1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroUkraine

Mazungumzo ya amani kati ya Urusi na Ukraine yaathirishwa

Wakio Mbogho11 Machi 2026

Juhudi za kimataifa za kusaka suluhisho la kidiplomasia katika vita kati ya Urusi na Ukraine zinaendelea, huku hali ya mapigano kwenye uwanja wa vita inazidi kuwa ngumu.

https://p.dw.com/p/5A9Zr
Uswisi, Geneva 2026 | Ujumbe wa Urusi wakati wa mazungumzo ya pande tatu na Marekani na Ukraine
Marekani imependekeza duru nyingine ya mazungumzo kati ya Urusi na Ukraine, yakiongozwa na Washington, kuhusu kumaliza miaka minne ya vita wiki ijayo, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky alisema JumannePicha: Yekaterina Chesnokova/ITAR-TASS/IMAGO

Jitihada hizo zimepata changamoto baada ya Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky kusema kuwa mazungumzo yaliyokuwa yafanyike wiki hii yameahirishwa hadi wiki ijayo. Afisi ya rais Zelensky ilitangaza kuwa mazungumzo hayo yanatarajiwa kufanyika nchini Uswisi au Uturuki, ambayo tayari imejitolea kuwa mwenyeji.

"Mazungumzo ya amani yalikuwa yamepangwa kufanyika Jumanne na Jumatano nchini Uturuki. Nimezungumza na Rais Reccip Erdoğan (wa Uturuki). Vita vya Mashariki ya Kati ni changamoto kwa wote, lakini bado kila mtu anakubaliana kuwa mazungumzo ya kumaliza vita nchini Ukraine ni muhimu. Tulikuwa tayari kwenda Uturuki, lakini upande wa Marekani ndio uliochelewesha mkutano huo wakisema tufanye wiki ijayo", alisema Zelensky.

Wakati juhudi za mazungumzo zikiendelea, hali ya mapigano inaendelea kuwa tete. Ukraine inadai imefanikiwa kuwasukuma nyuma wanajeshi wa Urusi katika baadhi ya maeneo ya mstari wa mbele na kurejesha maeneo kadhaa ya kusini mashariki mwa nchi. Hata hivyo, madai hayo hayajathibitishwa kikamilifu.

Kwa upande wake, Rais wa Urusi Vladimir Putin anasisitiza kuwa majeshi yake yanaendelea kupata mafanikio katika eneo la Donbas mashariki mwa Ukraine, na kwamba Moscow iko tayari kuendelea kutumia nguvu iwapo mazungumzo yatashindwa.

Mashambulizi ya kijeshi na droni yaendelea

Mashariki mwa Ukraine inayokaliwa na Urusi, Donetsk 2026 | Gari lililoharibika mbele ya hospitali ya watoto baada ya mashambulizi ya risasi/mabomu
Watu kadhaa waliuawa katika shambulio la kombora la Ukraine kwenye mji wa Bryansk nchini Urusi, mamlaka za Urusi zilisema JumannePicha: Alexander Ermochenko/REUTERS

Wakati huo huo, mashambulizi ya pande zote mbili yameendelea kusababisha vifo na uharibifu. Mabomu ya Urusi yamepiga mji wa Sloviansk mashariki mwa Ukraine na kuua watu kadhaa, huku mashambulizi ya droni yakijeruhi wengine katika miji mingine.

Ukraine nayo imedai kushambulia kiwanda muhimu cha vifaa vya makombora katika eneo la Bryansk nchini Urusi, kwa kutumia makombora ya masafa marefu aina ya Storm Shadow. Mamlaka za Urusi zimesema shambulio hilo limesababisha vifo vya raia na majeruhi kadhaa.

Zelensky pia ameonya mataifa ya Magharibi kutolegeza vikwazo dhidi ya Urusi, hasa katika sekta ya mafuta, akisema hatua hiyo inaweza kuisaidia Moscow kufadhili vita na kudhoofisha msimamo wa Kyiv.

Kwa sasa, mzozo mpya wa vita Mashariki ya Kati unaonekana kuvuta umakini wa dunia na kuathiri kasi ya juhudi za kidiplomasia kuhusu Ukraine.

Hata hivyo, viongozi wa kimataifa wanaendelea kusisitiza umuhimu wa mazungumzo ili kumaliza moja ya migogoro mikubwa zaidi barani Ulaya tangu Vita Vikuu vya Pili vya Dunia.