1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Matokeo ya uchaguzi mkuu bado yasubiriwa Tanzania

3 Novemba 2010

Waangalizi wa kimataifa watoa wasiwasi wao kuhusu utaratibu wa kutangaza matokeo

https://p.dw.com/p/Pwrh
Waangalizi wa Jumuiya ya MadolaPicha: AP

Chama tawala nchini Tanzania CCM kimesema kinataraji kupata ushindi mkubwa katika uchaguzi wa urais na wa bunge uliofanyika Jumapili iliyopita nchini humo. Hata hivyo waangalizi wa kimataifa wameelezea wasiwasi wao kuhusiana na utaratibu wa kuhesabu kura. Kwa siku ya pili polisi walitumia mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya wafuasi wa upinzani waliokuwa wanalalamikia kucheleweshwa kutolewa kwa matokeo mjini Dar es Salaam na katika maeneo mengine nchini Tanzania.

Tansania Sansibar Wahl Wahlen Polizei CUF
Polisi wakishika doria Visiwani ZanzibarPicha: AP

Mapema, mgombea wa urais aliyeshindwa Visiwani Zanzibar, Seif Sharif Hamad, alisema uchaguzi huo ulikuwa na walakin lakini akakubali atachukua wadhfa katika serikali ya muungano visiwani humo ili kuzuia machafuko yaliyotokea katika chaguzi mbili zilizopita visiwani Zanzibar.

Kiongozi wa kundi la waangalizi wa Umoja wa Ulaya David Martin alisema walikuwa na wasiwasi kuhusiana na utaratibu wa kutolewa matokeo. Hata hivyo mwenyekiti wa tume ya kitaifa ya uchaguzi nchini Tanzania Lewis Makame ameondoa wasiwasi akisema hadi kesho matokeo yote yatakuwa yametolewa.

Tansania Sansibar Wahl Wahlen Opposition CUF
Watanzania bado wasubiri matokeo ya uchaguziPicha: AP

Meneja wa Kampeni wa CCM Abdulrahman Kinana amesema wanatarajia kupoteza viti 51 kwa upinzani lakini hawana shaka watashinda uchaguzi.