Mashaka yatawala makubaliano ya usitishaji mapigano Syria | Matukio ya Kisiasa | DW | 17.09.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Mashaka yatawala makubaliano ya usitishaji mapigano Syria

Mashaka yametanda juu ya uwezekano wa kufikishwa msaada nchini Syria, wakati ambapo makubaliano yaliyofikiwa kati ya Marekani na Urusi na kuanza kutekelezwa nchini kote wiki hii yakikumbwa na ukiukaji zaidi.

Serikali na waasi wameripotiwa kushiriki mapigano makali karibu na mji mkuu Damascus, limesema shirika la uangalizi wa haki za binadamu. Raia waliuawa katika mashambulzi ya ndege za kivita ambazo hazikutambuiwa katika mkoa unaodhibtiwa na waasi wa Idlib, kaskazini-magharibi mwa Syria, liliongeza shirika hilo.

Shirika la habari la serikali ya Syria SANA, lilisema kanisa moja katika eneo la Aleppo linalodhibtiiwa na serikali, liliharibiwa baada ya waasi kufyatua roketi katika ukiukaji wa makubaliano hayo yaliyoanza kutekelezwa siku ya Jumatatu.

Urusi, ambyo ni mshirika muhimu wa rais wa Syria Bashar al-Assad, ilisema iko tayari kurefusha kwa siku tatu zaidi, usitishaji mapigano, ambao awali ulikuwa umepangwa kudumu kwa wiki moja.

Lakini iliongeza kuwa ili kufanya hivyo, Marekani inahitaji kuhakikisha kuwa makundi ya waasi inayowaunga mkono hauwakiuki makubaliano hayo, Jenerali wa Urusi Viktor Poznikhir aliliambia shirika la habari la serikali ya Urusi TASS.

Marekani ilisema ilitaka maendeleo ya wazi kabla ya kuanza kwa hatua zinazofuata za utekelezaji wa makubaliano ya usitishaji mapigano. Memaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani John Kirby alisema kilichoafikiwa wiki iliyopita mjini Geneva, ikiwa ni pamoja na kituo cha pamoja cha utekelezaji, "hakitotekelezwa hadi pale Urusi itakapotumia ushawishi wake kwa Syria.

Schweiz US Premierminister John Kerry und russischer Aussenminister Sergei Lavrow

Mawaziri wa Mambo ya nje wa Marekani, John Kerry na Urusi Sergei Lavrov walipotangaza makubaliano ya kusitisha mapigano Syria wakiwa mjini Geneva wiki iliopita.

"Urusi ina maamuzi ya kufanya kuhusu ushawishi walio nao kwa Assad na kiwango ambacho wanakwenda kuutumia au kutoutumia," Kirby alisema. Ikiwa watatumia ushawishi wao na hauna ufanisi, basi mpango huo hautatekelezwa na kwa masikito tutarejea tulipokuwa kwa muda mrefu, ambako ni kushambuliwa kwa raia kwa kutumia mabomu ya mapipa na gesi," alisema Kirby.

Mapambano karibu na Damascus

Mapema siku ya Ijumaa, waasi na vikosi vya serikali walishiriki mashambulizi makubwa nje ya mji wa Damascus, na kusababisha kuuawa kwa wapiganaji wasiopungua wawili.

Karibu dazen mbili za maroketi na magruneti vilifyatuliwa karibu na kijiji cha Jobar, mashariki mwa Damascus, lilisema shirika la uangalizi wa haki za binaadamu lenye makao yake mjini London Uingereza, na kuongeza kuwa makombora mawili yaliangukia katika mji wa kale, unaodhibitiwa na serikali.

Mapambano yalikuwa yakiendelea katika maeneo yasiopungua mawili, ambapo vikosi vya serikali vilikuwa vinawashambulia waasi, lilisema shirika hilo la uangalizi wa haki za binaadamu. Televisheni ya taifa ya Syria ilisema vikosi vya serikali vilizuwia shambulizi la waasi.

Kundi la waasi wa Kiislamu la Faylaq al-Rahman, lilisema katika ujumbe uliowekwa kwenye ukurasa wake wa twita, kwamba kulikuwa na mapambano makali Jobar, na kwamba wapiganaji wake wamewauwa wanajeshi kadhaa wa serikali.

Haikubainika nani alianza kukiuka makubaliano ya usitishaji mapigano, ambayo yamekuwa yakiheshimiwa kwa sehemu kubwa licha ya ukiukaji wa hapa na pale. Siku ya Alhamisi serikali ilisema raia wawili waliuawa, vikiwa vifo vya kwanza tangu kuanza usitishaji huo.

Urusi imeulaumu ukiukaji huo kwa waasi, wakati upinzani ukivituhumu vikosi vya Assad kwa kuvunja masharti ya makubaliano. Jobar ni sehemu ya mkoa wa Ghouta, ambao unashikiliwa kwa sehemu kubwa na makundi ya waasi, yakiwemo yale ya msimamo mkali. Makundi yenye mahusiano na Al-Qaeda yalio na uwepo katika eneo hilo, hayamo katika makubaliano ya usitishaji mapigano.

Siku ya Alhamisi vikosi vya serikali vilianza kuondoka kutoka barabara ya Castello, ambayo ni njia muhimu kuelekea eneo la waasi lililozingirwa la Aleppo Mashariki. Dazen kadhaa za magari yaliobeba msaada wa Umoja wa Mataifa zilizotaka kufikia maeneo yaliyozngirwa nchini Syria ziliendelea kukwaama katika mpaka wa Uturuki siku ya Ijumaa.

Syrien Friedensverhandlungen in Genf Staffan de Mistura

Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Syria Staffan de Mistura, ameilaumu serikali ya Assad kwa kuzuwia misaada.

De Mistura aunooshea kidole cha lawama utawala wa Assad

Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Syria Staffan de Mistura ameelekeza lawama kubwa za ucheleweshwaji wa kufikisha msaada kwa serikali ya Assad, ambayo bado haijatoa barua zozote zinazojulikana kama za uwezeshaji kwa magari ya misaada kuvuka maeneo ya mapigano.

Kaskazini mwa Syria, idadi kadhaa ya vikosi maalumu vya Marekani vinatarajiwa kusaidia mashambulizi ya Uturuki kufuatia maombi ya serikali mjini Ankara, alismea msemaji wa wizara ya ulinzi ya Mrekani Pentagon siku ya Ijumaa.

Msemaji huyo aliliambia shirika lahabari la Ujerumani dpa, kwamba wanajeshi hao tayari wamepelekwa, na kuongeza kuwa watavisaidia vikosi vya jeshi la Uturuki na waasi wenye msiamamo wa wastani kulikomboa eneo la mpakani kutoka mikononi mwa kundi la Dola la Kiislamu.

Mkutano wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa uliokuwa umepanga kufanya siku ya Ijumaa mjini New York kujadili suala hilo ulifutwa, huku Urusi ikiishutumu Marekani kwa kukataa kuziwasilisha kwa baraza la usalama, nyaraka zinazoainisha makubaliano ya pamoja yanayonuwia kusimamisha mapigano nchini Syria.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/adpe, afpe, ape

Mhariri: Isaac Gamba

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com