Mashirika ya haki za binaadamu yashinikiza kufungwa kwa Guantanamo | Matukio ya Kisiasa | DW | 11.11.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Mashirika ya haki za binaadamu yashinikiza kufungwa kwa Guantanamo

Rais mteule wa Marekani Barack Obama anapaswa kulipa kipau mbele cha juu suala la kufungwa kwa gereza la Guantanamo wakati atakapoingia madarakani hapo tarehe 20 mwezi wa Januari mwakani.

default

Ishara ya Rais Mteule wa Marekani Barack Obama akiwaza kufunga kambi ya Guantanamo.

Mashirika ya haki za binaadamu yamesema hayo pamoja na kutowa wito wa kufutwa kwa tume za kijeshi ambazo zimeanza kuendesha kesi dhidi ya watuhumiwa wa ugaidi wanaoshikiliwa huko Guantanamo. Mashirika hayo ya kutetea haki za binaadami yamekuwa yakitaka watuhumiwa hao wa ugaidi wanaoshikiliwa huko Guantanamo kesi zao kuhamishiwa katika mahkama za Marekani ambapo mchakato unaotakiwa wa kuwapa utetezi utaimarisha nafasi ya kuhukumiwa kwa haki.

Anthony Romero mkurugenzi mtendaji wa Umoja wa Uhuru wa Kiraia nchini Marekani amesema hakuna nafasi ya subira au kucheleweshwa katika nyanja hizo.Kundi lake ni mojawapo lililokuwa limejihusisha mno katika mahkama juu ya hatima ya mahabusu wa Guantanamo.

Ameongeza kusema kwamba wanatumai rais mteule Barack Obama mara tu baada ya kuapishwa atachukuwa hatua ya kijasiri na kusaini agizo kuu la rais kuamuru kufungwa kwa Guantanamo na kukomesha tume za kijeshi za ulaghai zinazoendesha kesi huko Guantanamo.

Romero anasema wakati umefika kurudisha maadili ya kisheria na haki za binaadamu ya Marekani.

Makundi mengine matano yamekuwa yakizihimiza serikali za Ulaya kukubali kuwapokea wafungwa wa Guantanamo ambapoi kwa hivi sasa kuna takriban 50 ambao hawatofunguliwa mashtaka yoyote yale ya uhalifu lakini hawawezi kurudishwa nchini mwao kwa hofu ya kufungwa na kuteswa.

Joanne Mariner mkurugenzi wa kitengo cha Ugaidi na Kupiga Vita Ugaidi katika shirika la haki za binaadamu la Human Right Watch kwa niaba ya Shirika la Kimataifa la Haki za Binaadamu Amnesty International,Kituo cha Haki za Kikatiba na shirika la Reprieve pamoja na Shirikisho la Kimataifa la Haki za Binaadamu lenye makao yake mjini Paris Ufaransa amesema Rais mteule Obama amejizatiti kutaka kufunga Guantanamo lakini atahitaji msaada wa Ulaya kwamba serikali za Ulaya zinaweza kutowa msaada mkubwa unaohitajika kwa kukubali kuwapokea baadhi ya mahabusu ambao hawawezi kurudishwa makwao.

Tokea watuhumiwa wa mwanzo au kama vile walivyoelezewa na aliekuwa waziri wa ulinzi wa Marekani Donald Rumsfeld kuwa ni wabaya kabisa miongoni mwa wabaya walipofikishwa huko kutoka Afghanistan hapo Januari 11 mwaka 2002 jumla ya watu 775 wenye umri kati ya miaka 13 hadi miaka 98 walishikiliwa katika kambi ya Guantanamo.

Sehemu kubwa ya watuhumiwa hao hivi sasa inaonekana kuwa walikuwa hawana hatia ya harakati za kigaidi na walikamatwa na wanamgambo wa kikabila na wale wenye kutafuta bakshishi nchini Afghanistan na Pakistan.Licha ya kutokuwa na hatia wengi wa wafungwa hao walikabiliwa na mbinu mbaya za usaili ambazo makundi ya haki za binaadamu yameshutumu kuwa ni mateso pamoja na vitendo vyengine vya dhuluma kabla na baada ya kufikishwa huko.

Mashirika hayo yamelifanya suala la Guantanamo pamoja na kutendewa vibaya kulikoorodheshwa pamoja na picha kutoka gereza la Abu Ghraib nchini Iraq kuwa alama ya matumizi ya nguvu kupindukia ya vita vya Bush dhidi ya ugaidi na kupotea kwa msimamo wa uadilifu wa Marekani.

Takriban wafungwa wanne walijiuwa huko Guantanamo na mamia walishiriki katika migomo ya kula mara kwa mara kupinga hali ya mazingira ambayo kwayo wanashikiliwa.

Zaidi ya wafungwa 500 wameachiliwa huru wengi wao wakirudishwa makwao baadhi yao chini ya masharti kwamba nchi inazowapokea itaendelea kuwashikilia au kuwaweka chini ya uchunguzi.

Wakati wa kampeni yake ya kugombania urais wa Marekani Obama alirudia mara kwa mara kusema jinsi sura ya Marekani nchi za nje kama kiongozi wa haki za binaadamu na mfano wa kuigwa wa utawala wa sheria ilivyoharibika kutokana na Guantanamo ambayo ameuita ukurasa wa kusikitisha katika histroria ya Marekani na kuahidi mara kadhaa kuifunga kambi hiyo.

 • Tarehe 11.11.2008
 • Mwandishi Mohamed Dahman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Frrz
 • Tarehe 11.11.2008
 • Mwandishi Mohamed Dahman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Frrz
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com