Mazungumzo ya Lausanne yaongezewa muda | Matukio ya Kisiasa | DW | 01.04.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Mazungumzo ya Lausanne yaongezewa muda

Licha ya Iran na mataifa makubwa duniani kutofikia makubaliano hadi sasa kwenye mazungumzo juu ya nyuklia ya Iran, kuna dalili nyingi za kupatikana kwa mkataba huku yakiongezewa siku moja.

Maafisa na wajumbe wa mazungumzo ya nyuklia ya Iran wakisubiri kuanza kwa kikao chengine cha majadiliano mjini Lausanne, Uswisi.

Maafisa na wajumbe wa mazungumzo ya nyuklia ya Iran wakisubiri kuanza kwa kikao chengine cha majadiliano mjini Lausanne, Uswisi.

Chanzo kimoja kutoka ujumbe wa Ujerumani kwenye mazungumzo hayo mjini Lausanne, Uswisi, kililiambia shirika la habari la Reuters kwamba kwa hali ilipofikia, kuna uwezekano wa kupatikana makubaliano kamili endapo pande zote zitaonesha dhamira njema.

Kwa mujibu wa chanzo hicho, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Frank-Walter Steinmeier na mwenzake wa Ufaransa, Laurent Fabius, walikubaliana uratibu wa pamoja kabla Fabius kuondoka Lausanne kurejea Ufaransa usiku wa jana.

Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, Philip Hammond, amesema mazungumzo hayo yamefanikiwa hadi sasa kuweka utaratibu mpana wa maelewano, ingawa alikiri kuwa bado imebakia kazi kubwa ya kufanywa.

"Baadhi ya mambo ni ya undani na ya kitaalamu sana, kwa hivyo hayo yanahitaji kufanyiwa kazi kwa undani zaidi lakini ndiyo kazi tuliyonao sasa na tutaendelea kuifanya." Hammond aliliambia shirika la habari la AP.

Waziri wa Mamo ya Nje wa Iran, Muhammad Javad Zarif, akielekea kwenye kikao cha mkutano.

Waziri wa Mamo ya Nje wa Iran, Muhammad Javad Zarif, akielekea kwenye kikao cha mkutano.

Mawaziri hao wa mambo ya nje, akiwamo John Kerry wa Marekani, wameendelea na mazungumzo hadi alfajiri ya leo kabla ya kwenda mapumziko, wakitarajiwa kurejea tena mchana wa leo. Mawaziri wa mambo ya nje wa Urusi na China waliondoka kabla mjini Lausanne na kuwaachia wasaidizi kuwawakilisha kwenye sehemu iliyobakia, huku Sergei Lavrov akisema angelirejea lau makubaliano yangelifikiwa.

Marekani yasema hatua zilizopigwa ni kubwa

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Marekani, Marie Harf, amesema kuna hatua kubwa zilizokwishapigwa na ambazo zinahalilisha kuongezwa muda angalau kwa siku moja, ingawa kuna baadhi ya mambo ambayo ni magumu sana.

Awali Kerry alikuwa amepanga naye kuondoka jana, lakini akabadilisha ratiba yake na kuendelea kubakia.

Kwa upande wake, ujumbe wa Iran kwenye mazungumzo hayo umesema utaendelea kubakia Lausanne kadiri inavyohitajika ili kuyasawazisha masuala yote yanayokwamisha kufikiwa makubaliano.

Suala la urutubishaji wa madini ya uranium linaonekana kuwa gumu zaidi, huku Iran ikishikilia haja ya kufanya hivyo kwa matumizi ya nishati, sayansi, viwanda na matibabu, lakini mataifa mengine yakiwa na wasiwasi kuwa inaweza kutumia teknolojia hiyo kuunda silaha za kinyuklia.

Ikiwa makubaliano yatafikiwa kama inavyotegemewa, Iran itaondolewa vikwazo vya kiuchumi na kisiasa, ambavyo vimeuathiri vibaya uchumi wa taifa hilo linalotegemea biashara ya mafuta.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AP/Reuters/AFP
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman

DW inapendekeza

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com