Mashindano ya ubingwa wa riadha. | Michezo | DW | 28.07.2010
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Michezo

Mashindano ya ubingwa wa riadha.

Mashindano ya riadha barani Afrika yaanza Kenya.

Wanariadha wakishiriki katika mashindano ya mabingwa barani Ulaya huko Barcelona.

Wanariadha wakishiriki katika mashindano ya mabingwa barani Ulaya huko Barcelona.

Zaidi ya wanariadha 700 wamekutana jijini Nairobi nchini Kenya katika mashindano ya siku tano barani Afrika yalioanza rasmi hii leo. Vigogo wa Kenya na Ethiopia wamewasilisha wakimbiaji wao maarufu wakiwemo Viviane Cheruiyot kwa upande wa wanawake kutoka Kenya na mshindi mara mbili wa Olimpiki Tirunesh Dibaba kutoka Ethiopia ambaye anarudi tena ulingoni baada ya mapumziko ya muda.

Kenya inaandaa mashindano hayo kwa mara ya kwanza na ina kikosi cha wanariadha 144 wakiwemo wanariadha wa mbio fupi,na washindani wa michezo mingine uwanjani, ambao katika siku za nyuma, wamekuwa wakilalamika kusahaulika kutokana na uhaba wa fedha kutoka shirika la riadha nchini humo - AK.

Kocha mpya wa timu hiyo Stephen Mwaniki ,anaamini kuwa kushiriki kwa wanariadha hao katika mashindano mengine kando na mbio ndefu ambayo kenya inasifika kwayo, kutasaidia kuimarisha na kutambulika zaidi kwa timu hiyo.

Wanariadha wengi wanatarajiwa kutumia mashindano haya kujitayarisha kwa mashindano yajayo ya Commonwealth yatakayo fanyika mwezi Octoba huko New Delhi ,India.

Timu hiyo ya Kenya inaweka matumaini yake kwa mwanariadha Viviane Cheruiyot, ambaye aliweka rekodi ya muda wa dakika 14 sekundi 27.41 katika mashindano ya ligi ya Paris Diamond, yaliokamilika wiki iliyopita na ambayo ameyatumia kufanyia mazoezi kwa mashindano haya ya mabingwa barani Afrika.

Huku Ethiopia ikiwa na matumaini makuu ya ushindi, kufuatia kuwepo nyota Tirunesh Dibaba, ambapo utakumbukwa ushindi uliopata Kenya katika mashindano yaliopita ya msimu wa joto hapa Ujerumani katika mji wa Berlin, kwa kukosa kushiriki kwake.

Huku nayo Nigeria inatarajia kuongoza katika mashindano haya hata baada ya kutoshiriki mwanariadha wake mashuhuri Olusoji Fasuba.

Mashindano hayo yanafanyika katika uwanja wa taifa uliokarabatiwa upya wa Nyayo katikati mwa jiji hilo kuu.

Usalama umeimarishwa kufuatia tukio la tarehe 11 mwezi Julai katika nchi jirani ya Uganda na kundi la kigaidi la Al Shabaab, lililosababisha mauaji ya watu takriban 76.

Kwengineko mashindano sawa barani Ulaya yakiingia siku yake ya pili hii leo huko Barcelona, Marcin Lewandoski kutoka Poland ameibuka wa kwanza kwa muda wa dakika 1 sekundi 49.78 katika mashindano ya wanaume ya mita 800. Hamid Oualich wa Ufaransa alimfuata nyuma huku Mhisapania David Bustos akiibuka wa tatu katika mbio hizo.

Na katika mbio za kuruka vihunzi mita 400 kwa wanaume, Aleksandr Derevyagin kutoka Urusi ameshinda katika muda wa sekundi 50.14 huku Fadil Bellaabous wa Ufaransa akiwa wa pili na Nathan Woodward kutoka Uingereza akimaliza watatu.

Mashindano hayo yanakamiliki Agosti mosi mwaka huu.

Mwandishi :Maryam Abdalla/AFPE

Mhariri:Josephat Charo