1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Medvedev ashinda uchaguzi wa Urusi kwa kishindo kikubwa

Josephat Charo3 Machi 2008

Medvedev amepata zaidi ya asilimia 70 ya kura lakini upinzani watishia kuwasilisha kesi mahakamani

https://p.dw.com/p/DH0q
Rais wa Urusi anayeondoka Vladamir Putin (kushoto) na Medvedev baada ya uchaguzi kumalizikaPicha: AP

Dmitry Medvedev amechaguliwa rais mpya wa Urusi kuchukua nafasi ya rais anayeondoka, Vladamiri Putin. Hayo ni kwa mujibu wa matokeo ambayo yanakaribia kukamilika yaliyotangazwa leo na tume kuu ya uchaguzi ya Urusi. Lakini inaripotiwa uchaguzi huo haukufanyika kwa njia ya demokrasia.

Kiongozi wa tume ya uchaguzi nchini Urusi, Vladamir Churov, amesema matokeo yanayompa ushindi Dimtry Medvedev yanafuatia kuhesabiwa kwa asilimia 99.4 ya kura zote zilizopigwa.

Kwa mujibu wa matokeo hayo Medvedev ameshinda asilimia 70.23 ya kura mbele ya mpinzani wa chama cha kikomunisti, Gennady Zyuganov, ambaye amejipatia asilia 17.76 ya kura.

Nafasi ya tatu inashikiliwa na Vladimir Zhirinovsky ambaye ameshinda asilimia 9.37 akifuatiwa katika nafasi ya nne na mgombea urais ambaye hana umaarufu mkubwa nchini Urusi, Andrei Bogdanov, aliyepata asilimia 1.29 pekee ya kura.

Idadi ndogo ya kura ambazo bado hazijahesabiwa zilipigwa katika nchi za kigeni barani Asia na Marekani.

Uchaguzi ulikuwa huru na wa haki

Licha ya machafuko kuripotiwa katika sehemu mbalimbali nchini Urusi, kiongozi wa tume ya uchaguzi, Vladimir Churov, amesema uchaguzi ulifanyika bila matukio yoyote ya kuutatiza. Kiongozi huyo amesema hawakugundua visa vyovyote vya wizi wa kura au kubadili matokeo ya uchaguzi huo. Amesema wapigaji kura asilimia 69.61 kati ya wapigaji kura wote milioni 108.95 waliojiandikisha walijitokeza kupiga kura.

Idadi kubwa ya wapigaji kura ilijitokeza katika eneo la Caucusus Kaskazini huku asilimia 91 ikijitokeza huko Chechnya, asilimia 92 katika eneo jirani la Ingushetia na asilimia 90 huko Dagestan.

Sherehe ilikuwa kamilifu hapo jana jioni. Baada ya muziki wa bendi maarufu ya Urusi, Ljubej, rais anayeondoka Vladamir Putin na rais mteule, Dimtry Medvedev, walitembea pamoja katika eneo lililokuwa limepambwa na mazulia mekundu.

Zaidi ya vijana 40,000 walisherehekea ushindi wa Medvedev pamoja na bendi inayocheza muziki wa miondoko ya ´Rock´ Russija Vperjod, yaani ´Urusi isonge mbele´ huku mvua kubwa ikinyesha.

Rais mpya wa Urusi, Medvedev akiwa amevalia jaketi la ngozi alizungumza kwa umati wa watu na kusema, ´Ningependa kutoa shukurani zangu kwa wale wote walionichagua. Kwa sababu tunakaribia thuluthi mbili ya raia wote nchini mwetu. Hali yetu ya baadaye ni muhimu sana kwetu na tunaweza kuendeleza mkondo uliopendekezwa na rais Putin. Tuna nafasi zote kuweza kufanya hivyo. Kwa pamoja tutashinda´

Baadaye umati wa watu ulipiga kelele kumuita mshindi halisi wa uchaguzi huo, rais Putin. Katika baridi kali na mvua kubwa rais Putin akasema, ´Naomba munipe dakika moja tafadhali nizungumze!! Uchaguzi wa rais wa Urusi umekamilika. Mgombea wetu Dimtry Medvedev anaongoza kwa idadi kubwa ya kura. Nawashukuru nyote pamoja na wananchi wote wa Urusi. Hii inadhihirisha wazi kwamba tunaishi katika taifa lenye demokrasia na taasisi zetu za kijamii zinatekeleza majukumu yake kikamilifu na kwa ufasaha. Uchaguzi wa rais umefanyika kulingana na katiba na sheria. Nina matumaini kwamba kampeni za uchaguzi sasa ni jambo lililokwisha pita.´

Alipomaliza kuzungumza rais Putin umati huo wa watu ulipiga kelele ukisema ´Urusi isonge mbele´.

Kulikuwa na shinikizo kubwa

Mwanasiasa wa Ujerumani wa sera za kigeni, Marie Luise Beck, wa chama cha Kijani na ambaye amekuwa akifuatilia uchaguzi wa Urusi kwa muda mrefu anasema wakati huu kulikuwa na shinikizo kubwa kuwataka watu wajitokeze kupiga kura.

´Inaonekana safari hii kulikuwa na shinikizo kubwa ikilinganishwa na uchaguzi wa bunge la Urusi, Duma, hasa kwa watu ambao hawangekwenda kupiga kura. Kila mahali watu walishinikizwa! Wanafunzi katika makazi yao walikwenda kupiga kura wakati wa muda wa mapumziko ya mchana. Kulikuwa na shinikizo kubwa kuiongeza idadi ya wapigaji kura. Hata katika uamuzi wa nani kumpigia kura, shinikizo lilitumika. Inaripotiwa katika kituo kimoja kulikuwa na malipo ya Rubel 400 kwa kila mtu aliyempigia kura Medvedev. Hizo ni kama euro 11 hivi.´

Waangalizi wa nchi za magharibi waliousimamia uchaguzi wa Urusi watatoa tathmini yao hii leo mjini Moscow. Mbunge wa Uingereza, Nigel Evans, amesema timu ya waangalizi 23 wa nchi za magharibi inahisi mapendekezo ya kufanya uchaguzi huru na wa haki hayakuzingatiwa.

Upinzani nchini Urusi umetishia kuwasilisha kesi mahakamani kuhusu matokeo ya uchaguzi huo.