Matumaini kutenzua mgogoro wa Mashariki ya Kati | Matukio ya Kisiasa | DW | 18.11.2008
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Matumaini kutenzua mgogoro wa Mashariki ya Kati

Rais wa Israel Shimon Peres akiwa ziarani Uingereza amesema, ana matumaini mema kuwa makubaliano ya amani yatapatikana katika kipindi cha miezi 12 ijayo,kufuatia uchaguzi wa Barack Obama kama kiongozi mpya wa Marekani.

Kwa maoni ya Rais Shimon Peres kuna nafasi nzuri ya kupatikana makubaliano ya mwisho ya amani katika Mashariki ya Kati,majadiliano na Wapalestina yatakapokamilishwa. Amesema,hakuna haja ya kuishinikiza Israel kutafuta amani kwani kwa hiyari,Israel imechagua kufuata njia hiyo.Ingawa katika siku za hivi karibuni hakuna maendeleo makubwa yaliyofanywa katika majadiliano hayo,Waziri Mkuu wa Israel Ehud Olmert anaeondoka madarakani amekubali kuwaachilia huru wafungwa 250 wa Kipalestina kama ishara ya nia njema baada ya kukutana na Rais wa Wapalestina Mahmoud Abbas siku ya Jumatatu.Lakini majadiliano hayo yalifanywa chini ya kivuli cha machafuko mapya yaliyozuka katika Ukanda wa Gaza unaodhibitiwa na kundi la Hamas.

Tangu majuma mawili yaliyopita, vikosi vya Israel na wanamgambo wa Kipalestina kutoka Gaza wanapambana takriban kila siku.Mapigano hayo yamesababisha vifo vya Wapalestina 15.Tarehe 5 Novemba Israel ilijibu mashambulizi ya wanamgambo wa Hamas kwa kuufunga kabisa mpaka wa Gaza na kuzuia usafirishaji wa mahitaji ya kila siku.Lakini kufuatia shinikizo la kimataifa, Israel juma lililopita iliruhusu mlolongo wa magari kusafirisha sehemu ya mahitaji ya mafuta katika mtambo pekee wa nishati kwenye Ukanda wa Gaza.Na jana Jumatatu mlolongo wa magari 33 uliruhusiwa kupeleka misaada ya kiutu.Nusu ya Wapalestina milioni 1.5 wanaoishi katika Ukanda wa Gaza wanategemea kulishwa na UNRWA-shirika la kimataifa linalohudumia wakimbizi duniani.Raia wa kawaida wanaendelea kuteseka na kuwa wahanga wa mapambano yanayozuka kati ya vikosi vya Israel na wanamgambo wa Hamas,huku misaada ya kiutu ikitiwa hatarini.

Rais Peres alieanza ziara yake ya siku tatu nchini Uingereza leo hii, alipoulizwa iwapo msimamo wa Hamas ni kizuzi kwa mchakato wa amani alisema,chama hicho hakisaidii kutekeleza matakwa ya Wapalestina.Kwa maoni yake,Hamas kinawazuia Wapalestina kuwa na taifa lao wenyewe. Hata hivyo amesema,anaamini kuwa kuna nafasi nzuri kwa makubaliano ya amani kupatikana kati ya Israel na Wapalestina katika kipindi cha miezi kumi na mbili ijayo.

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com