1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani na Iran zatishiana kuhusu maandamano ya Tehran

Amina Abubakar ap/afp/reuters
2 Januari 2026

Rais wa Marekani Donald Trumo na maafisa wakuu wa Iran, wametupiana maneno ya vitisho, huku maandamanao makubwa ya kupinga hali ya kiuchumi katika Jamhuri hiyo ya kiislamu yakizidi kutanuka.

https://p.dw.com/p/56Eyc
Bendera | za Marekani na Iran
Trump na maafisa wakuu wa Iran watishiana kuhusu maandamano yanayoikumba IranPicha: Dado Ruvic/REUTERS

Waandamanaji na maafisa wa Usalama walipambana katika miji kadhaa ya Iran hapo jana (01.02.2026) huku watu sita wakidaiwa kuuwawa. Haya yakiwa mauaji ya kwanza kuripotiwa tangu kuanza kwa maandamano hayo.

Wamiliki wa maduka katika mji Mkuu Tehran waliandamana kupinga kupanda kwa gharama za bidhaa na kutoimarika kwa uchumi. Maandamano hayo yaliogeuka na kuwa ya kisiasa pia yalisambaa kote nchini humo.

Baada ya mauaji hayo kuripotiwa rais wa Marekani Donald Trump aliandika katika mtandao wake wa X kwamba, iwapo Iran itaendelea kuwapiga risasi na kuwaua waandamanaji kama ilivyozoea, nchi yake ipo tayari kuingilia kati kuwaokoa waandamanaji hao aliyowaita wa amani.

Kauli hiyo ilipelekea mkuu wa bodi ya usalama ya Iran Ali Larijani kutoa onyo kali kwa Trump kwamba hatua ya Marekani kuingilia suala lake la ndani ni sawa na kuiyumbisha kanda nzima na kuharibu masilahi ya Marekani.

Tehran 2025 | Ali Larijani
Mkuu wa bodi ya usalama ya Iran Ali Larijani Picha: Courtney Bonneau/SIPA/picture alliance

Larijani pia aliandika katika mtandao wake wa X kwamba,  Trump anapaswa kuwa makini na usalama wa wanajeshi wake. Tamko lake linagusia hatua ya Marekani kuwepo katika mizozo mengi ya eneo hilo. Mwezi Juni Marekani iliishambulia kambi ya jeshi la anga ya Al Udeid huko Qatar baada ya Marekani pia kushambulia vinu vitatu vya nyuklia vya Iran  wakati wa vita vya Israel na Tehran vilivyodumu siku 12.

Shamkhani: Uchokozi wowote dhidi ya Iran utajibiwa haraka

Kwa upande wake Ali Shamkhani mshauri wa kiongozi wa juu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei alisema uchokozi wowote dhidi ya nchi yake utajibiwa haraka na kwa hatua kali, akisema usalama wa Iran ni mstari mwekundu usiopaswa kuvukwa.

Maandamano ya Iran yaliyoingia siku yake ya sita hii leo (02.02.2026) yamekuwa makubwa nchini humo tangu mwaka 2022 wakati wa maandamano ya kupinga kifo cha msichana wa miaka 22 Mahsa Amini kilichotokea akiwa kizuizini, baada ya kukamatwa kwa kosa la kutokuvalia hijabu.

 Iran Kuhdasht 2026 | Maandamano dhidi ya serikali
Maandamano ya kupinga kupanda kwa gharama za maisha na uchumi mbaya yafanyika IranPicha: UGC

Katika siku za hivi karibuni, viongozi wa Iran akiwemo Larijani na rais Pezeshkian wameyaelezea maandamano ya amani dhidi ya uchumi wa Iran kama maandamano halali na yanayoeleweka.

Lakini licha ya utambuzi huo, maafisa katika utawala huo wameonya kuwa kutakuwa na majibu makali kwa hatua zozote za kuchafua utulivu uliopo Iran.

Hii leo muendesha mashitaka wa mji wa Lorestan, Ali Hasavand, alinukuliwa katika tovuti ya Mahakama ya Mizan kwamba, ushiriki wowote wa mkusanyiko usio halali na hatua yoyote inayolenga kuleta machafuko, kuharibu mali za umma na kutoheshimu sheria kutachukuliwa kama kosa la uhalifu na litapata pia majibu makali.