1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mdahalo mkali kabla ya chaguzi za Ohio na Texas

P.Martin27 Februari 2008

Nchini Marekani,mahasimu wa chama cha Demokratik Hillary Clinton na Barack Obama Jumanne usiku walibadilishana maneno makali wakati wa mdahalo wao wa dakika 90 mjini Cleveland,Ohio.

https://p.dw.com/p/DE1P
*** Schmiester, Schluss mit freundlich? - Letztes Obama-Clinton-TV-Duell vor den Vorwahlen in Texas und Ohio *** Democratic presidential hopefuls Sen. Hillary Rodham Clinton, D-N.Y., left, and Sen. Barack Obama, D-Ill., shake hands after a Democratic presidential debate Tuesday, Feb. 26, 2008, in Cleveland. (AP Photo/Mark Duncan)
Maseneta Hillary Clinton na Barack Obama baada ya mdahalo wa Jumanne usiku 28 Feb.2008 mjini Cleveland,OhioPicha: AP

Mdahalo wa Jumanne usiku huenda ukaamua matokeo ya chaguzi zitakazofanywa katika majimbo mawili muhimu ya Ohio na Texas hapo tarehe 4 mwezi ujao.Kinyume na midahalo ya hapo awali kugombea kuteuliwa kupigania uchaguzi wa rais,maseneta Hillary Clinton na Barack Obama wa chama cha Demokratik,walitupiana maneno makali-kila mmoja akitetea sera zake kuhusu vita vya Irak,matunzo ya afya pamoja na sera za nchi za nje na walisisitiza tofauti kuu zilizopo katika misimamo yao.

Seneta Clinton mwenye umri wa miaka 60 alijitetea kuwa ana uzeofu wa kisiasa kuweza kukabiliana na mkongwe wa chama cha Republikan John McCain.Akaongezea kuwa kumeshuhudiwa matokeo ya huzuni, ya kuwa na rais asiye na uzeofu wala werevu wa kuongoza sera za nje na kulinda usalama wa taifa.Amesema hilo ni jambo lisilopasa kuruhusiwa tena.

Seneta Barack Obama wala hakusita kutoa jawabu lake.Akasema kuwa Clinton anachanganya mambo mawili: yaani uzeofu na kuwepo muda mrefu katika uwanja wa kisiasa.Akakumbusha kuwa katika mwaka 2002 Marekani ilipokabiliwa na uamuzi muhimu kabisa katika sera zake za nje iwapo iende vitani dhidi ya Irak au la,yeye alieleza wazi wazi sababu ya kutokwenda vitani,lakini Clinton alipiga kura kuidhinisha kuivamia Irak.

Clinton akajibu kuwa Obama anastahili kusifiwa kwa kupinga vita hivyo wakati wote,lakini akasisitiza kuwa baadae,wote wawili bungeni walipiga kura kuendelea kugharimia operesheni hizo za kijeshi.

Clinton alitazamiwa kuendelea kuishambulia kambi ya Obama kufuatia lugha kali aliyotumia wakati wa mdahalo wa juma lililopita katika jimbo la Texas.Huko Seneta Clinton alimshambulia vikali Obama kuhusu vijarida vilivyosambazwa hivi karibuni na kambi ya Obama.Clinton alilalamika kuwa vijarida hivyo vilivyohusika na sera zake za afya ni uongo na vinapotosha.

Obama alijibu kwa kusema kuwa yaliyokuwemo katika vijarida hivyo ni sawa sawa.Obama,katika mradi wake wa afya anataka kupunguza gharama,wakati Clinton akishikilia kuwa kila mmoja lazima ajikatie bima ya afya.

Hillary Clinton aliumaliza mdahalo huo kwa kukariri kwamba ilikuwa heshima kubwa kufanya kampeni kando ya Obama. Juu ya hivyo akaongezea kuwa atajitahidi awezavyo kujipatia ushindi.Amesema,ni kampeni ya kihistoria kwani kuna uwezekano wa kuwepo rais wa kwanza wa kike au rais mweusi wa kwanza nchini Marekani.