Mgogoro wa Ireland na Mwanamfalme William kuchumbia | Magazetini | DW | 17.11.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Magazetini

Mgogoro wa Ireland na Mwanamfalme William kuchumbia

Wahariri walikuwa na mengi ya kutia moyo hii leo licha ya mgogoro wa fedha unaotishia kuigubika Ireland

default

Watu wanapita karibu na benki ya Ireland inayokumbwa na matatizo ya fedha

Mgogoro wa fedha nchini Ireland,wanajeshi wa Ujerumani wawatimua wataliban kaskazini mwa Afghanistan na mwanamfalme William wa Uengereza achumbia, ni miongoni mwa mada zilizohanikiza magazetini hii leo.

Tuanzie, lakini, na mgogoro wa fedha nchini Ireland. Gazeti la "Stuttgarter Zeitung" linaandika"Kile ambacho Ireland inakihitaji zaidi hivi sasa ni subira pamoja na wakati wa kutosha ili kuzidurusu hesabu zake kwa msaada wa nchi zinazotumia sarafu ya Euro. Kwa sababu bado kuna matumaini mema. Sio data zote zinaashiria hali ya kutisha ya kiuchumi. Jaribio la pupa, lakini la kutaka kuziba mapengo yaliyojitokeza katika benki na kutoa sura nchi hiyo inaweza kuaminiwa kupatiwa mikopo, limeidhuru badala ya kuisaidia nchi hiyo. Mabadiliko yanategemewa, na pengine hata kabla ya mwaka huu kumalizika. Awamu hii ya mapambazuko, mtazamo wa aina mpya na udhibiti wa wasomi wake ni mambo ambayo jamhuri hiyo ndogo ya kaskazini magharibi ya Ulaya italazimika yenyewe iyatekeleze.

Gazeti la "Nürnberger Nachrichten" linazungumzia hali namna ilivyo huko Ireland na kuandika:"Hali katika nchi za eneo la Euro ni ngumu: mataifa yanayodaiwa yanahofia mamlaka yao, nayo mataifa fadhili yanahofia mali zao.Taasisi pekee ambazo hazina cha kuhofia ni mabenki makubwa makubwa. Benki hizo zimeshaelezea utayarifu wa kuwapatia wa-Ireland mikopo mikubwa mikubwa-tena bila ya kudai kinga ya aina yoyote. Funzo linalotokana ni hili: miaka mitatu baada ya kuripuka mgogoro wa fedha, bado natija zinaendelea kujaza makasha ya kibinafsi na hasara kufidiwa kwa fedha za walipa kodi.

Mada ya pili magazetini inahusu kutimuliwa wataliban na wanajeshi wa Ujerumani wanaotumikia vikosi vya kimataifa vya kulinda amani nchini Afghanistan-ISAF. Gazeti la "Braunschweiger Zeitung" linaandika:"Opereshini hiyo ya jeshi la shirikisho-Bundeswehr dhidi ya wataliban katika eneo hatari la kaskazini mwa Afghanistan, inasherehekewa kama ni ushindi licha ya kuwekwa siri. Angalao opereshini ya kijeshi imesaidia kidogo kupunguza uchungu wa kupotelewa na wenzao na hali ya kutojuwa la kufanya baada ya iopereshini kama hizo kushindwa kuleta tija. Hata hivyo, hakuna sababu ya kushangiria.Kwa sababu, kwa vyovyote vile, wanajeshi wa Ujerumani wanalazimika kuihama nchi hiyo haraka iwezekanavyo. Na huenda uamuzi ukafikiwa mwakani."

Flash-Galerie Prinz William und Kate Middleton

Mwanamfalme wa Uengereza William na mchumba wake Kate Middleton-harusi itasherehekewa msimu wa kiangazi mwakani

Na hatimae magazeti ya Ujerumani yalizungumzia pia kuhusu kuchumbia mwanamfalme William wa Uengereza. Gazeti la "Emder Zeitung" linaandika"William anafanya kile ambacho baba yake, ingawa alitaka lakini hakuruhusiwa: anamuowa bibi yule yule anaempenda kwa dhati. Yeye bado ni kijana, na analingana na wakati wake. Baba yake alikuwa tayari miaka 30, kwa hivyo mtu mzima kidogo kuliko yeye. Kuvikwa Charles taji la ufalme ni sawa na kuirejea katika enzi za kale, lakini William anaweza kuleta enzi mpya.Hata hivyo, Charles anaweza kusaidia-Anaweza kugharimia sherehe hiyo ya harusi ya mwanawe.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir /Inlandspresse

Mpitiaji: Miraji Othman

 • Tarehe 17.11.2010
 • Mwandishi Oumilkher Hamidou
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/QB5Z
 • Tarehe 17.11.2010
 • Mwandishi Oumilkher Hamidou
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/QB5Z