mataifa liliweka vikwazo vya kiuchumi dhidi ya Iraq. Dikteta huyo akalazimika kugawa vyakula kwa wananchi wake. Hakutana hata hivyo kusalim amri. Januari 17 mwaka 1991, rais wa wakati huo George Bush baba yake rais wa sasa alizungumza na taifa. Alikuwa na haya ya kusema;

Majeshi ya muungano yameanza mapambano ndani ya Iraq na Kuwait. Mapambano haya yanaendelea wakati huu nikizungumza. Hadi sasa majeshi ya ardhini hayajahusishwa. Saddam Hussein ameanzisha vita hivi miezi mitano iliyopita dhidi ya Kuwait, usiku wa leo tumeamua kuanzisha vita hivi.

Siku 12 baadaye vita vikamalizika.

Lakini vikwazo vya kiuchumi vilivyowekwa na baraza la usalama la umoja wa mataifa viliendelea kubaki. Na umoja wa mataifa ukaidhinisha azimio namba 687, ambalo Iraq ililikubali: Iraq inatakiwa kuanzia sasa kutokuwa na silaha za maangamizi ama kununua ama kutengeneza makombora yenye uwezo wa kufikia zaidi ya kilometa 150.

Wachunguzi wa umoja wa mataifa wakaanza udhibiti wa silaha za maangamizi za Iraq. Lakini hata hivyo Saddam Hussein alikuwa kila mara akizuwia kazi hiyo. Katika mwezi wa March 1996 aliwakatalia kwa mara ya kwanza wachunguzi hao kuingia katika maeneo ya kijeshi. Mwaka 1998 umoja wa mataifa ukawaondoa wachunguzi wake. Alijaribu pia kuchafua mipango mipya ya majadiliano.

Mwaka 2001 mataifa ya magharibi yalibadilisha lugha yao kuielekea Iraq. George W Bush akawa rais wa Marekani. Alitangaza kuwa Saddam Hussein amevunja maazimio ya umoja wa mataifa na badala yake ni lazima aadhibiwe. Vikwazo vipya dhidi ya Iraq vikaidhinishwa.

Mashambulizi ya kigaidi ya Septemba 11 2001 yalikuja kati yake. Baada ya hapo Marekani ikachukua hatua kali zaidi. Rais George W. Bush alisema kuwa anaushahidi , kuwa Iraq ina silaha za maangamizi na kwamba kuna uhusiano kati ya Iraq na mtandao wa kimataifa wa ugaidi. Na Tarehe 11 Septemba 2002, rais George W. Bush alizungumza mbele ya baraza kuu la umoja wa mataifa na akasema: Tunanukuu,

Kama utawala wa Iraq unataka amani, unalazimika haraka na bila masharti , iachane na mpango wake wa silaha zake za maangamizi na makombora ya masafa marefu. Kama utawala huu wa Iraq unataka amani unatakiwa haraka kuacha kuusaidia ugaidi na kusaidia kupambana na ugaidi, kama yalivyo mataifa mengine baada ya azimio la baraza la usalama la umoja wa mataifa.

Wiki moja baadaye alionyesha ishara Saddam Hussein kuwapo kwake tayari kuwarejesha wachunguzi wa kimataifa.

Tarehe 16 March 2003 walikutana rais Bush wa Marekani, waziri mkuu wa Uingereza Tony Blair na waziri mkuu wa Hispania Aznar nchini Hispania. Walimpa Saddam Hussein muda wa saa 24. Anatakiwa ajiuzulu ama aende uhamishoni. Dikteta huyo wa Iraq hakukubali.

Na Aprili 9 , 2003 majeshi ya Marekani yaliingia katikati ya mji wa Baghdad. Na utawala wa miaka 24 wa Saddam Hussein ukafikia mwisho.

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com